28.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 21, 2024

Contact us: [email protected]

HARUSI YA PROFESA J YAWAUNGANISHA CCM, UKAWA

Na VERONICA ROMWALD-DAR ES SALAAM


WABUNGE wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wa upinzani, hasa wale wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wameweka tofauti zao pembeni na kujumuika pamoja katika harusi ya Mbunge wa Mikumi, Joseph Haule (Chadema).

Mbunge huyo, maarufu kwa jina la Profesa J, mwishoni mwa wiki alifunga ndoa takatifu na mchumba wake, Grace Mgonjo, katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph, jijini Dar es Salaam.

Profesa J, ambaye amejizolea umaarufu mkubwa ndani na nje ya Tanzania kupitia muziki wa hip hop, alionekana mwenye furaha wakati wote tangu alipokuwa kanisani hadi ukumbini pamoja na mkewe, Grace.

Wabunge wa CCM walihudhuria kwa wingi katika harusi hiyo na kuzua gumzo katika mitandao mbalimbali ya kijamii, huku wengine wakisifu tukio hilo kuwaweka pamoja mahasimu hao wa kisiasa wanapokuwa bungeni.

Orodha ya wabunge hao wa CCM ni pamoja na Rashid Shangazi (Mlalo), Edwin Sanga (Kondoa Mjini), Stanislaus Mabula (Nyamagana) pamoja na Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Shinyanga, Lucy Mayenga, Sixtus Mapunda (Mbinga Mjini) na Mussa Ntimizi (Igalula), huku wale wa Ukawa wakiongozwa na Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini), Joseph Mbilinyi au ‘Sugu’ (Mbeya Mjini), Godbless Lema (Arusha Mjini) na James Mbatia (Vunjo).

Harusi hiyo ya aina yake ilihudhuriwa pia na wanachama na viongozi mbalimbali wa Chadema, wakiwamo Waziri Mkuu Mstaafu,  Edward Lowassa na mkewe, Regina Lowassa, Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.

Akihojiwa na kituo kimoja cha televisheni nje ya viwanja vya kanisa hilo la Mtakatifu Joseph, Profesa J alisema anamshukuru Mwenyezi Mungu kumpa neema ya kufanikisha suala hilo.

“Grace ni mchumba wangu ambaye nimekuwa naye kwa muda mrefu, takribani miaka 13 sasa, leo ni siku ya kipekee kwetu, tumeweza kutimiza ndoto yetu ya kufunga ndoa,” alisema.

Baadaye msafara wa maharusi hao uliondoka katika eneo la kanisa na kuelekea katika Hoteli ya Serena na jioni walielekea katika Ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.

Wabunge hao waliingia kwa mbwembwe ndani ya ukumbi huo, wakicheza nyimbo mbalimbali na kuamsha shangwe, nderemo na vifijo kutoka kwa wageni waalikwa.

Baadaye Profesa J, mkewe na wapambe wao waliingia rasmi ukumbini, huku akiimba wimbo wake wa ‘Kamili Gado’, uliowahi kutamba miaka ya hivi karibuni.

Hali hiyo ilizidisha furaha kwa wageni waalikwa, ambao walishindwa kujizuia na kuamua kutoka kwenye viti vyao na kujumuika katikati ya ukumbi kucheza pamoja na maharusi hao.

Akizungumza kwenye sherehe hiyo, Mbowe alimpongeza mbunge huyo: “Nawatakiwa maisha mema wewe na familia yako na ndugu zako pia, umeona leo jinsi wabunge wa vyama vyote walivyokuunga mkono katika hafla hii.

“Ni kwa sababu wanakuthamini, wanakuheshimu, umekuwa ni mbunge mwenye heshima na hekima, japo ni mjanja sana”.

Kwa upande wake, Mbunge wa Dodoma Mjini, Antony Mavunde (CCM), ambaye pia ni Naibu Waziri wa Wizara ya Kazi, Vijana na Ajira, alisema: “Nawapongeza sana kama alivyosema kaka yetu Mbowe, hii ni hatua kubwa sana ambayo mmefikia, nawatakia kila la heri katika maisha yenu, sisi marafiki zako tumefurahi kwa hatua hii kubwa mliyofikia”.

Mbatia, kwa upande wake, aliwausia wawili hao kuendelea kuishi kwa upendo na kuvumiliana katika maisha yao ya ndoa.

“Mithali 21:9, mstari huo unasema heri kuishi juu ya paa darini kabisa kuliko kuishi na mwanamke mgomvi ndani ya nyumba,” alisema Mbatia, wakati akinukuu kitabu cha Biblia.

Aidha, Profesa J akizungumza ukumbini humo, aliwashukuru wageni wote waliofika kujumuika naye.

“Kipekee nawashukuru mawaziri wakuu wastaafu, (Lowassa na Sumaye) na familia zao kwa kutenga muda kwa ajili yetu, imetupa nguvu na faraja kwamba tunajulikana na tunafahamika na tupo miongoni mwa watu wanaojulikana.

Wasanii maarufu walihudhuria harusi hiyo, wakiongozwa na Judith Wambura (Lady Jay Dee), Ambwene Yesaya (AY), Naseeb Abdul (Diamond Platinum) na kundi lake la WCB pamoja na Lucas Mhavile, maarufu Joti na wengine wengi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles