MANCHESTER, ENGLAND
BAADA ya Joe Hart kuwekwa benchi kwa michezo miwili ya mwanzo katika michuano ya Ligi Kuu England, mlinda mlango huyo wa klabu ya Manchester City, ameanza kuwaaga wachezaji wenzake ndani ya klabu hiyo.
Kocha mpya wa klabu hiyo, Pep Guardiola, aliweka wazi wiki iliyopita kwamba alikuwa hana mpango na mchezaji huyo tangu alipopewa taarifa ya kutaka kuchukua nafasi ya Manuel Pellegrin.
Japokuwa mlinda mlango huyo amekuwa na mchango mkubwa ndani ya kikosi hicho kwa kipindi chote, lakini ujio wa kocha huyo mpya umemfanya akose namba na tayari kocha huyo anatarajia kumalizana na mlinda mlango wa klabu ya Barcelona, Claudio Bravo, na tayari amewasili jijini Manchester kwa ajili ya vipimo.
Ujio wa Bravo umemuhakikishia kwamba hawezi kupata tena namba ndani ya kikosi hicho, hivyo usiku wa kuamkia leo amewaaga baadhi ya mashabiki wa klabu hiyo.
Mashabiki wameonekana kuwa na huzuni kutokana na mchezaji huyo kuwaaga na kocha Guardiola amedai kuwa hatakiwi kuingiliwa katika maamuzi kwa kuwa yeye anawajua wachezaji wake wote.
Inasemekana Jumanne wiki hii, Guardiola alirushiana maneno na kipa huyo wakati wa mazoezi ya pamoja, lakini Guardiola aliweka wazi kuwa hakuna lolote ambalo linaendelea kati yao na hakuna mgogoro wowote.
“Sina tatizo lolote na Hart, hata yeye anajua kwamba hakuna tatizo ambalo linaendelea na ninaamini anaweza kuendelea kucheza katika michezo ijayo.
“Siwezi kusema kama Hart anatakiwa kuondoka, lakini tunatakiwa kusubiri hadi ifikapo Agosti 31, ambapo dirisha la usajili litakuwa linafungwa, hapo ndipo tutajua nani anaondoka na nani anabaki,” alisema Guardiola.