Na Imani Nathaniel, Mtanzania Digital
Kampuni ya simu za mkononi ya Halotel Tanzania imeshika usukani mara ya tatu kwa kuwa na huduma ya intaneti yenye spidi ya kasi zaidi ukiliganisha na kampuni nyingine zinazotoa huduma.
Kwa mujibu wa ripoti ya robo ya tatu ya mwaka inayoishia Septemba iliyolotewa na Ookla, kampuni ya kimataifa inayofanya utafiti wa masoko ya mitandao ya simu na masuala ya uungaishi, Halotel imeongoza kwenye utafiti kwenye ripoti ya robo ya kwanza, pili na tatu mfululizo mwaka huu.
Kwa mujibu wa matokeo ya utafiti huo, spidi ya intaneti ya mtandao wa Halotel Tanzania kwa robo ya tatu ya mwaka huu ilikuwa na uwezo wa kupakua Megabyte (MB) 17.63 kwa sekunde, huku ikiicha kampuni ya Vodacom Tanzania yenye spidi ya kupakua Megabyte (MB) 13.63 kwa sekunde.
Spidi ya kampuni ya Airtel ambayo imeshika nafasi ya tatu kwa mujibu wa ripoti hiyo ni uwezo wa kupakua Megabyte 11.61 kwa sekunde, Tigo ilishika nafasi ya nne kwa kuwa na uwezo wa kupakua Megabyte (MB) 6.01 kwa sekunde huku TTCL ikifuatia ikiwa na spidi ya kupakua Megabyte 5.12 kwa sekunde.
Ripoti hiyo inaonyesha kwamba spidi ya kupakua ya Halotel ni kubwa zaidi ya wastani wa kitaifa wa Megabyte (MB)11.86 kwa sekunde kwa mitandao ya simu, na nusu ya uwezo wa kupakua kwa mitandao ambayo sio ya simu za mikononi ya Megabyte (MB) 33.17 kwa sekunde.
Katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka huu, Halotel pia iliongoza kwa kuwa na spidi ya kasi zaidi ya uwezo wa kupakua Megabyte (MB) 17.84 kwa sekunde, ikifuatiwa na Vodacom iliyokuwa na uwezo wa kupakua Megabyte (MB) 12.09 kwa sekunde na Airtel ikiwa ya tatu kwa uwezo wa kupakua Megabyte (MB) 10.60 kwa sekunde moja.
Ripoti hiyo pia inaonyesha kwamba, kwenye robo ya pili ya mwaka huu, Halotel pia iliongoza kwa kuwa na uwezo wa kasi zaidi wa kupakua Megabyte 17.12 kwa sekunde huku Vodacom Tanzania ikiwa ya pili kwa spidi ya kupakua Megabyte (MB) 14.42 kwa sekunde na Airtel ikashika nafasi ya tatu kwa kuwa na kasi ya kupakua Megabyte (MB) 10.24 kwa sekunde.
Kwa kupima uimara wa spidi wa kila mtoa huduma, katika robo ya tatu ya mwaka, uchambuzi wa utafiti wa soko la mitandao umesema kwamba Halotel iko katika kiwango cha juu kwa asilimia 79.9, ikifuatiwa na Vodacom yenye uimara wa asilimia 76.1, Airtel kwa asilimia 73.2, Tigo kwa asilimia 48.9 , huku TTCL ikiwa na uimara wa mtandao kwa asilimia 42.8.
Kwenye robo ya pili, Halotel pia iliongoza kwa kuwa na uimara mkubwa wa kimtandao kwa asilimia 80, ikifuatiwa na Vodacom iliyokuwa na asilimia 72.1. Hii inamaanisha kwamba uwezo wa kupakua na kuweka taarifa au kitu chochote kwenye mtandao kwa Halotel ni mkubwa zaidi ya watoa huduma wote.
Taarifa ya robo ya tatu iliyotolewa karibuni ya Mamlaka ya Mawasiliano Nchini (TCRA) imeonesha kwamba idadi ya wateja wa Halotel Tanzania imeongezeka na kufikia milioni 7.2 mwezi Septemba mwaka huu kutoka wateja milioni 7 mwezi robo ya pili ya mwaka iliyoishia June.
Halotel, ambayo hivi karibuni imenunua masafa ya 2600MHz toka TCRA yenye thamani ya dola za Marekani milioni 30.2 (takribani shilingi bilioni 70), imesema inatarajia kufikisha wateja milioni 10 hadi kufikia mwaka ujao.
Ripoti ya Ookla imeonesha kwamba mkoa wa Dar es Salaam ndio unaongoza kwa kuwa na spidi kubwa ya intaneti kwenye mitandao ya simu ukiwa na uwezo wa kupakua Megabyte (MB) 13.90 kwa sekunde, ikifuatiwa na Mwanza ambao una spidi ya kupakua Megabyte (MB) 13.45 kwa sekunde.
Ripoti hiyo pia imeonesha kwamba, mkoa wa Arusha unashika nafasi ya tatu kwa kuwa na mtandao wa simu wenye spidi ya kupakua Megabyte (MB) 11.29 kwa sekunde, ukifuatiwa na Mbeya yenye spidi ya kupakua Megabyte (MB) 11.13 kwa sekunde na Dodoma ina spidi ya kupakua Megabyte (MB) 7.28 kwa sekunde.