Na Renatha Kipaka, Kagera
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU) mkoani Kagera imebainisha kuwepo na malalamiko (164) katika kipindi cha Januari hadi Machi 31, 2022 kutoka katika Halmashauri zote za mkoa huo.
Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Kagera, John Joseph wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Bukoba Mei 23, mwaka huu amesema taasisi zinazolalamikiwa ni za umma na binafsi.
“Nitumie nafasi hii kusema kuwa idara zinazolalamikiwa kutokana na taarifa hii ni Halmashari malalamiko 108, idara ya fedha 45, idara ya elimu 10, Maendeleo ya Jamii 9, Ugavi 16, maji 6, idara ya afya 19, watendaji wa kata na vijiji 3 huku taarifa 56 zikihusu watu binafsi, taasisi za kifedha, mashirika binafsi (NGOs), polisi, mahakama, Tanesco pamoja na Chama Kikuu cha Ushirika Karagwe (KDCU).
“Mashauri mapya 6 yalifunguliwa mahakamani na kufanya jumla kufikia 51 yanayoendelea kusikilizwa mkoani Kagera huku mengine manne yakiwa tayari yametolewa uamuzi likiwamo la Takukuru Kagera ambapo imefanikiwa kushinda mashauri mawili,” amesema Josepha na kuongeza kuwa:
“Takukuru tumefanya tafiti nane yenye zaidi ya Sh Bilioni 7 katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Kagera ikiwa ni pamoja na ufuatiliaji wa ukarabati wa miradi ya maji, ujenzi wa hospitali, vituo vya afya pamoja na zahanati na katika miradi hii ilibainika kuwa na mapungufu ikiwemo kutumia vifaa vyenye ubora uliopendekezwa,” amesema Joseph.