Na Allan Vicent, Busega
Halmashauri ya wilaya ya Busega Mkoani Simiyu imedhamiria kuboresha sekta ya elimu katika kipindi cha miaka 5 ijayo ili kuinua kiwango cha elimu na ufaulu kwa watoto wa shule zote.
Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti mpya wa halmashauri hiyo, Sundi Mniwe alipokuwa akiongea na MtazaniaDigital wilayani humo hivi karibuni.
Alisema licha ya halmashauri hiyo kufanya vizuri katika sekta ya elimu kiwango cha ufaulu bado kiko chini na watoto wa kike hawana mwamko mkubwa wa elimu jambo ambalo wamedhamiria kulisimamia ipasavyo ili kuinua sekta hiyo.
Amesema kuwa katika kipindi cha miaka 5 atahakikisha wanaboresha miundombinu ya shule zote ili kuweka mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia ikiwemo kuwapa motisha walimu na wanafunzi wanaofanya vizuri katika masomo yao ili kuongeza ari na mwamko wa kielimu katika wilaya hiyo.
Aidha, amebainisha kuwa licha ya wilaya hiyo kuwa changa wakazi wake wana mwitikio mkubwa wa kimaendeleo hivyo atahakikisha wanashirikishwa katika mipango yote ikiwemo kuchangia ujenzi wa miundombinu ya shule zao.
Mwenyekiti huyo ambaye ni diwani wa kata ya Ngasamo iliyoko katika tarafa ya Kivukoni alieleza kuwa katika kipindi hiki cha miaka mitano watakuwa wakali sana kwa wazazi na walezi watakaozuia watoto wao kwenda shule ikiwemo kuwaozesha.
Amebainishaa kuwa baraza la madiwani halitafumbia macho vitendo vyovyote vinavyorudisha nyuma maendeleo ya mtoto wa kike kielimu na kuonya kuwa yeyote atakayebainika kumpa ujauzito mtoto wa kike atachukuliwa hatua kali.
Makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Ng’habi Mwami Mojo ambaye ni diwani wa kata ya Kalemela aliunga mkono maono hayo na kubainisha kuwa elimu ndiyo ufunguo wa maisha kwa watoto wao.
Alisisitiza kuwa watahakikisha kila kata inakuwa na shule ya sekondari na kutakuwa na madarasa na madawati ya kutosha, aliwataka walimu wa shule zote kutekeleza wajibu wao ipasavyo ili kuongeza kiwango cha ufaulu katika shule zao.
Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Anderson Njiginya alimpongeza, Sundi kwa kuchaguliwa kwake kuwa Mwenyekiti wa halmashauri hiyo na kuahidi kuwa watampa ushirikiano wote ili kuharakisha maendeleo ya wananchi. Â
Alieleza kuwa halmashauri hiyo imeendelea kuboresha sekta ya elimu kwa kiwango kikubwa jambo ambalo limepelekea kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi wanaojiunga na shule za sekondari ambapo kwa mwaka juzi jumla ya watoto 5191 walifaulu darasa la saba na mwaka huu ni 5673.
Alibainisha kuwa kipaumbele kikubwa cha halmashauri hiyo kuongeza kasi ya mapato ili kufanikisha ujenzi wa shule za msingi katika kila kijiji na sekondari katika kila kata.
Njiginya aliongeza kuwa katika kipindi cha miaka 5 ijayo wamejiwekea mkakati wa kujenga shule mpya 24 za sekondari na mkakati huo wameuanza mwaka 2018/2019 lengo likiwa kuwa na jumla ya shule 44 ifikapo Juni 30, 2024 ili kupunguza mlundikano wa wanafunzi darasani.