32.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Halmashauri 46 kukumbwa na uhaba wa chakula

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

TATHMINI iliyofanywa na Wizara ya Kilimo, imebaini halmashauri 46 katika mikoa 13 zenye dalili ya kukubwa na upungufu wa chakula kutokana na changamoto zilizoathiri uzalishaji wa chakula kwa msimu wa 2018/19, ikiwa ni pamoja na upunfufu wa mvua.

Wizara hiyo imefanya tathmini ya awali ya hali ya uzalishaji wa mazao ya chakula kwa mwaka 2018/19 na upatikanaji wa chakula kwa mwaka 2019/20 katika mikoa 26 ya Tanzania Bara.

Tathmini hiyo huangalia baadhi ya mazao muhimu yanayohitajika zaidi ikiwamo mahindi, mtama, ulezi, mchele, mikunde, ngano, ndizi, muhogo na viazi.

Akizungumza jana Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, alisema msimu wa uzalishaji wa 2018/19 ulikabiliwa na changamoto katika baadhi ya maeneo hivyo kuathiri uzalishaji wa mazao.

“Kufuatia matokeo haya, Serikali itafanya tathmini ya kina ya hali ya chakula na lishe katika halmashauri zilizobainika kuwa na maeneo yenye viashiria vinavyoweza kusababisha upungufu wa chakula,” alisema Hasunga.

Alizitaja halmashauri hizo kuwa ni Bunda DC, Bunda TC, Musoma DC, Musoma MC, Rorya, Uyui, Igunga, Nzega DC, Nzega TC, Kaliua, Kishapu, Shinyanga DC, Shinyanga MC na Msalala.

Nyingine ni Mwanga, Same, Siha, Hai, Misungwi, Ukerewe, Kwimba, Sengerema, Simanjiro, Kiteto, Hanang, Mbulu TC, Itilima, Maswa, Meatu na Busega.

Pia zimo Longido, Ngorongoro, Monduli, Ikungi, Manyoni, Singida DC, Tanga Jiji, Lindi DC na Iringa DC.

“Ingawa Mkoa wa Dar es Salaam unawekwa kwenye upungufu wa chakula, lakini si miongoni mwa mikoa ya uzalishaji wa mazao hivyo kujitosheleza kwa asilimia 3 tu kutokana na eneo dogo linalolimwa lisilokidhi mahitaji ya chakula ya wakazi wake,” alisema.

Kwa mujibu wa Hasunga, ikilinganishwa na msimu uliopita uzalishaji wa mazao ya chakula umeshuka kwa tani 483,665 ambapo mahindi yameshuka kwa tani 455,642 na mchele kwa tani 210,454.

Alisema katika maeneo yanayopata mvua misimu miwili, mvua za vuli hazikufanya vizuri na pia za masika zilichelewa kuanza na hivyo kuathiri shughuli za kilimo.

Alitaja changamoto nyingine kuwa ni visumbufu hususani viwavijeshi panya na kweleakwelea.

“Kuchelewa kuanza kunyesha kwa mvua na mtawanyiko usioridhisha kwenye baadhi ya maeneo ya nchi yanayopata msimu mmoja hususan katika mikoa ya Dodoma, Singida, Tabota, Shinyanga, Morogoro, Mwanza, Simiyu na Manyara,” alisema.

Hata hivyo licha ya kushuka kwa uzalishaji, tathmini ya wizara hiyo inaonyesha uzalishaji wa mazao ya chakula kitaifa katika msimu wa 2018/19 utafikia tani 16,408,309 ambapo nafaka ni tani 9,007,909 na yasiyo ya nafaka ni tani 7,400,400. Uzalishaji wa mazao yasiyo ya nafaka umeongezeka kwa tani 46,283.

“Kwa kuzingatia kigezo cha upimaji wa kiwango cha utoshelevu, matokeo yanaonyesha kwa mwaka 2019/20 nchi itakuwa na kiwango cha utoshelevu cha asilimia 119,” alisema Hasunga.

Alisema pia mikoa 11 inatarajiwa kuwa na kiwango cha ziada kwa asilimia 128 hadi 227 ambayo ni Rukwa, Ruvuma, Songwe, Katavi, Njombe, Mbeya, Kigoma, Iringa, Kagera, Morogoro na Mtwara.

Waziri huyo aliwataka wakulima waliopata chakula cha ziada wasiharakishe kuuza mazao yao mapema bali wasubiri hadi bei zitakapokuwa nzuri ndipo wauze. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles