Aziza Msoud na Shabani Matutu, Dar es Salaam
HALI inazidi kuwa tete kwa vigogo kadhaa wa Serikali juu ya sakata la uchotwaji wa zaidi ya Sh bilioni 300 kwenye akaunti ya Tegeta Escrow, baada ya kuwapo taarifa kuwa wengi watafikishwa mahakamani.
Iwapo leo vigogo ambao majina yao yamekuwa yakitajwa tangu juzi watafikishwa mahakamani, wataongeza idadi baada ya juzi watumishi wawili wa Serikali kufikishwa katika Mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salaam.
Jana asubuhi baadhi ya maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), walionekana wakiranda katika viwanja vya mahakama hiyo.
Mmoja wa maofisa hao alipoulizwa na waandishi wa habari juu ya kuwapo kwao eneo hilo, alisema wapo kwenye maandalizi ya kuwapandisha kizimbani vigogo wengine.
Hata hivyo, ilipotimu saa 7 za mchana, ofisa huyo alisema kuna baadhi ya nyaraka za watuhumiwa zilikuwa zinarekebishwa kabla ya kufika mahakamani.
Baadhi ya watuhumiwa ambao jana walipigiwa simu na kutakiwa kufika Takukuru, inaelezwa hawakupokea simu kwa hofu ya kuburuzwa mahakamani. Hadi tunakwenda mitamboni harakati hizo zilikuwa zimekwama.
Watumishi waliofikishwa mahakamani juzi ni Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Rugonzibwa Majunangoma ambaye alisomewa mashtaka ya kupokea rushwa ya Sh milioni 323.4 zilizokuwa katika akaunti ya Tegeta Escrow kutoka kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya VIP Engeering James Rugemalila.
Kabla ya Rugonzibwa kufanya kazi Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, alikuwa mwanasheria wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (RITA), ambako alihusika na mufilisi wa Kampuni ya IPTL.
Rugonzibwa, aliichunguza IPTL, alisimamia watumishi wake wakati kampuni hiyo iko katika mufilisi na alisimamia mashauri mbalimbali yanayoihusu.
Mshitakiwa mwingine, ni Theophillo Bwakea ambaye alifikishwa mahakamani kwa kosa la kupokea rushwa ya Sh milioni 161.7 kutoka kwa Rugemalila.
Bwakea ni Mhandisi Mkuu wa Mradi wa Wakala wa Umeme Vijijini (REA), na
kabla ya kufanya kazi huko, alikuwa Wizara ya Nishati na Madini, kitengo cha kusimamia umeme, ambako anadaiwa alishiriki kutunga sera ya kampuni binafsi kuuza umeme Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na ilipoanza kutumika, Kampuni ya kufua umeme ya IPTL ilikuwa ya kwanza kupata zabuni.
Ngeleja agoma
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, William Ngeleja, amewagomea wajumbe wa kamati hiyo waliomtaka ajiuzulu kutokana na kutajwa kuhusika na mgawo wa fedha za Escrow.
Pamoja na hatua hiyo, wajumbe walimtaka Ngeleja ajizulu au akae pembeni ili kumpisha makamu mwenyekiti aongoze vikao jambo ambalo alilipinga.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu ambaye ni mjumbe kwenye kamati hiyo, alisema tangu kuanza kwa vikao hivyo Januari 13, mwaka huu, Ngeleja amekuwa akiviendesha kwa nguvu licha ya wajumbe kumtaka akae pambeni.
“Amekuwa akiendesha vikao tangu juzi na hata juzi aliendesha na kuondoka saa 4 na kumwachia makamu wa kamati hii kumshikia,” alisema.
Alisema juzi baada ya Ngeleja kukaa na kuanza kuendesha kikao hicho, alimtaka kuachia kiti hicho kama ambavyo maazimio manane ya Bunge yalivyowataka wenyeviti waliotajwa kuhusika katika kashfa hiyo ya Tegeta Escrow ambapo yeye anadaiwa kupewa mgawo wa Sh bilioni 40.4 kinyume na sheria.
Lissu alisema pamoja na kumshauri kuachia ngazi, bado Ngeleja aligoma kwa madai akifanya hivyo ataonyesha wazi kuwa alihusika katika kashfa hiyo.
“Ngeleja alisahau katika azimio la Bunge, halikusema wale waliotuhumiwa walikuwa wezi, lakini akashindwa kujua katika azimio jingine Bunge lilitaka vyombo vya uchunguzi kuchunguza ili watakaobainika wachukuliwe hatua ambazo zitathibitisha kama walihusika au la,” alisema Lissu.
Alisema sheria ya maadili ya uongozi wa umma, inawataka viongozi wa umma kutojihusisha na migongano ya kimaslahi na vitendo vya rushwa.
“Kwa mujibu wa sheria za utumishi wa umma, Ngeleja baada ya kutajwa katika ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), akihusishwa kupokea fedha hizo, ilitosha atangaze kujiuzulu,” alisema Lissu.
Alisema kama Ngeleja, ataendelea kukiuka uamuzi wa Bunge, suala hilo watalirudisha bungeni ili lijadiliwe upya.
Zitto
Akizungumzia kuhusu suala hilo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe, alimsihi Ngeleja kutekeleza maamuzi ya Bunge kwa kuachia nafasi hiyo.
“Namsihi Ngeleja kama kijana mwenzangu atekeleze maamuzi ya Bunge na aache kumtega Spika Anne Makinda,” alisema.
MTANZANIA ilipomtafuta Ngeleja kwa njia ya simu ili kuzungumzia madai hayo, muda wote simu yake ilikuwa imezimwa hadi tunakwenda mitamboni.