24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Hali ilivyokuwa wakati Bunge likisitishwa

Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA

RAIS Dk. Magufuli aliingia  viwanja vya Bunge saa 9.58 na kupokelewa na Spika wa Bunge, Job Ndugai, kisha kuingizwa ofisini kwa spika.

Baadaye alitoka nje na kupigwa wimbo wa Taifa,baada ya wimbo huo na ule wa Afrika Mashariki, Spika Ndugai alimkaribisha kuingia bungeni ili kuhutubia wabunge na wageni waalikwa.

Alipopewa nafasi ya kuzungumza, aliwataka watu wote kusimama ili kuwaombea marehemu ambao wamewahi kuwa wabunge katika Bunge la 11.

Wakati wa utambulisho, aliyekuwa Rais  mstaafu Jakaya Kikwete, alishangiliwa kwa nguvu na wabunge pamoja na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally.

Wengine walioshangiliwa ni marais wastaafu, Benjamini Mkapa, Ali Hassan Mwinyi, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dk. Anna Makakala na Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Deogratius Ndejembi. 

MKUCHIKA NA UCHAGUZI

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, George Mkuchika, alisema watasimamia kauli ya Rais Dk. Magufuli kwa kuhakikisha hakutakuwa na rushwa katika uchaguzi huo.

“Naona fahari kwa jinsi ambavyo Takukuru inafanya kazi, haina muda mrefu, utendaji kazi wake umeendelea kuaminiwa na wananchi tukumbuke wakati inaanzishwa wilaya 21 zilikuwa hazina ofisi.

“Sasa hivi mambo yanaenda vizuri na kama alivyosema rais, Takukuru itasimamia kwa kuhakikisha kunakuwa hakuna rushwa,”alisema.

Akitoa tathmini ya wizara yake kwa kipindi cha miaka mitano, Waziri Mkuchika alisema anajivunia kwa jinsi ambayo suala la watumishi hewa na wale wasiokuwa na vyeti lilivyosimamiwa.

“Tumefanya uhakiki, kulikuwa kuna malipo hewa, nchi yetu ilifika mahala si pazuri, tumefanya jambo kubwa na kwa sasa nidhamu kwa watumishi wa umma imekuwa kubwa na wanaofanya kazi ni wale wenye sifa,”alisema.

Alipoulizwa atarudi kwenye  kinyang’anyiro katika Jimbo Newala Mjini, Mkuchika alisema yeye bado ni kijana na ana uhakika kama chama chake kitampa ridhaa atarudi tena katika nafasi hiyo.

KANYASU 

Akizungumza nje ya viwanja vya Bunge, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Costantine Kanyaso, alisema kuongoza wizara hiyo, ni kazi ngumu, lakini anamshukuru Rais Dk. Magufuli anavyowasaidia hasa wakati  janga la ugonjwa wa corona.

“Wizara yetu ni nyeti ila tunamshukuru mheshimiwa rais kwa jinsi ambavyo amekabiliana na janga la ugonjwa wa corona, sasa hivi milango imefunguka na tunaendelea kuchapa kazi, tunaamini popote utalii tutaupeleka,”alisema.

WABUNGE 

Wakizungumza na MTANZANIA nje ya viwanja vya Bunge, baadhi ya wabunge walipongeza Serikali ya kwa kutatua changamoto mbalimbali katika sekta ya elimu, afya, miundombinu na umeme huku wengine wakipinga.

Mbunge wa Viti Maalumu, Rhoda Kunchela (Chadema), alisema kuna baadhi ya masuala katika awamu ya tano yametekelezwa, mengine bado hivyo wananchi wanatakiwa kuipa dola Chadema ili itende kazi iliyotukuka.

“Mimi natangaza nia yangu ya kugombea ubunge Jimbo la Mpanda Mjini, kuna baadhi ya mambo hayajakaa vizuri kule mfano suala la stakabadhi ghalani malalamiko yamekuwa ni mengi,”alisema.

Mbunge wa Ngara, Alex Gashaza (CCM), alisema kipindi cha miaka mitano, Serikali imefanya kazi iliyotukuka katika Jimbo la Ngara kwa kupata vituo vitatu vya afya na kuongezwa shule mbili za kidato cha tano na sita.

“Tuna mamlaka mbili za Lulenge na Ngara, mwanzo tulikuwa na kilomita 1.5 za lami, sasa hivi zimefika 7, tulikuwa tuna vijiji 18 pekee vyenye umeme, sasa hivi tuna vijiji 25, kikubwa tumepata bilioni 12 kutokana na mradi wa Lusumo, hizi ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo maeneo yetu na tutapokea kwa ‘phase’ mbili,”alisema.

Mbunge wa Viti Maalumu, Agness Maro (CCM), alisema Mkoa wa Mara wanamshukuru rais kwa kipindi cha miaka mitano kwani amewasaidia, ikiwemo huduma za afya kuboreshwa pamoja na hospitali ya rufaa kuboreshwa.

“Mimi binafsi nimewasaidia wanawake kwa kuwapa mikopo isiyokuwa na riba , nimeanzisha saccos pamoja na walemavu kuwapa vifaa hasa wale wenye mahitaji kwa kifupi kwetu Mara tunamshukuru rais wetu,”alisema.

Mbunge wa Momba, David Silinde (Chadema), alisema Rais Magufuli amejaribu kuonyesha kwa vitendo yale yote aliyoahidi hivyo kuna haja ya kuendelea kumuunga mkono ili ndoto zake ziweze kutimia.

“Tuna haja ya kuendelea kumuunga mkono na mimi nitaendelea kumuunga mkono hata kwa awamu inayokuja,”alisema ambaye ametangaza kujiunga na CCM.

Mbunge wa Solwa, Ahmed Salim (CCM), alisema atagombea tena katika awamu ijayo kutokana na kutimiza matakwa ya mahitaji katika jimbo lake na anaamini hatapata mpinzani.

Mbunge wa Manonga, Seif Gulamali (CCM), alisema Rais Magufuli ameitendea haki ilani ya CCM,wakati anaingia madarakani kulikuwa hakuna shule ya kidato cha tano na sita lakini kwa sasa zipo mbili.

Mbunge wa Mlalo, Rashid Shangazi (CCM), alisema bado kuna changamoto ya barabara kutopitika katika jimbo lake hivyo anaamini wananchi wakimuongezea muda atahakikisha zinakamilika.

Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete (CCM), alisema atagombea katika awamu ijayo kwani mambo mazuri yamefanyika katika jimbo lake.

Mbunge wa Kinondoni, Maulid Mtulya (CCM), alimshukuru rais kwa soko kubwa Mabatini na Ananasifu ambayo yanajengwa pamoja na shule mpya zinaendelea kujengwa.

Akizungumza kuhusu hotobu ya Rais Katibu wa Jumuiya ya Wanawake wa CCM, Qeen Mulozi, alimpongeza Rais, Magufuli kwa kazi kubwa aliyoifanya ya utekelezaji wa ilani sambamba na utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles