30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

HALI HII YA UCHUMI INATIA MASHAKA

NA JAVIUS KAIJAGE,

MIEZI michache baada ya Serikali ya Awamu ya Tano kuingia madarakani Watanzania wakaanza kupata furaha kuwa ile hali ya Serikali kushindwa kukusanya mapato ya kutosha ilikuwa inakwisha. Furaha hiyo ilitokana na hatua za kubana matumizi pamoja na kuwabana wakwepa kodi ambazo zilichukuliwa na Serikali.

Tulishuhudia jinsi Rais John Magufuli na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa walivyoibana Mamlaka ya Usimamzi wa Bandari (TPA) pamoja na Mamlaka ya Mapato (TRA). Tukashuhudia mapato ya kila mwezi ya Serikali yakivuka kiwango cha Sh. trilioni moja kwa mwezi.

Hali hiyo iliwafurahisha wananchi kwa sababu ilionekana kama dalili njema ya Serikali kuweza kumudu kuigharamia Bajeti yake bila kuwa na nakisi.

Lakini sasa wasiwasi umeanza kurudia baada ya ripoti za kila mwezi za TRA kuonyesha kuwa makusanyo ya mapato ya ndani yamebaki kama yalivyo na wakati mwingine malengo ya makusanyo hayafikiwi.

Lakini kwa upande mwingine, ripoti za kila mwezi za Benki Kuu (BOT) nazo zinaonyesha kuwa wafadhili walioahidi kutoa fedha kwa ajili ya kusaidia Bajeti ya Serikali wameshindwa kutimiza ahadi zao ipasavyo. Ripoti ya BOT ya Disemba inaonyesha katika kipindi cha miezi mitano ya utekelezaji wa Bajeti wafadhili walikuwa wametoa kiasi cha asilimia 32 tu ya kiwango cha fedha ambacho waliahidi kukitoa katika kipindi hicho.

Katika kipindi cha kati ya Julai na Novemba mwaka jana Serikali ilitarajia kupokea kiasi cha Sh. trilioni 1.01 kama misaada lakini takwimu zinaonyesha kuwa kiasi kilichokuwa kimetolewa na kupokelewa na Serikali ni Sh. bilioni 328.8 pekee.

Kwa upande mwingine, ni asilimia 18.2 tu ya mikopo ya masharti nafuu ndicho kilipokelewa na Serikali katika kipindi hicho. Wakati matarajio yao ilikuwa ni kupata kiasi cha Sh. trilioni 1.7, Serikali ilifanikiwa kupata kiasi cha Sh. bilioni 441.48 tu.

Hali hii ni ya kutia mashaka kwa sababu kwa kiasi kikubwa hizi ndizo fedha ambazo zinapaswa kuelekezwa kwenye miradi ya maendeleo. Zinapokosekana inamaanisha kuwa miradi mingi ya maendeleo haitaweza kutekelezwa kwa ufanisi.

Kwa kuwa sehemu kubwa ya miradi inayopaswa kutekelezwa kwa fedha hizo ipo maeneo ya vijijini, ni dhahiri kuwa wananchi wa maeneo hayo ndio watakaoathirika zaidi kwa kukosekana kwa fedha hizo.

Pamoja na kutekeleza miradi ya maendeleo, lakini upatikanaji wa fedha hizo ulitarajiwa pia kusisimua uchumi  kwani utekelezaji wa miradi hiyo ungewapatia wananchi fedha na hivyo kuongeza ukwasi na mzunguko wa fedha. Lakini hayo hayatatimia kwa kiwango kilichotarajiwa na matokeo yake uchumi utaathirika.

Juzi hapa tumeshuhudia kilio cha watu wengi, ambacho bado hakijaisha, kuhusu watu kutokuwa na pesa. Jibu jepesi lililotolewa ni kuwa fedha imeadimika kwa watu waliokuwa wanapiga madili.  Jibu hilo la jumla lilikuwa baya sana kwa sababu si kweli kuwa wote waliokuwa wanalalamika walikuwa ni wapiga dili. Tulishuhudia kuporomoka kwa baadhi ya biashara, hususani hoteli, lakini Serikali ikabaki na msimamo wake ule ule wa wapiga dili.

Labda inachosahau ni kuwa kuporomoka huko kwa biashara kunamaanisha kupungua kwa wigo wa walipa kodi wa ndani na hiyo ni sawa na kusema kupungua kwa kiwango cha kodi kinachokusanywa.

Ripoti za TRA zinaanza kuonyesha ukweli huo kwa sababu makusanyo yameanza kubakia katika kiwango kile kile na si kuongezeka kama ilivyotarajiwa.

Mambo haya mawili, yaani kupungua kwa mapato kutoka kwa wafadhili na kupungua kwa makusanyo ya kodi za ndani, kunauumiza uchumi na kwa jinsi uchumi wetu ulivyo mwananchi wa kawaida ndiye mhimili machungu ya hali hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles