24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

HAKUTAKUWA NA MTOTO ATAKAYEACHA SHULE SABABU YA FEDHA

Wanafunzi wakipanda Lori

Na CHRISTINA GAULUHANGA, SABASABA

UMASKINI kwa baadhi ya wananchi ni kichocheo cha familia nyingi kushindwa kujiendeleza kielimu hasa ile ya sekondari.

Hali hiyo husababishwa na ukosefu wa ada pamoja na mila na desturi potofu.

Hata hivyo, Serikali chini ya Rais Dk. John Magufuli iliona kero hii na kuamua kuanzisha sera ya elimu bure kwa wote ambayo kwa kiasi fulani imesaidia kuwaokoa wananchi hasa wale wenye kipato cha chini.

Hivi sasa, kumekuwapo na ongezeko la shule nyingi za kata ambazo zimewasaidia wazazi kuwapeleka watoto wao kupata elimu hiyo.

Taasisi mbalimbali zikiwamo benki zimeanzisha mifumo itakayomuwezesha mzazi au mwanafunzi kuweka akiba kidogokidogo ili kuweza kupata ada kwa faida ya watoto wake hapo baadaye.

Ofisa Uhusiano wa Benki ya NMB, Doris Kilale anasema benki hiyo iliona umuhimu wa elimu kwa jamii na kuamua kuanzisha akaunti ya Wajibu ambayo inaleta hamasa kwa mzazi na mwanafunzi mwenyewe kuona umuhimu wa kuweka akiba.

“Tulitafakari cha kufanya kuisaidia jamii hata wale wazazi wenye kipato cha chini, watoto wao waweze kuendelea na masomo, tuliona akaunti ya Wajibu ndio suluhisho kwetu na kwa jamii nzima,” anasema Doris.

Anasema baada ya kuangalia kwa undani changamoto za ulipaji ada pamoja na wazazi wengi na wanafunzi kushindwa kutunza fedha, walionzisha akaunti hiyo isiyo na masharti ambayo ni mwokozi wa kila mzazi.

Doris anasema akaunti hiyo imegawanyika katika sehemu tatu ambazo ni NMB Mtoto Akaunti, NMB Chipukizi na NMB Mwanachuo.

Anasema akaunti hiyo inasaidia mzazi au mlezi kumwandalia mtoto mazingira bora hususan ya kielimu ambapo fedha zinazowekwa zinategemeana na uwezo wa kila mzazi au mwanafunzi husika ambaye atakuwa anaiendesha hiyo akaunti.

Dorisi anasema lengo kuu la akaunti hiyo ni shule, ambapo pia wamefanya maboresho hivyo haina makato yoyote ya mwezi pia fedha zilizowekwa hazipungui na zina riba mara mbili.

“Faida nyingine katika akaunti hii imepewa fursa ya kufanya miamala isiyotozwa fedha hivyo mteja wa akaunti hii anafaidika zaidi,” anasema Doris.

Kwa upande wake Ofisa Bidhaa Binafsi wa NMB, Heazon Mpate anasema faida ya akaunti hiyo ni kwamba unaweza kufungua kulingana na umri wa mtoto wako.

Anasema akaunti imegawanya wateja katika mafungu matatu ambayo ni kuanzia umri wa  mwaka mmoja hadi miaka 12, miaka 13 hadi 17 na ya mwisho miaka 18 na kuendelea.

Mpate anasema ufunguzi wa akaunti hiyo inasaidia kumuongoza mzazi na mtoto katika matumizi ya fedha zake na kuacha kuzitumia ovyo.

Kwa upande wake Ofisa  Uhusiano Kitengo cha Biashara, Baraka Kyamba anasema benki hiyo pia ina akaunti nyingine inayoitwa Fanikiwa ambayo ni mahususi kwa wafanyabiashara ndogondogo, inayolenga kuwapa fursa ya kutambuliwa na kupewa mikopo.

Anasema wafanyabiashara wanaojiunga na akaunti hiyo wanaweza kunufaika na mkopo kuanzia Sh 50,000 hadi Sh milioni 30.

Kyamba anasema pia mteja wa akaunti hiyo atakuwa ni mwanachama wa Klabu ya Biashara ya NMB ambazo zipo nchi 34.

Anasema wamekuwa wakitoa mafunzo ya elimu ya hesabu za biashara kwa kila mteja wa akaunti hiyo, kuwaunganisha na wataalamu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ili kupata elimu ya ulipaji kodi na kuwafundisha jinsi ya kupata hati miliki za ardhi wanazomiliki.

Anasema wanachama wa akaunti hiyo wanapata fursa ya kupata masoko, wateja, ushauri wa kibiashara na mikopo kwa maofisa mikopo waliopo nchi nzima.

Kyamba anasema mteja wa akaunti hiyo anaweza kunufaika na kadi maalumu ya Benki (Master Card) na hundi.

Anabainisha kuwa wapo baadhi ya wazazi na wanafunzi ambao bado hawajapata elimu sahihi ya utunzaji fedha hivyo hutumia fedha zao vibaya.

Anasema NMB imejipanga kuwaelimisha watu wa aina hiyo ili kuweza kujiwekea akiba benki.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles