Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MAMLAKA ya Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imesema nchi ina mafuta ya aina zote ya kutosha na hakuna tatizo linaloonyesha kutokea upungufu wa mafuta siku zijazo.
Taarifa hiyo ya EWURA ilitolewa jana na Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Felix Ngamlagosi, ilieleza kuwa nchi ina petroli ya kutosha matumizi ya siku 12, dizeli ya siku 15 na mafuta ya taa siku 16.
Alisema meli zinaendelea kuingiza mafuta kwa mujibu wa ratiba ilivyopangwa.
Ngamlagosi alisema baadhi ya mikoa hususan Ruvuma na Mtwara, ilikuwa na upungufu wa petroli kutokana na mapumziko marefu ya sikukuu za Saba Saba, Eid el Fitr na mwisho wa wiki.
“Katika hali hiyo baadhi ya maghala hayafanyi biashara siku hizo. Katika mikoa iliyotajwa, wateja walipata wasiwasi wa uhaba wa mafuta na kununua kwa wingi, jambo ambalo liliongeza tatizo.
“Hata hivyo, mikoa ya Ruvuma na Mtwara imeendelea kupokea mafuta ya aina zote tangu Julai 8, mwaka huu na hali ya soko inaendelea kutengamaa.
“EWURA inawasihi watumiaji wa mafuta ya jamii ya petroli kutokuwa na wasiwasi na waendelee kununua kwa utaratibu wa kawaida,” alisema Ngamlagosi .