26.1 C
Dar es Salaam
Friday, December 9, 2022

Contact us: [email protected]

Hakuna mtoto anayezaliwa na ukorofi

NIMESHAKUTANA na wazazi wengi wanaolalamikia tabia ya ukorofi wa watoto wao. Hawa ni watoto wepesi kurusha rusha mikono na miguu kama namna ya kupinga unachowaelekeza kufanya. Huwa wana ushindani, wagomvi wanapokuwa na wenzao. Ukorofi unakwenda sambamba na tabia ya kupenda kujiona ni mtawala anapokuwa na wenzake. Matokeo yake ni migogoro na wenzake mara kwa mara.

Ukorofi, kwa hakika, ni ujumbe. Ukorofi ni lugha ya kusema moyo wa mtoto unakosa kitu fulani anachokihitaji. Ni sawa na mtu aliyeshinda njaa siku kadhaa. Kwa vyovyote vile ni dhahiri atakosa utulivu. Mwili wake utahitaji chakula. Mtoto mkorofi kimsingi anaamini watu wanaomzunguka hawajatambua nafasi yake ipasavyo. Ndani yake mna sauti inayomwaminisha kuwa hatambuliki. Imani hiyo potofu huchochea jitihada za kutafuta kutambulika kwa namna isiyokubalika.

Ubishi na ukaidi anaoufanya wakati mwingine bila hata yeye kujua anafanya nini ni namna ya kujirudishia mamlaka anayoamini hana. Anapobishana na mzazi, anapogombana na wenzake, kimsingi anajaribu kujirejeshea ushawishi ambao anaamini hana.

Mambo mengi yanaweza kuzaa ukorofi. Wapo baadhi ya wanataaluma wanaamini mtu huzaliwa na ukorofi. Inawezekana. Lakini kwa sehemu kubwa tafiti zinaonyesha kuwa ukorofi ni zao la malezi. Hapa kuna mambo makubwa matatu. Kwanza, inawezekana kwa sababu ya ku

tamani mtoto ‘anyooke’ umekuwa na sheria kali mno. Unaamini mtoto hawezi kufanya kitu bila kuamrishwa. Kwa sababu ya kuamini hivyo, umejikuta ukijenga mazingira ya mapambano yasiyo na sababu.

Lakini pili, inawezekana ikawa ni mazingira ya malezi. Hapa tunazungumzia wazazi au watu wanaoishi na mtoto kuwa na tabia za ukali, ugomvi, kutokujali, na aina nyingine za matumizi ya mabavu. Kwa kawaida, watoto wananasa

kwa haraka sana mambo yanayogusa hisia zao. Wanapoona mtu mzima anafanya jambo fulani na watu anaowaamini wanalichukulia kawaida, wanakuwa na uwezekano mkubwa wa kufanya kile kile wakati fulani.

Bila kujali chanzo chake kuna hatua za kuchukua kushughulikia ukorofi. Kwanza wekeza katika kujenga urafiki. Hatuzungumzii urafiki wa siku mbili au tatu. Tunazungumzia urafiki wa kudumu ambao mtoto hatakuwa na sababu ya kuwa na mashaka nao. Kama tulivyoona, mtoto mtundu kimsingi analo hitaji kubwa la uhusiano wa karibu na wewe mzazi.

Unapojitahidi kuwa karibu naye usishangae mwanzoni bado mtoto akaendelea kuwa mkaidi vilevile. Usikate tamaa. Mpe nafasi ya kukuamini kwa kujenga urafiki imara. Sambamba na urafiki, punguza amri na kelele zisizo za lazima. Kumbuka kuwa amri bila urafiki huchochea uasi. Badala yake jenga tabia ya mazungumzo ya utulivu unaposhughulika naye. Badala ya kuagiza, jaribu kushirikiana naye. Mwonyeshe kuwa unajali na kuthamini kile anachokipenda.

Kumbuka ukorofi wake unato- kana na hali ya kujisikia kutokue- leweka. Kwahiyo katika mazungumzo mpe nafasi ya kusema. Mwache aongee yaliyoujaza moyo wake na usiwe mwepesi kukosoa hisia zake wala kujitetea. Mpe uzingativu kwa kuacha shughuli unazofanya kwa ajili yake. Ushirikiano wa kiwango hiki utamchangamsha. Ukiweza kufanya hivi bila unafiki mtoto ataanza kukuamini na kidogo kidogo atabadilika.

Pia mheshimu kama mtu mwingine yeyote unayemheshimu. Heshima ina mambo mengi. Usimdhalilishe mbele ya wenzake kwa maneno au vitendo. Kama kuna sababu ya kumwadhibu, fanya hivyo kwa staha. Kumheshimu mtoto hakukuondolei mamlaka yako kama mzazi.

Aidha tengeneza mazingira ya kumshirikisha kwenye maamuzi. Kwa sababu tayari ana utundu, mweke karibu unapotaka atekeleze jambo. Badala ya kumwambia ‘kafanye,’ badili lugha iwe, ‘tufanye’ hata kama hulazimiki kufanya. Inapobidi hasa kwenye hatua za mwanzo, shirikiana naye kufanya hicho unachotaka akifanye.

Christian Bwaya ni mhadhiri wa Saikolojia Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWE- CAU). Twitter: @bwaya, Simu: 0754870815

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,735FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles