HAKIKI KATUNI KABLA YA MTOTO KUIANGALIA

0
1553

NA AZIZA MASOUD,

WATOTO wengi wamekuwa na utamaduni wa kuangalia katuni au vikaragosi kama inavyofahamika kwa nchi jirani.

Huu ni utamaduni pendwa uliobarikiwa na wazazi wengi ambao wanawaruhusu watoto wao kuangalia katuni kama sehemu ya kuburudika na kuwasaidia kujifunza mambo mbalimbali.

Familia nyingi za kipato cha kati ambao wamefanikiwa kununua televisheni nyumbani watoto wake huanza kupenda kuangalia katuni kuanzia miezi sita na kuendelea.

Wanapofikia umri wa miaka miwili na nusu mpaka mitatu watoto huanza kuona vipindi ama kanda za katuni kama sehemu yao ya mchezo wa kila siku.

Katuni pamoja na kwamba zinawafanya watoto wachangamke akili na kujifunza mambo mbalimbali, pia zinaweza zikamfundisha mtoto maadili mabaya.

Kwa sasa kumekuwa na katuni nyingi ambazo hazina msaada kwa mtoto, badala yake zinachangia kuwaharibu.

Zipo katuni ambazo zinawafundisha  watoto katika maadili mazuri na kuwatengeneza na kuwa na maisha ya utii na heshima, jambo ambalo  ni lengo kuu la wazazi wengi.

Mbali na katuni hizo, zipo ambazo zina mlengwa tofauti, mfano kuna katuni ambazo zina maudhui mabovu, ikiwamo ushirikina, kufundisha watoto utundu usiokuwa na maana.

Zipo nyingine zinaonyesha maudhui ya  uhusiano ama kuonyesha watu wakiwa wanauawa kwa kuchinjwa, yote hayo ukiyaangalia kwa undani hayana faida kwa mtoto katika maisha yake ya kila siku ya kujifunza.

Kwa sasa wazazi wanapaswa kufahamu kwamba, baadhi ya katuni wanazonunua kwa ajili ya watoto ama kuwaruhusu waangalie si salama kwao.

Ni vema kuweka utaratibu wa kuanza kuziangalia katuni kabla ya kumruhusu mtoto kuangalia, lengo likiwa ni kujua kilichomo kama kinafaa kwa ajili ya mtoto.

Hiyo itasaidia kuizuia kutomfikia mtoto endapo itakuwa na maudhui mabovu.

Tafuta njia nzuri ya kumwelewesha mtoto sababu ya kutoangaliwa katuni hiyo na si kwakutumia maneno makali wala kumfokea.

Jaribu kutafuta mbadala wa katuni hiyo, ili uweze kumridhisha na asijisikie mnyonge.

Ni muhimu kuwa makini katika vitu kama hivi, kwakuwa vinaweza vikamharibu mtoto na kumjengea taswira  mbaya kwa sasa na siku za usoni.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here