24.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 31, 2023

Contact us: [email protected]

HAKI YA MALIPO KIFO CHA AKWILINA NI UWAJIBIKAJI

Na DK. HELLEN KIJO BISIMBA


IJUMAA ya wiki iliyopita, tulipata taarifa za kusikitisha na za kutisha kuhusu kifo cha mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) jijini Dar es Salaam, Akwilina Ackwiline. Tukio hili ni simanzi kubwa na ya kutisha kwa Taifa letu.

Kwanza nianze kwa kutoa pole kwa wazazi na ndugu wa marehemu na kwa wanafunzi wa NIT, pia poleni ndugu zangu Watanzania tumefika mahali pasipotakiwa kufika.

Tuliposikia kifo hiki kilivyotokea kwa mujibu wa mashuhuda na vyombo vya habari ni kwamba, askari wa Jeshi la Polisi walikuwa wakizuia maandamano ya wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Swali lililojitokeza na ambalo wengi tunahoji ni kwamba huu utamaduni wa kukabiliana na raia kwa risasi za moto umejengeka lini?

Lakini pia kwa mujibu wa taarifa, huyu binti alikuwa ndani ya daladala, sasa mtu ndani ya basi anaandamana? Na je, alikuwa akifanya fujo gani risasi imlenge?

Jambo ambalo linazidi kushangaza ni kwamba msemaji wa kwanza wa Polisi alikiri kuwa risasi ya Jeshi la Polisi ndiyo iliyompiga binti huyo kwa mujibu wa mahojiano yaliyonukuliwa na chombo kimoja cha habari.

Baadaye kauli zimeanza kugeuka kuwa huenda waandamanaji walikuwa na silaha za moto. Kwa jambo zito kama hili, tusingetegemea kauli za ‘huenda ‘tangu siku ya tukio ilibidi ifahamike silaha gani ilitumika kwani askari polisi walikuwa sehemu ya tukio wakati likitokea.

Kama waandamanaji walikuwa na silaha na askari walikuwa wanakabiliana nao, tungetegemea tuwe tumejulishwa aina ya silaha iliyotumika na kanusho kutoka kauli ile ya kwanza.

Pili, inasemekana viongozi wa maandamano ndiyo wakamatwe na wengine wakisema binti huyo alikuwa kwenye gari lililobeba waandamanaji. Kwa watu wanaojua thamani ya utu, hizo si hoja za kuweka mbele wakati Mtanzania amepoteza uhai wake.

Hakuna sababu yoyote ya kuua raia tena  akiwa ndani ya gari. Imeelezwa huyu ni mwanafunzi alikuwa ana safari zake. Nilitegemea kusikia kauli nzito kutoka kwa mkuu wa nchi.

Lakini nimeona ‘ametweet’ akieleza kusikitishwa na kutoa pole na kwamba ameagiza uchunguzi. Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, alifika msibani kabisa na tumeona kilio cha dada wa marehemu  kikionesha jinsi gani ndoto za ndugu kuhusu binti huyu aliyezimika zilivyozimwa.

Waziri mwenye dhamana ya usalama wa raia yaani Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba na Mkuu wa Jeshi la Polisi, Simon Sirro, wanahitajika hapa kujihoji na kwa ustaarabu wachukue hatua ikiwemo kujiuzulu.

Haitoshi kusema tunachunguza, mbona mengi yamechunguzwa na hatuoni majibu hadi sasa. Tukiangalia sana na maumivu yaliyo moyoni, inaumiza sana kuona kifo cha aina hii kinatokana na masuala ya siasa.

Rais aliyesikitishwa achukue hatua za kiuwajibishaji. Pia hatutegemei polisi ambao wanaonekana kuhusika ndiyo wachunguze suala hili. Wameshaonesha kujitetea haki, haitatendeka. Kipatikane chombo huru kuchunguza suala hili.

Kwa upande mwingine suala la kujiuliza ni nini kinachochunguzwa ilhali waliohusika wanajulikana? Kwanini wasifikishwe mahakamani ili mahakama ifanye kazi yake ya kuona hatia na kiasi cha hatia hiyo kwa watuhumiwa hao?

Tujiulize, hizi chaguzi zinazofanyika nchini kiasi cha damu kumwagika ni kwa faida ya nani? Tutafakari sana na tujikumbushe wenzetu Kenya hivi karibuni kusanyiko kubwa lilikutana kumwapisha mtu aliyesemekana rais wa watu (Raila Odinga), Serikali na vyombo vyake havikuingilia kusanyiko lile na liliisha kwa amani.

Hivi hao wanaosemekana walikuwa wanaandamana wangesindikizwa na polisi hadi walikokuwa wanaandamana kungekuwa na shida gani? Na kama kweli walikuwa na vurugu njia pekee ilikuwa kurusha risasi za moto zisizo na mwelekeo?

Inaonesha kuwa kulikuwa na kusudio la kuua na si kutawanya waandamanaji kwani mabomu ya machozi yangetosha kabisa kuwatawanya waandamanaji badala ya risasi za moto kutumika.

Alipoulizwa Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alinukuliwa akisema askari huyo alirusha risasi hewani. Je risasi hiyo ingerushwa hewani ingeshukaje na kumpata mtu aliye chini tena ndani ya basi?

Demokrasia ni ustaarabu unaohusu watu, yaani ni mfumo wa utawala wa watu walioweka watu madarakani kwa ajili yao. Nilivyoguswa na kifo hiki na vingine vya aina hii, inabidi kujiuliza iwapo tumeshafikia kiwango cha huu ustaarabu wa mfumo wa demokrasia ya vyama vingi.

Damu ya Akwilina itaendelea kutulilia kwa kweli. Huko Afrika Kusini wamempata Rais mpya, Cyril Ramaphosa, baada ya aliyekuwepo madarakani (Jacob Zuma) kujiuzulu kwa shinikizo.

Rais mpya Ramaphosa amezungumza kwa kauli nzito kuwa upinzani si uadui ila ni wa lazima ili kukiwezesha chama kilichopo madarakani kufanya kazi yake na kikifanya kazi yake vizuri upinzani utajifia wenyewe.

Ndugu zangu Watanzania hili la Akwilina mnaliona ni sawa kweli kiasi cha kuwa na upande, badala ya wote tujitokeze kulaani  kwani ni fedheha na aibu yetu wote.

Hapa damu isiyo na hatia imemwagika tunatakiwa tusimame kidete uwajibikaji utokee haitoshi kusema uchunguzi, kwanini kukabili raia na risasi za moto na kuzirusha ovyo? Haki za raia ziko wapi ulinzi na usalama hapa ukoje?

Kwa heshima kubwa sana kwa kuiangalia ile damu ya binti yule ambaye imeonekana hadharani, wenye mamlaka wachukue hatua mara moja waache kuwanyooshea wengine vidole, vidole virudi kwao wajiengue maana hii si sahihi hata kidogo.

Tulikubali siasa za vyama vingi ili kukuza njia bora za utawala si kupoteza watu. Mwalimu Nyerere alipata kueleza kuwa pale ambapo polisi waliua raia kule Kilombero mkoani Morogoro, kuwa risasi hazikununuliwa ili kuua raia bali ni kwa ajili ya kuwalinda.

Hili alilisema kwa ukali na kwa msisitizo. Huu ni ukweli hadi sasa tukumbuke kuwa hawa raia wana haki hata hizo za kuandamana na wasipofuata utaratibu, kazi ya polisi si kuua bali ni kutuliza na kuchukua hatua stahiki na si vinginevyo.

Kama mfumo umetushinda tuuweke kando maana maamuzi ni yetu. Wakati tukiomboleza tufikirie sana tunavyoweza kuepuka kabisa kutoa uhai wa mtu kwa hali yoyote ile maana haki ya kuishi ikishaondoka huwezi kuirudisha.

Haki ya malipo kwa kifo hiki ni uwajibikaji na uwajibishwaji na mamlaka zilizopo madarakani. Watanzania tukemee hali hii kwani inataka kuweka kambi hapa kwetu, kwani tunaelekea wapi? Tusijepotea njia.

Nenda kapumzike kwa amani binti yetu Akwilina, uhai wako wa thamani umeyeyushwa pasi na sababu!

Mwandishi ni Mkurugenzi Mtendaji wa KItuo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC). Anapatikana na kwa namba; 0713 337 240.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,208FollowersFollow
567,000SubscribersSubscribe

Latest Articles