WIKI hii, Julai 1, Benki ya Dunia iliingiza Tanzania katika kundi la nchi zenye kipato cha kati.
Hizi ni habari njema hata pamoja na kwamba wapo wanaoona kuna mapungufu fulani fulani katika utendaji.
Hatua ya kutoka katika umaskini na kupanda kwenda katika hatua nyingine ya juu huusisha suala zima la uchumi au maendeleo ya kiuchumi.
Lakini pamoja na hayo maendeleo ya kiuchumi huguswa na vitu au mambo mengi mfano kutenda haki, amani, usalama, utulivu nakadhalika.
Mtu yeyote anapokuwa katika mazingira yenye kutenda haki, amani, utulivu humwezesha kufanya kazi kwa bidii na hatimaye kuwa mzalendo kwa nchi yake ikiwa ni pamoja na kulipa kodi.
Sasa mazingira yanapokuwa tofauti na hayo, ndiyo ambayo yanachangia kwa kiasi kikubwa kurudisha nyuma maendeleo ya nchi .
Kwa sababu hiyo sisi tunaweza kusema tumekuwa mabalozi wazuri wa kusisitiza suala la haki kila wakati, kwa sababu tumekuwa tukiamini haki ni msingi wa mambo yote mazuri.
Na ndio maana tumekuwa tukikosa na wakati mwingine kukumbusha kutenda haki hasa katika vyombo vile vya kimaamuzi na kiutendaji.
Tumekuwa tukisisitiza kwamba vyombo hivyo vinapaswa kutambua wajibu wao kuwa ni kutafuta namna ya kutatua matatizo na si kuyaongeza.
Yapo baadhi ya matukio si yote ambayo yamefanywa na vyombo hivyo na hivyo kutoa taswira ya kukomoa au kuumiza baadhi ya watu kwa makusudi.
Tumekuwa tukisisitiza hayo kutokana na kuwapo kwa ripoti ambazo zinaonyesha kuwa barani Afrika kwa muda mrefu sasa watu wameumizwa na vitendo vya kudhulumiwa haki zao msingi.
Kwa mujibu wa ripoti hizo hata kutopea katika umaskini wa kimawazo, na hivyo wengi kuhadaika na kauli za wanasiasa, viongozi na watu wenye nafasi katika jamii, msingi wake ni dhuluma ya haki zao za msingi.
Kwa misingi kama hiyo sisi kama chombo cha habari tunao wajibu wa kukumbusha kwamba vyombo hivyo kila inachofanya kabla ya kutoa uamuzi wowote basi vitambue vinao wajibu wa kuchunguza, kusikiliza, kubadilisha na kuboresha.
Zipo nyakati tumeshuhudia vyombo hivi vikichukua uamuzi wa ghafla hata katika masuala nyeti sana katika mifumo ya sheria, utumishi nk.
Vyombo hivi vinapaswa kutambua kwamba chochote kitakachofanyika bila kufuata misingi hiyo tuliyoitaja hapo juu kitakwenda kuathiri mustakabali mwema wa Taifa letu.
Wakati fulani aliyepata kuwa kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Baba Mtakatifu Benedikto wa XVI, alitoa changamoto kubwa kwa watawala wa dunia.
Kwa maneno yake mwenyewe alisema; “jamii yenye haki hujengwa na wanajamii wenye haki”.
Maana yake tukitaka kujenga jamii yenye haki hatuna budi sisi wenyewe kuwa wenye haki.
Kiongozi huyo alikwenda mbali na kusema; wao kama kanisa hawana mbinu za kiufundi wala nafasi ya kuingilia mambo ya siasa moja kwa moja lakini alibainisha wazi utume ambao alisema kama kanisa haliwezi kuuacha hata kidogo ni ule wa kuutangaza ukweli.
Ukweli si jambo ambalo linapaswa kubebwa na taasisi zetu za kidini tu bali hata katika serikali zetu na taasisi zake, mahakama zetu, vyombo vya ulinzi na uslama kama Jeshi la Polisi, Bunge nk.
Kuna msemo mmoja kwamba; ukweli ndio utakaowaweka watu wote huru: iwe katika siasa au katika nyanja yoyote ya kijamii.
Kwa sababu hiyo tunaamini ujenzi wa jamii yenye misingi ya haki ni wajibu wetu sote lakini serikali, mahakama na Bunge linawajibika kujenga dhamira hiyo.
Mahakama itambue kama ni taasisi ya kupigania haki, serikali ni wakala wa haki vivyo hivyo hata Bunge.
viongozi wakiwamo wale wa kisiasa, na wananchi watambue kuwa wao ni wawajibikaji katika shughuli za kijamii na iwapo wote hawa watauzingatia ukweli ndani ya dhamiri zao zilizojengwa juu ya ukweli na ukweli tupu, basi jamii ina uhakika wa kujenga haki na amani na matokeo ya hayo ni kupaa kimaendeleo.