24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

HAKI HAIPATIKANI KWA KISASI, KISASI HUZAA KISASI

KATIKA kazi tunazozifanya tunakutana na mambo mengi yanayotokana na ukiukwaji wa haki za binadamu. Katika kukiukwa kwa haki za binadamu, kuna mambo ambayo ukisikia mtu amefanyiwa  unashangaa sana inakuwaje binadamu anaweza kumfanyia binadamu mwenzake jambo kama hili?

Hivi karibuni kuna dada mmoja alisimulia kisa kilichohuzunisha sana. Alinieleza jinsi ambavyo ndugu zake kwa kudhani wanamsaidia walimnyang’anya mtoto wa miezi mitano ili ati wamsaidie kulea.

Walimvizia akiwa hayupo nyumbani wakamchukua mtoto wake huyo na hakujua kapelekwa wapi na iwapo ni mzima au la. Walikaa na mtoto wakimwaminisha kuwa mama yake amekufa hadi mtoto amekuwa mkubwa kabisa anakaribia kumaliza masomo ya sekondari ndiyo mama huyu akaletewa mwanawe. Hili ni jambo la kikatili sana.

Kuna siku katika kazi tulipata taarifa ya watu waliowaua watu wengine kwa njia za ukatili kabisa hadi mmoja wetu akasema kuwa pamoja kuwa tunapinga adhabu ya kifo, mambo mengine yanaudhi sana unaweza kutamani kuifungulia adhabu hiyo kwa muda ili watu wa sampuli hii washughulikiwe.

Pia niliona kwenye mitandao ya kijamii mwanamume aliyempiga mke wake vibaya sana karibu ampofushe jicho na ndugu za yule mke ambao ni baba yake na kaka zake walimshughulikia yule mwanamume vilivyo, walimpiga hadharani na kupasua pasua vioo vya gari lake na kuliponda ponda.

Walichukia sana alivyoweza kumpiga dada yao kiasi kile, waliona dawa na yeye apigwe na alipigwa barabara. Ili mradi yako mambo mengi sana watu wanayoyafanya yanatia watu wengine hasira kupitiliza.

Hata hii hali iliyozuka nchini ya watu kuwakatakata watu wenye ualbino na kuwaua ama kufukua makaburi, imeleta ghadhabu kubwa kiasi cha watu wengine kuona  kuwa watu wakikamatwa bora wauawe.

Ni hivi kama nilivyojadili wiki iliyopita, tumeshuhudia kwa maumivu na masikitiko makubwa askari wanane wa Jeshi la Polisi wakiuawa. Hili nalo lilikuwa tukio baya sana na kama nilivyosema lilikuwa ni tukio la kulaaniwa na ndivyo tulivyofanya.

Hata hivyo, kwa kiasi tukio hili lilivyoumiza tumeona  Jeshi la Polisi likifanya bidiii  kuwasaka watu hao waliofanya unyama huu. Watu waliofanya ukatili huu kwa kweli walitakiwa wapatikane na wapatiwe adhabu stahiki. Jambo ambalo limeendelea kutokea huko naona  linaleta hofu kubwa kuwa pamoja na kuwa askari wanajaribu kuwapata wahalifu wale, inaelekea kulipiza kisasi zaidi ya  kutafuta haki kwa wale waliopotezewa maisha yao.

Nimepokea waraka ulioandikwa  kuelezea hali  ya watu huko Kibiti  kutokana na msako unaofanywa na polisi. Inaonekana msako huo umeleta kadhia kubwa sana ya watu kuumizwa wengine kuuawa na pia kuna kutishwa kwa hali ya juu, unasema waraka huo.

Ninaelewa kabisa jinsi suala hili na mengine ya aina hii yanavyopaswa kukemewa na kushughulikiwa kwa kiasi kwamba hayatajirudia tena. Hata hivyo,  kinachotakiwa kufanyika ni weledi zaidi ya hasira  vinavyoweza kuleta kisasi badala ya kutibu tatizo.

Kisasi huzaa kisasi. Hawa watu wanaoumizwa kwa ujumla wao wanaweza kuweka na wao visasi mioyoni mwao na mwisho wake wakashindwa kuisadia polisi pale wanapohitajika kufanya hivyo.

Nimemkumbuka sana aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini, Hayati Nelson  Mandela. Huyu alikuwa mwanasheria na alijaribu kutafuta haki kutoka kwenye makucha ya makaburu wa Afrika Kusini wakati ambao kufanya hivyo kulionekana kuwa ni uhaini. Alikamatwa na kuwekwa ndani na kisha  alipatikana na hatia ya uhaini na kufungwa maisha.

Katika utetezi wake ambao uko katika andiko  na hata sauti  iliyorekodiwa, alikuwa akirudia maneno haya: “And that’s why I am willing to die” yaani na kwa ajili hiyo niko tayari kufa.

Alikuwa tayari kufa akitetea haki yake na wananchi wenzake. Alipofungwa jela, aliteseka sana kwa mujibu wa kitabu chake. Hata kuna wakati aliugua ugonjwa wa kifua kikuu akiwa huko huko jela. Alipoachiliwa  baada ya miaka 27 jela ya mateso, watu walifurahi na hata walimchagua kuwa rais wa nchi yao.

Kitu kikubwa sana alichokifanya Mandela ni kutafuta suluhu na kusamehe. Kwa jinsi ambavyo tulikuwa tunasikia mambo yalivyokuwa Afrika Kusini, wapo waliotazamia ndugu Mandela aanze kuwashughulikia hawa watu waliomtesa kiasi kile. Waliomfunga kwa dhuluma  kwa miaka 27.

Akiwa kifungoni aliona mateso na ukatili mkubwa na si yeye tu na watu wengine wengi hasa weusi. Hakufanya hivyo. Nilipata fursa ya kwenda kutembelea Robben Island, kisiwa chenye gereza kuu alilokuwa amefungwa Mandela kwa muda mwingi. Sasa hivi kimegeuka kuwa  sehemu ya utalii.

Huko nilikuta watu waliokuwa wanahudumu wengine ni  wale waliowahi kufungwa huko. Tulimkuta kijana mmoja akiwa na umri wa miaka 35 ambaye alifungwa akiwa mtoto mdogo wa miaka 15 na alitoka baada ya Mandela kufunguliwa na Afrika Kusini kuwa huru na ubaguzi.

Alitusimulia jinsi ambavyo yeye na wenzake walivyoamua kwenda kumuona askari mkuu wa gereza lile aliyekuwa anawatesa sana. Aliposikia kuna watu waliotoka Robben Island wanataka kumuona wakati huo akiwa mgonjwa amedhoofu  aliogopa sana. Vijana wale wanasema walienda kumtangazia msamaha. Walisema hakuna chochote ambacho wangemfanyia ambacho kingeweza kulipiza yale aliyowafanyia. Msamaha waliona ndiyo nafuu yao maana hata wangemlipiza kisasi asingeweza kuumia kiasi wao walivyoumia.

Yule kijana alipokuwa anatusimulia wale wenye machozi ya karibu walilia sana wakisikiliza mateso aliyoyapata, lakini hakuwa na nia ya kulipiza kisasi.

Hapo ndipo nilitafakari dhana ya haki. Haki ni stahiki. Hukumu  ni malipo ya haki kwa aliyekosea na kisasi ni kurudia  kitu kiovu alichokifanya mwovu. Kisasi kinamfanya anayekitenda kurudia kile alichotendewa ambacho yeye hakukipenda na kwa kutokipenda ameamua na yeye amrudishie aliyemtendea. Wapo wanaodhani kuwa ni sawa mtendaji atendewe.

Tukiongea lugha ya haki  kisasi si haki. Hukumu kwa mujibu wa sheria na mifumo ya  haki ni haki ya yule anayeipokea. Lakini hukumu kwa mifumo  isiyo haki kama vile ubaguzi uliokuwa unaendelea Afrika Kusini  si haki.

Nimeongea mifano kadhaa na ukiiangalia unaweza usione inaungana vipi. Ninachojaribu kusema ni kuwa yapo mambo yanayovunja haki za watu kwa njia mbalimbali. Mfano haki inayoweza kuvunjwa kwa masuala ya kijamii kama mfano wa mama aliyenyang'anywa mtoto, ukatili mwingine kama wa kuua watu kama albino au vikongwe kwa sababu mbalimbali zikiwemo za kishirikina na hata mauaji yanayofanywa na wahalifu kama majambazi na watu kama wale waliowaua askari.

Haya yote yanastahili kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria. Nchi yetu ina sheria hata  kama zina upungufu lakini zipo. Kila anayetendewa akiamua na yeye kutenda alichotendewa kisasi hakina mwisho, ndiyo maana zipo sheria zinazowezesha mkosaji kusaidiwa.

Kwa vile polisi wameumizwa kama wengine wanavyoumizwa, ingefaa wao wasishiriki kabisa katika  kutafuta waliotenda matendo yale kwa vile ni rahisi sana kutumbukia kweye wimbi la kisasi badala ya kutafuta haki. Kisasi si haki na kisasi huweza kuendeleza kisasi. Ndiyo maana kwa kuacha kulipiza kisasi, Afrika Kusini wamejaribu kuishi na wale waliowaumiza ila walitafuta suluhu.

Tushauri  weledi utawale na si hasira wala kisasi.

Dk. Helen KijoBisimba

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles