27.5 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

HAIWEZEKANI KUPIGA KURA KUMTOA MADARAKANI TRUMP

Na SUBI SABATO, MAREKANI


MJADALA kuhusu uwezekano wa kuondolewa madarakani Rais Donald Trump, umeshika kasi maeneo mbalimbali duniani. Hapa Marekani ni jambo linalozungumzwa kila kukicha, siasa zao zimetawaliwa na mambo mengi, vituko vingi na kadhalika. Lakini swali je, inawezekana kumtoa madarakani Trump? Nitajibu swali hili kwa mifano na kifupi.

Kwa mujibu wa sheria na Katiba ya Marekani, haiwezekani kumshtaki rais aliyepo madarakani katika kesi ambayo inamlazimu kuhudhuria mahakamani na yenye makosa ya kihalifu (Criminal case).

Hivi ni vitu nyeti sana, ambavyo vinabeba uzito unaoweza kumwondoa rais madarakani, isipokuwa wabunge wa Baraza la Wawakilishi (chemba ya kwanza hii ina wabunge 435), watafikisha bungeni ibara za kumpigia kura za kutokuwa na imani naye na kutangaza kusudio lao kuhusu tuhuma zinazohusu kiongozi wa Serikali, ambapo safari hii ni Rais, kisha ipigwe kura kuwapata wabunge 218 wanaounga mkono hoja ya kumng’oa Trump.

Ikiwa watafanikiwa, hoja hiyo italazimika kupelekwa kwenye Baraza la Seneti. Muundo wa Bunge la Marekani, Seneti ni chemba ya pili ya baraza la wawakilishi ambayo inao wabunge 50 wenye mamlaka ya kutoa hukumu ikiwa theluthi mbili ya wabunge hao wataridhia kuondolewa kwa Rais Trump.

Hadi sasa katika historia ya Marekani ni marais, Andrew Johnson, Richard Nixon na Bill Clinton, wamewahi kupigiwa kura ya kutokuwa na imani nao. Marais Johnson na Clinon, waliokolewa na Baraza la Seneti baada ya kukosekana kura za kutosha ili kuwaondoa madarakani na hivyo walifanikiwa kumaliza vipindi vyao wakati huo.

Rais Nixon baada ya kugundua uhusika wake katika kashfa ya Watergate na kuwepo uwezekano mkubwa wa kuitwa katika baraza la Seneti ili kujitetea, alimtaka mwanasheria mkuu wa Serikali amfute kazi mchunguzi wa kesi ya Watergate.

Lakini mwanasheria mkuu alipokataa na kujiuzulu kwa kujua kosa, Nixon alimfuta kazi mwendesha mashtaka mkuu wa Serikali na hapo ndipo alipojipalia makaa zaidi. Baada ya kutambua kuwa amejiongezea makosa katika harakati za kuficha ukweli wa makosa ya awali, Rais Nixon, aliamua kuachia ngazi.

Tangu aingie madarakani Rais Trump kumekuwa na mazungumzo na tetesi za kwamba Rais hapendezwi na uchunguzi unaofanywa na mwendesha mashtaka mkuu wa sasa, Robert Mueller, kwamba Rais alitarajia kuwa mwanasheria mkuu wa Serikali wa sasa, Jeff Sessions, angekuwa na uwezo wa kuingilia kati, lakini kwa bahati mbaya haiwezekani kwa kuwa Sessions alishajitoa kuhusiana na uchunguzi huo kutokana na baadhi ya makosa ambayo tayari yalishatilia mashaka na walakini endapo akijihusisha angekuwa katika maamuzi yasiyoingiliwa wala kuvutia upande wowote.

Kutokana na ukweli huu, Rais sasa anabakiwa na uchaguzi wa kumfuta kazi Sessions ili aweze kumweka mwanasheria mkuu mwingine. Hata hivyo, hilo halitamzuia kumfuta Mueller na kumweka mwingine au rais aamue mwenyewe kumtimua kazi Mueller kama alivyofanya Nixon.

Hili la pili wanachelea historia isijirudie. Hilo la kwanza bado ni vuta nikuvute ndiyo maana tunaona malumbano kwenye ukurasa wa Trump wa Twitter dhidi ya Sessions akidhani itasababisha ajiuzulu bila kutimuliwa, lakini mara zote Sessions ametoa tu majibu kwa wanahabari wanapouliza au kutolea majibu ya kimaandishi.

Linakuja suala la je, inawezekana kumtoa Trump madarakani kwa kumpigia kura ya kutokuwa na imani naye? Jibu ni kwamba haiwezekani kwa hali ilivyo wakati huu hata ikiwa kuwa washirika wake watano wa kibiashara na kwenye kampeni za uchaguzi za kisiasa za uchaguzi mkuu wa mwaka 2016 na baadaye uongozi serikalini.

Kwa mfano Michael Cohen, Paul Manafort, George Papadopoulos na wengine waliokutwa na makosa baada ya baadhi ya ripoti za uchunguzi wa Mueller kufikishwa kortini, kwa sababu mosi, ya ile sheria niliyotaja hapo awali kuwa huwezi kumshtaki moja kwa moja rais aliyepo madarakani ikiwa mashtaka hayo yatamtaka ahudhurie kesi na yanaweza kumtoa madarakani.

Hii italeta mkanganyiko mkubwa sana ikiruhusiwa kwa sababu hataweza kuendesha Serikali na hakuna ajuaye kwa muda gani kutokana na ukweli kwamba kesi hazina muda maalumu mpaka kufikia hukumu, inaweza kuchukua muda mrefu sana.

Pili, ni ile niliyozungumzia awali kuhusu Baraza la Kongresi (House of Senate) kwamba ni lazima wapate makosa yote anayotuhumiwa rais, wajiridhishe kuwa uhaini, rushwa, makosa makubwa ya kihalifu, wapige kura na wafanikiwe katika chemba zote mbili ndipo katiba ifuate mkondo wake.

Kwa hali ilivyo, chama cha Democrats kimejitahidi mara kadhaa kupeleka hizo ‘articles of impeachment’ lakini haiwezekani kwa sababu wana hoja hafifu na hivyo hawana jinsi hali kusubiri mpaka uchunguzi wa Mueller ukamilike watumie ripoti yake au waombee rais Trump afanye kosa wakati huu.

Sababu nyingine ni kwamba, chemba zote zinashikiliwa na wabunge wa chama cha Republicans ambao hawana nia ya kumwondoa madarakani rais anayetokana na chama chao.

Kwa hiyo turufu inabaki kwa chama cha Democrats ambao wanapaswa kushinda wabunge wengi kwenye uchaguzi wa wabunge miezi mitatu ijayo kutoka sasa, ili wawe wengi wa kutosha kupiga kura au ikiwezekana wafanikiwe kuwashawishi na kuwageuza nia baadhi ya wabunge wa upande wa chama cha Republicans.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles