HABARI NJEMA KWA WAGONJWA SARATANI YA TEZI DUME

0
1619
Saratani ya tezi dume huwakumba hadi vijana

 

NA JOSEPH HIZA,

MOJA ya maradhi yanayoshuhudia kampeni kubwa kukabiliana nayo katika miaka ya hivi karibuni duniani ni pamoja na saratani ya tezi dume kutokana na ukubwa wa athari inazosababisha.

Ni maradhi yanayoshika nafasi ya tatu kwa kusababisha vifo vinavyotokana na saratani kwa wanaume duniani.

Pia ni chanzo kikuu cha vifo vinavyosababishwa na saratani kwa wanaume wenye umri wa miaka 70 na kuendelea.

Hata hivyo, satarani ya tezi dume kwa sasa inawapata zaidi wanaume kuanzia miaka 25.

Tafiti za Chama cha Saratani cha Marekani (ACS) na cha Afrika Kusini (CANSA) zimebaini kuwa, mwanamume mmoja kati ya sita hupata saratani ya tezi dume katika uhai wake. 

Kutokana na takwimu za mwaka 2010 za dunia nzima, malaria iliua watu 500,000, kifua kikuu watu milioni 2.1, Ukimwi watu milioni 1.8 na saratani watu milioni 9.9.

Takwimu hizo ni ushuhuda kuwa idadi ya watu waliofariki dunia kutokana na ugonjwa wa saratani ni kubwa ikilinganishwa na ya magonjwa mengine

Ni ugonjwa hatari ambao usipobainika na kutibiwa mapema inakuwa tiketi ya kifo.

Lakini habari njema zilizoibuka sasa kuhusu ugonjwa huo ni kuwa moja ya majaribio makubwa kabisa ya kimaabara kwa ajili ya saratani ya tezi dume yametoa matokeo mazuri mno, kwa mujibu ya watafiti wa Uingereza.

Dawa ya kutibu saratani ya tezi dume ambayo imesambaa imebainika kuokoa maisha wakati ilipotolewa mapema kwa mgonjwa, kwa mujibu wa utafiti wao.

Majaribio hayo yaliitazama tiba mpya ya homoni ijulikanayo kama abiraterone kama inayotolewa kwa ziada kwa matibabu wapewayo wagonjwa wenye saratani ya tezi dume, ambao walikuwa waanze tiba ya kipindi kirefu ya homoni.

Profesa Nicholas James wa Chuo Kikuu cha Birmingham nchini Uingereza, ambaye aliongoza utafiti huo alisema: “Haya ni matokeo yenye nguvu zaidi niliyowahi kushuhudia kuhusu saratani ya tezi dume – ni kama vile hutokea mara moja katika safari yetu ya kikazi.

“Hii ni moja ya upunguzaji mkubwa wa vifo niliyowahi kushuhudia katika majaribio ya kimaabara kwa wagonwa wazee wenye saratani."

Abiraterone, ambayo pia huitwa Zytiga, ni tiba ya homoni. Ni tofauti na chemotherapy, ambayo huua seli za saratani, hii huzua zaidi homoni za testosterone kuzifikia tezi za kibofu zisije tengeneza uvimbe.

Majaribo hayo yalihusisha wagonjwa 2,000.

Nusu ya wanaume waliotibiwa na tiba ya homoni wakati nusu wengine walipokea tiba ya homoni na abiraterone.

Kati ya wanaume 1,917 walioshiriki katika jaribio hilo, kulikuwa na vifo 184 katika kundi la wale waliopewa mseto wa dawa kulinganisha na 262 waliopewa tiba moja tu ya homoni.

Profess James aliongeza: "Abiraterone tayari inatumika kutibu baadhi ya wanaume, ambao maradhi yamesambaa lakini matokeo yetu yameonesha kuwa wengi zaidi wanaweza kunufaika nayo.”

Kila mwaka wanaume 46,500 wanabainika kuwa na saratani ya tezi dume nchini Uingereza huku 11,000 wakifariki dunia kutokana na maradhi hayo.

Matokeo ya majaribio hayo yaliwasilishwa katika Mkutano wa Mwaka wa Chama cha Tiba ya Vivimbe Marekani (ASCO) mjini Chicago na kuchapishwa na Jarida la Utabibu la New England mwishoni mwa wiki iliyopita.

Mtendaji Mkuu wa Tasasisi ya Utafiti wa Saratani(ICR), Sir Harpal Kumar, alisema: “Matokeo yanaweza kuleta mageuzi chanya katika matibabu ya saratani ya tezi dume.

“Abiraterone inaweza kabisa kuwasaidia wagonjwa wengi zaidi wa saratani ya tezi dume kuliko ilivyodhaniwa kabla."

ICR pia imeyakaribisha matokeo hayo mapya ya aina yake katika harakati za kutafuta tiba sahihi ya maradhi haya.

Profesa Johann de Bono alisema matokeo yalionesha kwamba wakati zilipotumika mwanzo wa matibabu, abiraterone zilikuwa na manufaa mazuri kwa wagonjwa.

Machi mwaka huu, wagonjwa wa saratani ya tezi dume nchini England waliambiwa kwamba watapatiwa mapema tiba ya abiraterone.

Taasisi ya Taifa ya Afya na Huduma Nzuri (NICE) awali ilisema matibabu hayakuwa nafuu kigharama kwa Taasisi ya Taifa ya Huduma za Afya (NHS) hadi saratani zitakapokuwa katika hatua fulani.

Profesa Paul Workman, , alisema kwamba anatarajkoa kuiona abiraterone inapitiwa upya na NICE kwa matumizi ya wagonjwa mapema kadir iwezekanavyo.

Saratani ya tezi dume ni nini?

Neno saratani hutokea wakati chembe chembe za uhai au seli katika sehemu fulani ya mwili zinapoanza kukua bila kufuata utaratibu wa mfumo wa mwili na kutengeneza vijiuvimbe vidogo vidogo.

Kwa kawaida seli huwa zinajigawa, kupevuka na baadaye kufa kwa kufuata taratibu za mfumo wa mwili. Lakini seli za saratani hazifuati mfumo huo.

Badala ya kufa, zenyewe huishi muda mrefu kuliko chembe chembe za kawaida na wakati huo huo huendelea kutengeneza seli nyingine na kuwa uvimbe wa saratani.

Tezi dume hutokea katika mwili wa mamalia wa kiume pekee pale seli katika kiungo hicho zinapoanza kukua bila kufuata utaratibu wa mfumo wa mwili hapo ndipo mtu hupata saratani ya tezi dume.

Ugonjwa huu pia hujulikana kama saratani ya kipofu cha mkojo. Kuna visababishi vingi vinavyochangia mwanaume kupata saratani ya tezi dume.

Vifuatavyo ni baadhi yake: Kwanza kabisa ni umri. Nafasi ya kupata saratani ya tezi dume huongezeka sana hasa ukifikia umri wa karibu miaka 50 na kuendelea.

Nasaba ni kihatarishi kingine ambapo wanaume wenye historia ya tatizo hili kwenye familia zao, yaani wale ambao mmoja wa ndugu zao wamewahi kuugua ugonjwa huu huwa katika hatarini ya kupata kansa hiyo kutokana na kurithi jeni za ugonjwa huo.

Suala jingie ni lishe ambapo wanaume wanaopenda kula nyama na walaji wa chakula chenye kiasi kikubwa cha mafuta hasa ya wanyama huwa katika hatari kubwa ya kupata saratani ya tezi dume wisho

Katika hatua zake za awali, dalili za saratani ya tezi dume hazitofautiani na zile za kuvimba kwa tezi dume . Dalili hizo ni pamoja naKupata shida wakati wa kuanza kukojoa, kutiririka kwa mkojo baada ya kumaliza kukojoa, kukojoa mkojo wenye mtiririko dhaifu.

Kadhalika kukojoa mara kwa mara hasa nyakati za usiku, Kujikakamua wakati wa kukojoa na kushindwa kumaliza mkojo wote na kutoa mkojo uliochanganyika na damu.

Pamoja na kueleza dalili hizo inapaswa kutambulika kuwa, mwanaume anapoanza kuona na kuhisi baadhi ya dalili hizo, anapaswa kujua kuwa, seli za saratani katika tezi dume lake huwa zina umri wa takribani miaka saba na kuendelea.

Iwapo saratani imesambaa mwilini kiasi cha kuhusisha sehemu nyigine za mwili, mgonjwa anaweza kuwa na maumivu makali ya mifupa katika maeneo ya nyonga, mapajani na kiunoni.

Aidha mgonjwa huwa na dalili nyingine zinazoweza kumpata mgonjwa mwingine yeyote wa saratani kama vile kupungua uzito, kuhisi kichefuchefu, uchovu, kizunguzungu na kadhalika.

Wanaume wanashauriwa kufanyiwa uchunguzi kwa kuwa imegundulika kuwa wanaume wengi wakiziona na kuzihisi dalili hizo huona soni kwenda kumwona daktari.

Baadhi ya watu huzihusisha na magonjwa ya zinaa au na dhana potofu za kishirikina.

Wapo wanaokwenda mbali zaidi hata kuuita ugonjwa huo kuwa ni wanaume wanaopenda uhusiano wa kinyume na maumbile huku wengine wakiurahisisha kwa kuuita kuwa ni ugonjwa wa utu uzima kana kwamba saratani ya tezi dume ni jambo la kawaida kwa watu wazee.

Mambo kama hayo hupelekea wanaume wengi kujinyanyapaa wenyewe na hata wengine kujitibu kwa uficho au kwa kutumia waganga wababaishaji mpaka pale mambo yanapokuwa yamewazidi ndipo hupelekwa hospitalini na mara nyingine huwa wamechelewa na kupoteza maisha yao bure kwa ugonjwa ambao ungeweza kutibiwa mapema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here