CAIRO, MISRI
BAADA ya timu ya taifa Ghana kuweka kambi nchini Dubai kwa wiki kadhaa, nyota wa timu hiyo Asamoah Gyan, amethibitisha kuwa wapo tayari kwa ajili ya michuano hiyo ya Mataifa ya Afrika nchini Misri.
Timu hiyo imepangwa kwenye Kundi F ikiwa pamoja na timu zingine kama vile Cameroon, Benin na Guinea-Bissau, huku Ghana ikitarajia kuanza mchezo wao wa kwanza dhidi ya Benin kwenye uwanja wa Ismailia, Juni 25.
Gyan amekuwa nyota wa Ghana ambaye ameingia kwenye historia ya kuwa mfungaji bora wa kipindi chote, hivyo ameweka wazi kuwa, kikosi hicho kipo tayari kwa ajili ya kupambana.
Ghana wamewahi kuchukua taji hilo mara nne katika historia yao huku mara ya mwisho kulichukua ilikuwa mwaka 1982, lakini safari hii wanaonekana kujiandaa kwa ajili ya kutaka kuandika historia mpya.
“Tupo tayari kwa ajili ya michuano hiyo, tumefanya mazoezi ya nguvu kwa kipindi cha siku 10 na sasa tunaamini tumekamilika kwa kuwa hadi sasa hakuna mchezaji ambaye ni majeruhi kutokana na kambi hiyo,” hivyo mashabiki wakae tayari,” alisema mchezaji huyo. Siku chache kabla ya kutajwa kikosi cha timu ya taifa Ghana, mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 33, alitangaza kustaafu kuitumikia timu hiyo, lakini rais wa nchi Nana Akufo-Addo, alimtaka mchezaji huyo kubadilisha maamuzi hadi pale itakapo malizika michuano hiyo