Na EVANCE MAGEGE -Muleba
MHARIRI wa Mafunzo wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd ambaye ni gwiji wa habari nchini, Chrysostom Rweyemamu, amezikwa jana nyumbani kwao katika Kijiji cha Iyunga, Wilaya ya Muleba mkoani Kagera.
Watu mbalimbali walihudhuria mazishi hayo, akiwamo aliyekuwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Alfred Tibaigana.
Mazishi hayo yaliongozwa na Paroko, Revocatus Miruko wa Parokia ya Rukindo, ambaye alisema kifo cha Rweyemamu kinawafundisha wanadamu kufahamu maisha ya duniani ni sawa na mshumaa ambao huwaka na kuzima.
Alisema binadamu wote ni wasafiri hapa duniani kwa hiyo maisha yetu huisha kama mshumaa unavyowaka.
“Rweyemamu ni mtu wa watu, kaacha vitu mbalimbali milele na hiyo inatufundisha kutenda mema ungali mchana kwa kuwa usiku ukifika hatutakuwa na muda wa kutosha wa kujiandaa kufanya matendo mema.
“Katika maisha na kifo, kiashiria chake kikubwa ni kuishi kwa matendo mema kwa sababu kila binadamu atavuna alichopanda na ikumbukwe kuwa binadamu duniani hapa si sehemu yetu kwani tumeandaliwa mahali pengine kwa kuishi milele,” alisema Paroko Miruko.
Kabla ya misa ya mazishi, mama mzazi wa marehemu, Martha Rweyemamu, alisema kuwa ameupokea msiba wa mwanawe kwa mikono miwili kwa sababu anajua haya ni mapenzi ya Mwenyezi Mungu.
Alisema mwanawe alimtegemea na alimpenda, lakini anaamini Mungu ndiye amempenda zaidi, hivyo hakuna binadamu yeyote wa kupinga chochote juu ya kifo.
Naye Mhariri Mtendaji wa Gazeti la MTANZANIA, Denis Msacky, alisema kifo cha Rweyemamu si pigo kwa familia tu, bali na kwa tasnia nzima ya habari na Kampuni ya New Habari (2006) Ltd alikokuwa akifanya kazi.
“Pengo lake haonekani wa kuliziba na kwamba kampuni itamuenzi kwa miongozo yake mbalimbali ya kihabari. Poleni sana wanafamilia na ndugu kwa msiba huu,” alisema Msacky.
Mwakilishi wa majirani aliyejitambulisha kwa jina moja la Cecylia, alisema alimfahamu Rweyemamu tangu mwaka 1965 na amemlelea hadi watoto wake.
Alisema alikuwa ni mtu aliyependwa na wanakijiji wote na alikuwa akiwaalika kumtembelea Dar es Salaam alikokuwa akiishi.
Rweyemamu alifariki dunia Mei 27, mwaka huu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Awali mtoto wa marehemu, George Chrysostom, alisema baba yake alikuwa akisumbuliwa na uvimbe tumboni na alifanyiwa upasuaji vizuri, lakini hali ilibadilika ghafla na kupoteza uhai.
Alisema daktari aliyekuwa akimtibu kabla ya kufikwa na umauti, aliwaeleza kuwa baba yao alianza kupata shida ya kupumua ghafla hatua iliyosababisha kupoteza uhai.