PATRICIA KIMELEMETA NA MANENO SELANYIKA
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemuachia huru Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima na wenzake watatu waliokua wakikabiliwa na shtaka la kushindwa kutunza silaha.
Uamuzi huo umetolewa jana na Hakimu Mfawidhi Cyprian Mkeha, wakati alipokua akisoma hukumu hiyo.
Alisema mahakama imeamua kuchukua uamuzi huo baada ya kupitia maelezo ya ushahidi yaliyotolewa na pande zote mbili ambazo ni upande wa mashtaka na ule wa utetezi.
Alisema baada ya kupitia maelezo hayo, upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha makosa yanayowakabili washtakiwa.
“Nimeamua kumuachia huru Gwajima na wenzake watatu katika kesi yao ya kushindwa kutunza silaha kwa sababu upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha mashtaka yanayowakabili katika ushahidi.
Alisema katika kesi hiyo, mashahidi walikuwa 10 ambapo upande wa mashtaka ulileta mashahidi 4 na ule wa utetezi ulikuwa na mashahidi 6.
Awali wakili wa Serikali, Inspekta Hamisi Saidi, alidai mahakamani hapo kesi hiyo ilisomewa hukumu huku upande wa utetezi ulikuwa unasimamiwa na Wakili Peter Kibatala.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni George Msava ambaye ni Msaidizi wa askofu Gwajima, Yekonai Bihagaze na George Milulu.