Na AGATHA CHARLES – Dar es Salaam
RAIS Dk. John Magufuli amewatunuku kamisheni maofisa 194 wa Jeshi la Wananchi la Tanzania (JWTZ) katika hafla iliyofanyika kwa mara ya kwanza Ikulu, Dar es Salaam.
Hafla hiyo iliyofanyika jana, imeacha gumzo ikiwa ni mara ya kwanza kamisheni kutolewa ndani ya Ikulu na pia nje ya Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi Monduli, Arusha tangu kilipohamishiwa huko mwaka 1976.
Inaelezwa kuwa ni desturi kwa marais wote waliotangulia kwenda Monduli ili kutunuku vyeo hivyo tangu chuo hicho kilipohamishiwa huko.
Baadhi ya wadadisi wanasema uamuzi wa Rais Magufuli kuwatunuku maofisa hao Ikulu tofauti na watangulizi wake waliokuwa wanakwenda chuoni hapo, unatokana na sera yake ya kubana matumizi.
Hata hivyo, wapo wanaopinga hoja hiyo wakidai kuwa upo uwezekano gharama zilizotumika tangu kuwasafirisha maofisa hao na kufanya hafla hiyo zikawa ni kubwa.
Katika hafla hiyo, maofisa hao wa awamu ya 59 (Refu), wanaume 168 na wanawake 26, walitunukiwa cheo cha luteni usu huku watatu kati yao wakipatiwa zawadi kutokana na kufanya vyema katika mafunzo hayo.
Kupitia taarifa iliyosambazwa kwa vyombo vya habari jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa, Rais Magufuli aliamua tukio hilo lifanyike Ikulu kwa lengo la kutoa heshima kwa maofisa wa JWTZ, kama ambavyo viongozi wengine serikalini wamekuwa wakipata heshima ya kuapishiwa hapo.
Magufuli aliitoa kauli hiyo baada ya chakula cha mchana katika ukumbi wa Ikulu.
“Kwamba mawaziri tunapotaka kuwaapisha tunawaapishia hapa, wakuu wa mikoa tunawaapishia hapahapa, makatibu wakuu tunawaapishia hapahapa, kwanini hawa maofisa wa jeshi tusiwaapishie hapahapa kwenye nyumba yao? Nyinyi ndio mnalinda nchi, nyinyi ndio mnasimamia usalama wa nchi hii, lakini nikiuliza hapa inawezekana wengine mpaka wamekuwa mabrigedia jenerali hawajawahi kukanyaga Ikulu, wakati hapa ni kwenu,” alisema Magufuli.
Pia alipongeza juhudi za Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Davis Mwamunyange, makamanda na askari wote wa JWTZ kwa jukumu kubwa wanalolitekeleza la kuhakikisha nchi ipo salama.
Alisema Serikali itahakikisha inaboresha zaidi masilahi na mazingira ya kazi kwa jeshi hilo na vyombo vingine vya ulinzi na usalama.
Awali, akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa chuo hicho, Meja Jenerali Paul Peter Massao, alisema maofisa hao wote ni Watanzania, huku kati yao akiwapo mmoja aliyesoma nchini Uingereza na alikuja hapa nchini ili kutunukiwa na wenzake kwa mujibu wa taratibu.