GUARDIOLA ATAMANI KUFUNDISHA TIMU YA TAIFA LAKINI SI HISPANIA

0
1342

LONDON, ENGLAND


Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola, amesema ana ndoto ya kuifundisha timu ya taifa siku moja lakini si timu ya taifa lake la Hispania.

Guardiola ameshinda makombe 47 kwa ujumla ya Hispania akiwa mchezaji wa timu ya taifa na nahodha wa timu ya Barcelona na kuvishwa nishani ya fedha katika michuano ya Olimpiki mwaka 1992.

Tangu amekuwa kocha ameshinda mataji 27, hii ni pamoja na akiwa Barcelona, Bayern Munich na Manchester City.

Kocha huyo mwenye umri wa miaka 47 mkataba wake wa kuifundisha Manchester City unamalizika mwaka 2021, lakini anaweza kukubali kuvunja mkataba wake na kusaini mkataba wa muda mrefu iwapo atahitajika na taifa lingine kufundisha.

Kocha huyo alipoulizwa kuhusu kuifundisha Hispania alisema: “Kamwe jambo hilo haliwezi kutokea,” alisema juzi katika mkutano na waandishi wa habari kabla ya mchezo wa Ligi Kuu England dhidi ya Fulham.

Hata hivyo, hakusema sababu za kukataa kufundisha timu ya Hispania, ingawa hakuwahi kuficha hisia zake kwamba anafurahi kuwa raia wa Catalunya.

Msimu uliopita Guardiola alipigwa faini baada ya kuvaa kitambaa cha njano ambacho kiliashiria kuunga mkono mambo ya kisiasa yaliyokuwa yakiendelea eneo la Catalunya.

Akizungumzia kufundisha timu ya taifa, baada ya kuhusishwa kutakiwa na timu ya Argentina, Guardiola, alisema: “Katika maisha yetu tuna ndoto za kitu gani unapenda kukifanya hapo baadaye, lakini haina maana kwamba inaweza kutokea.

“Napenda kuwa katika michuano ya Kombe la Dunia, Ligi za Ulaya, napenda hali hiyo, kwani inanivutia niwepo, nilikuwa na nafasi moja tu ya kufanya hivyo nikiwa katika timu ya taifa.

“Katika miaka 12, 14 ijayo labda inaweza kutokea tena. Ni ndoto tu kama kocha na binadamu, inawezekana ikatokea au isitokee.”

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here