MANCHESTER, ENGLAND
BAADA ya timu ya Manchester City kukubali kichapo cha mabao 2-0, juzi dhidi ya Wolves kwenye michuano ya Ligi Kuu nchini England, kocha wa timu hiyo Pep Guardiola amewatuliza mashabiki wa timu hiyo huku akiwaambia bado wana nafasi ya kutetea ubingwa.
Mchezo huo ulikuwa wa nane tangu kuanza kwa msimu huu, hivyo Manchester City wanashika nafasi ya pili wakiwa na pointi 16 baada ya kukubali kufungwa michezo miwili, sara mmoja na kushinda michezo mitano, wakati huo Liverpool wakishinda michezo yote na kuwafanya wawe na pointi 24.
Mbali na kuanza vibaya msimu huu, kocha huyo anaamini bado michezo imebaki mingi hadi kumaliza msimu hivyo mashabiki wasiwe na wasiwasi wana nafasi ya kutetea ubingwa japokuwa wameachwa nyuma pointi nane.
“Jamani! Hapana kuna michezo mingi imebaki hadi kumalizika kwa msimu, tumepoteza mchezo wetu dhidi ya timu ambayo ilikuwa bora kutokana na mipango yao, walikuwa na nguvu, kasi pamoja na mipira mirefu.
“Nilikuwa ninaujua ubora wa wapinzani, lakini siku zote timu ambazo zinafanikiwa kutwaa ubingwa zinakuwa na wakati mgumu msimu unaofuata, ila bado tuna nafasi kubwa ya kufanya vizuri kwa kuwa kuna michezo mingi imebaki hadi kumalizika kwa msimu.
“Naweza kusema kwenye mchezo huo hatukuwa kwenye ubora wetu, lakini wapinzani wetu Liverpool wanaendelea vizuri na hawajapoteza mchezo hata mmoja, lakini hii ni Oktoba, tutakuja kuona hadi kufikia Mei mwakani,” alisema Guardiola.
Mabingwa hao wamekuwa kwenye kipindi kigumu kutokana na kuwakosa nyota wake katika safu ya ulinzi kama vile Aymeric Laporte na John Stones ambao wanasumbuliwa na majeruhi, lakini kwa kuwakosa wachezaji hao kuna mlazimisha kocha huyo kuwatumia wachezaji kama vile Nicolas Otamendi na kiungo wake Fernandinho kucheza nafasi ya beki wa kati.