27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

GRACA MACHEL: TUWAENZI MASHUJAA WETU WAKIWA HAI

Na Leah Mushi, Afrika Kusini

Mwanaharakati wa Masuala ya Wanawake na Watoto wa Afrika, Mama Graca Machel amesema ni wakati sasa kwa taifa la Afrika Kusini kuwaita mashujaa wa taifa, kuwashukuru na kuwaenzi wakiwa hai kwa kuwa hakuna ajuaye kama wanasikia na kuona vile wanavyosifiwa wakati wa misiba yao.

Aidha, amekemea tabia ya jamii kuwananga na kuwasema watoto wa wapigania uhuru kwa kuwa wengi wao wamekosa miongozo na malezi bora ya wazazi kwani wazazi hao walikuwa na ujasiri wa kuacha familia zao na kupigania taifa hivyo si sawa kuwasema na kuwanyooshea vidole badala yake waoneshe upendo zaidi kwao katika kile kilichofanywa na wazazi wao.

Akizungumza mbele ya umati wa watu kutoka maeneo mbalimbali duniani waliofika kutoa salamu za mwisho wakati wa kuaga mwili wa Marehemu Winnie Mandela ambaye amekuwa akimuita dada mkubwa, aliyefariki dunia Aprili 2, mwaka huu nchini Afrika Kusini.

Pamoja na mambo mengine, Mama Graca ambaye pia ni mjane wa Rais wa zamani wa afrika Kusini, Hayati Nelson Mandela, amezungumzia kuhusu rambirambi na ahadi zinazotolewa misibani ambapo amewataka wananchi na wanasiasa kuacha maneno ya hadaa kwani mengi yanayoahidiwa hayatekelezwi.

“Kwa sasa ukiangalia Afrika Kusini mambo yamekuwa mabaya zaidi kuliko Mandela alipokuwa hai, na hii inaonesha kiasi gani watu hawaishi ahadi zao walizoahidi na ndiyo jambo hata leo watu wengi wameahidi kuendeleza harakati za Winnie Mandela lakini nani anajua kama zitatekelezwa?” amehoji mama Grace.

Hata hivyo, ameitaka jamii kwa ujumla kuamka na kusaidia kuinua jamii kwa kuwa zaidi ya asilimia 50 ya wananchi ni masikini na hakuna juhudi za mmoja mmoja za kulikomboa taifa katika tatizo hilo badala yake kila mtu anaitupia lawama serikali.

“Ebu jiulize, ni namna gani shujaa wa taifa angejisikia pale ambapo amekaa mbele ya watu wa rika tofauti jinsia tofauti wenye mirengo tofauti ya kisiasa wote wakimsifia na kumshukuru kwa werevu wake wa kulipigania taifa?” amesema.

Katika hotuba yake hiyo aliyoitoa kwa zaidi ya nusu saa, Mama Graca ameahidi kutomzungumzia  Winnie Mandela kwa kuwa kila mtu amekuwa akifanya hivyo na badala yake kuitaka jamii kubadilika.

Mama Graca Machel ambaye alikuwa mke wa Nelson Mandela tangu mwaka 1998 mpaka mauti yalipomkuta mwaka 2013 alikuwa rafiki wa karibu wa marehemu Winnie Mandela na wamekuwa wakishirikiana katika masuala mbalimbali ya kutetea haki za raia nchini Afrika Kusini na Afrika kwa ujumla.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles