24.5 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

GIANNI INFANTINO ATAWEZA KUMALIZA SUALA LA UTATA KWA WAAMUZI?

MARTIN MAZUGWA NA MITANDAO


HUENDA kati ya watu wanaoongoza kwa kutupiwa lawama katika mchezo wa soka ni waamuzi ambao ndio wenye dhamana ya kuufanya mchezo wa soka uwe na ladha au kuipoteza kabisa ladha hiyo kutokana na maamuzi yao.

Kila siku zinavyozidi kwenda mbio  katika mchezo wa soka ndivyo mambo yanavyozidi kuwa mengi huku makosa mbalimbali yaliyokuwa yakijitokeza siku za nyuma yakizidi kupatiwa ufumbuzi ili yasijirudie tena.

Kumekuwa na malalamiko yasiyokwisha kwa waamuzi kushindwa kuzitafsiri vyema sheria za soka huku mabao yakizidi kuwa na utata kila kukicha hivyo kufanya watu kutokuwa na imani na waamuzi.

Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) lililoanzishwa Mei 21, 1904 ni moja kati ya shirikisho kongwe na lenye wanachama wengi duniani linaloongoza mchezo wa soka ulimwenguni.

Zaidi ya marais wanane wamepita katika Shirikisho hilo huku kila rais akiacha alama zake katika shirikisho hilo kubwa ulimwenguni tangu zama za Rais wa kwanza, Robert Guerin raia wa Ufaransa ambaye aliongoza kwa kipindi cha miaka miwili hadi kwa Infantino.

Mara baada ya marais hao kupita hatimaye ni zama za Gianni Infantino  raia wa Italia ambaye hadi sasa amefikisha mwaka mmoja tangu alipoingia madarakani kumpokea Issa Hayatou aliyekuwa msimamizi mara baada ya aliyekuwa Rais wake, Sepp Blatter kuondolewa kwa kashfa ya rushwa.

Rais huyo ameamua kuja na teknolojia mpya ambayo itawasaidia waamuzi kuondokana na utata pindi wanapokuwa uwanjani.

Mechi ya Ufaransa dhidi ya Hispania yafanyiwa majaribio ya teknolojia hiyo

Kama ulipata nafasi ya kushuhudia pambano la kukata na shoka kati ya Ufaransa dhidi ya Hispania, huenda ukahisi mwamuzi aliyechezesha pambano hilo alifanya makosa makubwa zaidi kutokana na mwamuzi kulikubali bao la utata la mshambuliaji, Antoine Griezmann.

Lakini baadaye akalikataa bao la winga wa kulia wa Hispania, Gerard Deulofeu, ambalo lilizusha maswali mengi kwa mashabiki waliojitokeza kushuhudia mchezo huo ulioisha kwa Ufaransa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Ingawa ilikuwa ni majonzi kwa Wahispaniola lakini ulikuwa mchezo wenye manufaa makubwa katika mchezo wa soka kwani ulikuwa wa kufanyiwa majaribio ya teknolojia mpya ya video ambayo itamsaidia mwamuzi kuondoa utata na kufanya maamuzi yaliyo sahihi.

Hii yote inafanywa na Infantino ili kuufanya mchezo wa soka uzidi kupunguza makosa kutoka Goal Line Technology iliyozinduliwa na mtangulizi wake.

Fainali za Urusi kuzindua teknolojia hii

Teknolojia hii ambayo ni mpya kabisa katika mchezo wa soka, itaanza rasmi kufanya kazi katika fainali zitakazofanyika nchini Urusi mwaka 2018 ambayo ni nchi pekee itakayoweka historia ya kuzindua huduma hii.

“Tunaamini kuwa fainali ijayo ya Kombe la Dunia itakayofanyika Urusi itakuwa ya kwanza kutumia huduma hii ambayo itasaidia kwa kiasi kupunguza makosa ya waamuzi,” anasema.

Infantino hivi sasa yupo katika ziara ya siku nne akizitembelea nchi za Urusi na Qatar ambazo zitakuwa wenyeji wa mashindano haya makubwa katika miaka ya 2018 na 2022.

Wakati Ulaya kukiwa na mabadiliko hayo Afrika bado giza

Wakati barani Ulaya wakizidi kuendelea katika teknolojia na kuufanya mchezo wa soka kuwa wenye thamani hali ni tofauti kabisa na barani Afrika ambapo mambo yanaendelea kama zamani huku waamuzi wakitupiwa lawama kila kukicha kwa kushindwa kwenda sawa na kasi ya mchezo wa soka.

Afrika ni kati ya mabara yanayoongoza kwa lawama juu ya waamuzi kutokana na uduni wa nyezo zao ambazo zimekuwa zikifanya waonekane ni wala rushwa.

Awali, Ulaya walikuwa wakitumia teknolojia ya Goal line ambayo imeonekana kushindwa kutibu tatizo la kuondoa utata hivyo kuamua kuongeza chombo kingine ambacho kitakuwa kikimpa msaidizi mwamuzi ili aweze kutoa maamuzi yasiyo na utata.

Teknolojia ya Goal ilibuniwa mara baada ya kutokea kwa utata katika fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010 mara baada ya goli la kiungo Mwingereza, Frank Lampard fainali zilizofanyika nchini Afrika Kusini.

Mfumo huu ukaanza kutumika rasmi katika fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika mwaka 2014 nchini Brazil ambayo ndio nchi iliyopata nafasi ya kuizindua teknolojia hiyo.

Ameongeza timu za Afrika kutoka tano hadi tisa

Licha ya ukubwa wa bara la Afrika lakini ushiriki wake ulikuwa finyu zaidi, bara lenye wajumbe 54 wanaopiga kura za kumchagua Rais wa Fifa kuwakilishwa na timu tano halikuwa jambo zuri.

Infantino ameliona hili kutokana na kulithamini bara la Afrika tayari kiongozi huyo ameamua kuongeza nchi kutoka tano hadi saba ili kuipa fursa na Afrika kufanya vizuri katika mashindano hayo makubwa duniani.

Teknolojia ya goal au video ni ipi itatibu tatizo hili?

Ndani ya vipindi viwili vya utawala wa  Fifa, tumeshuhudia teknolojia mbili ambazo zote zinatumia gharama kubwa katika uendeshaji wake, je, ni nani atafaulu katika hili la kuwaondolea lawama waamuzi ni Infantino au Blatter?

Tayari tumeishuhudia teknolojia ya Goal line ambayo imekuwa ikitupiwa lawama kila kukicha kuwa muda mwingine huwa haitendi haki, ni zamu ya Infantino kuutafuna mfupa huu uliomshinda mtangulizi wake.

Ni jambo la kusubiri na kuona kama ataweza kufanikisha jambo hilo ambalo huenda likawa mkombozi kwa waamuzi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles