22.9 C
Dar es Salaam
Sunday, June 23, 2024

Contact us: [email protected]

Ghasia: Nipo tayari kuwajibika

Hawa Ghasia
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Hawa Ghasia

NA SHABANI MATUTU, DAR ES SALAAM,
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Hawa Ghasia, amesema kwamba yuko tayari kuwajibika iwapo atabainika amevuruga Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika juzi nchini.
Waziri Ghasia aliyasema hayo wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, kuhusu taarifa ya awali ya upigaji kura katika Serikali za Mitaa.
“Nitakuwa tayari kuwajibika kama nitapatikana na kosa la kuwa sehemu ya kuvuruga uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
“Kushindwa kusimamia vizuri uchaguzi na kusababisha kasoro ni moja ya makosa makubwa na kwa wale watakaobainika kuhusika watachukuliwa hatua kali kulingana na uzito na kiwango cha uhusika wao. Hatua hizo ni pamoja na kufukuzwa kazi, kuvuliwa madaraka, kushushwa cheo ikiwamo wengine kukatwa mishahara,” alisema Waziri.
Alisema kuwa Serikali itawachukulia hatua kwa sababu Tamisemi ilikuwa imekamilisha vifaa vyote vilivyokuwa vikihitajika katika uchaguzi huo.
“Tamisemi tulitoa vifaa vinavyotosheleza kwa ajili ya uchaguzi huo hivyo sasa inashangaza kusikia kuna mahali vifaa havikuwepo na kusababisha kutofanyika uchaguzi,” alisema.
Alisema hatua wanazotarajia kuchukua kufanikisha kuwapata wahusika ni pamoja na wizara kutoa agizo la kuitaka mikoa kuwasilisha taarifa kamili kuhusu kilichojitokeza katika halmashauri hizo ili zichambuliwe na wizara kwa ajili ya kuwabaini ili wachukuliwe hatua stahiki.
Waziri Ghasia alitaja idadi ya mikoa iliyofanya uchaguzi bila ya kutokea kasoro kuwa ni 145 kati ya 162 zilizofanya uchaguzi, wakati halmashauri tatu zikiwa hazikufanya uchaguzi kutokana na kucheleweshwa kwa vifaa.
Alisema kuwa halmashauri 14 zilizokumbwa na kasoro na kusababisha kutofanyika kwa uchaguzi huo zinatarajiwa kufanya uchaguzi wake ndani ya siku saba.
Waziri Ghasia alisema kuwa ili kuondoa vurugu zilizojitokeza katika uchaguzi wa juzi, Serikali imejipanga kuitumia Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kusimamia uchaguzi wa mwaka 2019.
“Tulipanga kuwaachia NEC kusimamia uchaguzi wa mwaka huu lakini baada ya kuzungumza nao walisema hawataweza kutokana na kukwepa kuelemewa na gharama kubwa.
“NEC walitueleza kwamba kuna uwezekano mkubwa wa kushiriki katika kusimamia uchaguzi ujao wa 2019 kuliko sasa ambako wamelemewa na kazi ya kushughulikia uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura,” alisema Waziri Ghasia.
Akizungumzia mafanikio katika uchaguzi huo, Waziri Ghasia alisema wamefanikiwa kwa asilimia 98.
“Kwa kiasi kikubwa uchaguzi umekuwa na maboresho makubwa ukilinganisha na ule wa mwaka 2009 ambao ulitumia karatasi nyeupe ambayo mpiga kura alitakiwa kuandika majina ya wagombea anaowataka kuwachagua,” alisema Waziri Ghasia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles