26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

GGML yang’ara tuzo za ATE, Majaliwa aahidi makubwa

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

JITIHADA za Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) kuwajengea uwezo wahitimu wa vyuo vikuu kwa kuwapatia mafunzo kazini zimeendelea kuonekana baada ya kampuni hiyo kuibuka mshindi wa pili katika tuzo zilizoandaliwa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET).

GGML ilibeba tuzo katika kundi la waajiri wakubwa kutokana na mchango wake wa uzalishaji wa rasilimaliwatu wenye ubora kwa soko la ajira.

Hatua hiyo inakuja siku chache baada ya kampuni hiyo kupokea wahitimu 50 kutoka vyuo vikuu mbalimbali nchini ambao wameanza kupatiwa mafunzo kazini mwaka huu. Kati yao 30 ni wanawake na 20 wanaume. Mwaka jana jumla ya vijana 26 walihitimu mafunzi hayo ndani ya GGML.

Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, katika hafla iliyofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, Meneja Mwandamizi (Rasilimaliwatu) kutoka GGML, Charles Masubi aliishukuru Serikali kwa kutambua mchango wa kampuni hiyo katika uzalishaji wa vijana bora wanaokubalika katika soko la ajira.

 Awali, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, alisema Serikali itaendelea kushirikiana kikamilifu na sekta binafsi katika utoaji elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi ili kuzalisha wataalamu wenye ujuzi wa kutosha unaohitajika katika sekta mbalimbali.

Pia aliwapongeza waajiri kwa kutoa nafasi za mafunzo kwa vitendo, uanagenzi, utarajali pamoja na namna wanavyoshiriki katika kuandaa mitaala inayotumika kwenye vyuo na taasisi za elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi.

Alitoa wito kwa waajiri wote nchini kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha malengo ya kukuza ujuzi na kuongeza soko la ajira yanafanikiwa kwa mustakabali wa maendeleo ya Taifa.

“Maendeleo ya uchumi wa nchi yoyote yanategemea sana ngazi ya ujuzi wa nguvukazi uliyokuwa nayo. Hivyo, mchango wa wadau ni muhimu,” alisema.

Alisema ushirikiano huo ni muhimu katika kuendeleza ujuzi kwa ajili ya kujenga uchumi wa viwanda. “Nataka nitumie fursa hii kuwapongeza lakini Serikali inatambua na inathamini juhudi mnazozifanya katika utoaji wa ajira kwa wahitimu wetu, tunawapongeza sana.”

Akizungumzia kuhusu kauli mbiu ya mwaka huu inayosema “Kuimarisha Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi kwa Uzalishaji wa Wafanyakazi Wenye Ujuzi Nchini Tanzania”, Waziri Mkuu alisema kauli hiyo ni thabiti kwani inaweka msisitizo katika ujenzi wa rasilimali watu yenye ujuzi.

Naye, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda alisema Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa Makakati wa Taifa wa Uendelezaji wa Ujuzi wa Mwaka 2016/17-2025/26 ambao moja ya malengo yake ni kuwa na ushirikiano kati ya waajiri, wadau na vyuo au taasisi za elimu.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Suzanne Ndomba-Doran alisema ili Tanzania iweze kushiriki kikamilifu katika soko shindani la Afrika Mashariki na dunia ni lazima hatua za makusudi zichukuliwe katika kukuza ujuzi hususani kwa vijana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles