24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

GGML yaja na teknolojia za kisasa maonesha ya OSHA, wananchi wavutiwa mifumo ya usalama

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

KATIKA kuadhimisha siku ya usalama na afya mahala pa kazi duniani – 2023 ambayo kitaifa yanafanyika mkoani Morogoro, Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) imekuja na teknolojia mpya za kisasa katika kudumisha usalama na afya mahala pa kazi hali ambayo imekuwa kivutio kwa wananchi wanaotembelea banda la kampuni hiyo kwenye uwanja wa Tumbaku.

Teknolojia hizo ambazo ni mahsusi kwa afya na usalama wa wafanyakazi wanaofanya kazi migodini, zimetajwa kuwa za kipekee kutokana na ubunifu wa uhakika uliotekelezwa na kampuni hiyo kuleta mageuzi kwenye sekta ya uchimbaji madini.

Akifafanua kuhusu bunifu hizo mjini Morogoro katika banda la maonesho GGML, Afisa Mwandamizi wa Usalama na afya  mahali pa kazi, Sospeter Mkombati amesema licha ya kwamba kampuni hiyo ni mdau namba moja wa maonesha hayo, mwaka huu imeamua kuja na vitu tofauti.

Amesema GGML kwa miaka mingi iliyoshiriki maonesha hayo yanayoratibiwa na Wakala wa Afya na Usalama Mahali pa kazi (OSHA), ililenga kuelimisha umma kuhusu masuala ya usalama mahala pa kazi, lakini safari hii inataka kuwafundisha ili wananchi wanaotembelea banda hilo wakalete mageuzi kwenye kampuni zao.

Amesema teknolojia hizo ambazo GGML imekuja nazo katika maonesho ya mwaka huu ambayo kauli mbiu yake inasema “Mazingira salama na afya ni kanuni na haki ya msingi mahali pa kazi”, zinathibitisha kipaumbele cha kwanza cha kampuni hiyo ambacho ni usalama na afya mahali pa kazi.

Mkombati ametaja teknolojia ya kwanza kuwa ‘Refugee chamber’ ambayo ni chumba maalumu cha dharura ambacho huwekwa ndani ya mgodi chini ya ardhi ili kuwawezesha wafanyakazi waliopo ndani ya mgodi kwenda kukusanyika hapo wakati wakisubiri uokozi mwingine kutoka juu.

“Refugee chamber ni kifaa ambacho hutumia underground kwa kumsaidia mfanyakazi pale kunapotokea ajali mbalimbali labda mwamba umeshuka au ajali ya moto, mfanyakazi badala ya kuhaha namna ya kutoka anakwenda kwenye chumba hicho chenye uwezo wa kuchukua zaidi ya watu 20 huku kikiwa kimesheheni vifaa mbalimbali vya uokozi kama vile mitungi ya hewa ya oksijeni pamoja na mitambo ya kutoa taarifa.

“Kwa hiyo waliopo nje watajua waandae uokoaji wa aina gani kuelekea kwenye chumba hicho ambacho hakiwezi kupenya moto wala mawe ya miamba huko chini ya ardhi,” amesema.

Ameitaja teknolojia nyingine waliokuja nayo kuwa ni ya mifumo ya kudhibiti ajali za moto kwenye magari ambapo sasa magari yote ya kampuni hiyo ikiwamo mitambo, imefungwa mifumo hiyo kwenye injini.

Amesema mifumo hiyo inauwezo wa kutoa maji maalumu kuzima moto wowote unaoweza kutokea ndani ya injini ya gari au mtambo bila dereva kuamuru au kushuka kwenye gari kutafuta kizima moto.

Mkombati ameongeza kuwa teknolojia ya tatu ambayo GGML imekuja nayo kwenye maonesho hayo, ni  matumizi ya ndege zisizo na rubani (drone) katika kupiga picha na video ndani ya mgodi ili kutambua usalama wa miamba kabla ya mfanyakazi kwenda kuchimba.

“Wafanyakazi walikuwa wanakwenda kuchimba, muda mwingine ndani ya miamba  wanakuta mawe hayajakaa vizuri na kuleta wasiwasi kuhusu uthabiti wa miamba hiyo lakini sasa tumekuja na teknolojia ya drone ambayo huenda ndani kuchukua picha kisha tunaangalia wapi pako salama na sio salama ili kuhakikisha mazingira salama kwa wafanyakazi wetu,” amesema.

Teknolojia nyingine ameitaja kuwa ni ngazi maalumu ya uokozi ambayo inatumika kwenye njia ya dharura wakati wa kujiokoa kutoka ndani ya mgodi mbali na njia kuu ya kuingia na kutoka mgodini.

“Ukiacha chumba cha dharura “refugee chamber”, GGML imebuni njia ya dharura au escape way ambayo ina ngazi za kisasa zinazomuwezesha mfanyakazi anayejiokoa kutoka mgodini kupanda ngazi hizo bila kuteleza lakini pia kila baada ya mita sita anaweza kupumzika maana muda mwingine kunaweza kuwa na umbali wa mita 150 kutoka ndani ya mgodi kuja nje.

“Teknolojia hii inatumia kitu kama drum za plastic ambapo ndani kuna ngazi zisizoteleza na sehemu za kupumzika (platform) hivyo ni teknolojia mpya ambayo makampuni ya sekta hii ya madini yanaweza kuiga na kuitumia,” amesema.

Ofisa huyo mwandamizi wa usalama, pia ameongeza kuwa GGML sasa imekuja na choo maalumu ambacho kimebuniwa kwa ajili ya kuwasitiri wafanyakazi wanaochimba madini ndani ya mgodi.

Amesema choo hicho kinawawezesha wafanyakazi kujisitiri humohumo ndani ya mgodi bila kutoka nje ya mgodi kwenda kujisaidia haja kubwa au ndogo.

“Vyoo hivi vinapelekwa ndani ya mgodi ambapo mfanyakazi anatembea mita chache na kujisitiri. Ni vyoo vya kisasa, vina dawa za kuua wadudu na vikikaribia kujaa vinachukuliwa na mashine kupelekwa nje ya mgodi kusafishwa,” anasema.

Ameongeza kuwa wananchi waliotembelea banda hilo wameeleza kuvutiwa na vifaa hivyo vya ubunifu hali inayozidi kuwaongezea ari wafanyakazi wa kampuni hiyo kuzidi kuzingatia masuala ya usalama na afya mahali pa kazi na kufanya kazi kwa bidi.

Mmoja wa wananchi waliotembelea banda la GGML, Novatus Chuwa amesema amejifunza vitu vingi ambavyo ni vigeni, lakini sasa vinamvuti kuchagua kufanya kazi migodini kwa sababu ya uhakika wa usalama mahali pa kazi.

Naye Alice Kyando amesema uwingi wa watu wanaokimbilia kwenye banda la GGML umethibitisha kuwa namna gani kampuni hiyo imejipanga kuhakikisha mazingira ya kazi yanaandaliwa vema na kumfanya mfanyakazi anafanya kazi mahali salama na kwa kufuata miongozo ya kimataifa usalama na afya mahala pa kazi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles