23.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

GGML yaanza kutekeleza mpango wa uchimbaji mwaka 2021

Na Mwandishi wetu, Geita

Kampuni ya uchimbaji dhahabu mkoani Geita (GGML) imeanza kuchimbaji wa wazi na wa chini kwa chini katika mgodi wa Nyamulilima ikiwa ni siku chache baada ya Serikali kuidhinisha mpango huo kwa mwaka 2021.

Hatua imekuja baada ya GGML kupokea ruhusa ya mpango wa uchimbaji madini kutoka kwa Mkaguzi Mkuu wa Migodi yote nchini, Dk. Abdul Rahman Mwanga.

Afisa Uendeshaji Mkuu wa AngloGold Ashanti –Afrika, Sicelo Ntuli akizungumza na waandishi wa habari katika hafla ya uzinduzi wa uchimbaji huo mpya katika mgodi wa Nyamulilima. Kulia kwake ni Makamu wa Rais – Miradi Endelevu wa GGML, Simon Shayo.

Dk. Mwanga aliruhusu mpango huo mwishoni mwa wiki baada ya GGML kupeleka nyaraka zote Tume ya Madini na kupatiwa vibali.

Kufuatia ruhusa hiyo, GGML sasa imeanza kufanya shughuli zake za uchimbaji kama zinavyoainishwa kwenye kijitabu kilichokamilika na kutiwa saini na Mkaguzi Mkuu wa migodi yote nchini. GGML inapaswa pia kuendesha shughuli zake kwa kuzingatia masharti na miongozo ya sheria za nchi ya Tanzania.

Vile vile, Kampuni itaweka taarifa mpya kila mwaka katika mpango wa uchimbaji uliothibitishwa na kwa kuzingatia mabadiliko makubwa katika shughuli za uchimbaji.

Akizungumzia ruhusa hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa GGML Bw. Richard Jordinson ameipongeza serikali kwa kuendeleza ushirikiano wa miaka mingi na kufafanua kuwa GGML sasa itapata fursa ya kupanua wigo zaidi wa uzalishaji na kutimiza matarajio ya wadau wake.

“Kupata kibali cha mpango huu wa uchimbaji ni ushahidi wa rekodi yetu nzuri ya uchimbaji madini nchini. Hii inaonyesha pia imani iliyonayo Serikali kwa kampuni yetu kama mdau wa maendeleo,” alisema Jordinson.

Miradi inayotajwa katika mpango wa uchimbaji wa GGML ni pamoja na Mradi wa Nyamulilima utakaohusisha maeneo ya kituo cha nane (8), Star and Comet, Xanadu, Selous, Mabe pamoja na Roberts. Uchimbaji wa wazi katika eneo la Nyamulilima unatarajiwa kuongeza uzalishaji dhahabu katika mgodi wa GGML ambapo uchimbaji unaweza kuendelea hadi mwaka 2027.

“Ruhusa ya kuanza shughuli za uchimbaji katika eneo la Nyamulilima ni habari njema kwa wadau wetu, wafanyakazi na wakandarasi. Inatoa pia fursa nyingi kwa jamii inayotuzunguka kufaidika kutokana na shughuli za AngloGold Ashanti. Tunatarajia kuendelea kufanya uwekezaji kwenye jamii inayotuzunguka kwa kuwa hiyo ni mojawapo ya tunu zetu,” aliongeza Jordinson.

Naye Kaimu Meneja Mkuu wa GGML, Wayne Louw alisema uzinduzi huo wa uchimbaji katika mgodi wa Nyamulilima umetimiza ahadi ya kampuni hiyo kwa wadau wake wakiwamo wafanyakazi na wakandari.

“Pia uchimbaji huu ni faida ya kipekee kwa mkoa wa Geita na jamii inayozunguka mgodi. Kulingana na miongozo ya uchimbaji wa madini ya Kampuni mama ya AngloGold Ashanti ianze shughuli zake hapa nchini, itaendelea kuwekeza kwa jamii inayotuzunguka,” alisem Wayne Louw.

Hivi karibuni GGML iliibuka mshindi wa jumla wa kampuni zinazofanya vizuri kwenye sekta ya madini nchini Tanzania kwa mwaka 2019/2020. GGML iliibuka mshindi  katika vipengele vya Wajibu wa Kampuni kwa Jamii (CSR), Utunzaji mazingira na usalama, ukusanyaji wa mapato ya Serikali (kodi) pamoja na uwezeshaji wa wazawa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles