*….aipongeza GGML kuajiri asilimia 98 Watanzania mgodini
Na Mwandishi Wetu, Geita
MKUU wa wilaya ya Nyang’wale, Jamhuri William amesema uongozi wa Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGM) umewatoa kimasomaso Serikali ya mkoa wa Geita katika ufadhili wa maonesho ya teknolojia ya madini tangu yalipoanzishwa miaka mitano iliyopita.
Pia ameipongeza kampuni hiyo kwa kutoa fursa za ajira kwa Watanzania zaidi ya asilimia 98 ya waajiriwa wote wa kampuni hiyo iliyoanza shughuli za uchimbaji wake rasmi hapa nchini mwaka 2000.
Mkuu huyo wa wilaya ametoa pongezi hizo jana mjini Geita alipotembelea mabanda yaliyopo katika Maonesho ya Tano ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini Geita na kufanya majumuisho katika banda ya GGML kwenye viwanja vya Bombambili mkoani Geita.
Alisema katika kipindi cha miaka mitano GGML wameshiriki maonesho hayo lakini pia wamekuwa wadhamini wakuu na kufanya kazi kubwa ya kuboresha maonesho hayo.
“Niwapongeze na kuushukuru uongozi wa GGML kwa kazi kubwa wanayoifanya katika mkoa wetu wa Geita…kwa kweli wametutoa kimasomaso na tunaendelea kuwashukuru na kuwasihi tuendelee hivyo hivyo,” alisema.
Alisema kipindi fulani wakati madini haya yakiwa chini ya ardhi, Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Nyerere alisema kwamba hatachimba madini haya mpaka Watanzania wawe na uwezo na teknolojia sahihi ya kuyachimba ili yaweze kunufaisha wananchi.
“Tumeona wafanyakazi wengi wa GGML ni Watanzania wenzetu, tena ni mahiri kabisa katika kusimamia hii sekta ya madini kwani katika kila sekta wapo Watanzania wanasimamia, hivyo ni muhimu wananchi kushiriki katika tasnia hii ya madini,’ alisema.
Alisema maonesho ya mwaka huu ni mazuri kwa sababu yamejumuisha wadau wengi zaidi ya 600 kutoka makampuni mbalimbali ya madini na wadau wake.
“Niwashukuru wadau wote ambao wamejitokeza kuleta bidhaa kwa ajili ya maonesho haya. Nitoe wito kwa wananchi wa Geita na mikoa jirani kujitokeza kwa wingi kuja kuona teknolojia mbalimbali za madini na uzalishaji mali ambazo zitasaidia kuboresha maisha yao.
“Pia nimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kutoa fursa kwa mkoa wa Geita kuonesha dunia nini ambacho tunaweza kufanya, tumejaliwa bidhaa za kilimo, madini na shughuli mbalimbali za kiuchumi, ni muda muafaka kwa watanzania kutoka sehemu mbalimbali kuja kuwekeza katika mkoa wa Geita kwani fursa zipo,” alisema.
Awali Meneja Mawasiliano wa Kampuni ya GGML, Stephen Mhando mbali na kumkaribisha Mkuu huyo wa wilaya katika banda hilo kuu la GGML, pia alimueleza kwamba kampuni hiyo imetekeleza kwa vitendo maboresho ya sheria ya madini ambayo inatoa nafasi kwa wazawa kushiriki mnyororo wa shughuli za uchimbaji wa madini.
Alitolea mfano baadhi ya kampuni hizo kuwa ni pamoja na African Underground Mining Services (AUMS), ambayo inahusika na kutoa huduma za uchimbaji na uendeshaji wa migodi hasa chini ya ardhi (underground), kwa GGML.
Vilevile Kampuni ya Blue Coast Investment Limited ambayo ni mmoja wa wakandarasi watoa huduma wa kampuni ya GGML.