27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, February 8, 2023

Contact us: [email protected]

GGML mdhamini mkuu maonyesho ya teknolojia za uchimbaji madini Geita

 MWANDISHI WETU

GEITA Gold Mining Limited (GGML), ndiye mdhamini mkuu wa maonyesho ya tatu ya teknolojia za uchimbaji madini mkoani Geita, yaliyoanza jana na kutarajia kuhitimishwa Septemba 27. GGML imetoa udhamini wa Sh milioni 200, unaohusisha gharama za kusawazisha eneo la maonyesho, kugharamia mabanda 100 pamoja na umeme wa dharura katika kipindi chote cha maonyesho hayo.

Maonyesho hayo yanafanyika katika viwanja vya Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji na Mauzo Nje ya Nchi (EPZA) Mjini Geita.

“GGML inajivunia kudhamini maonyesho haya kwa mwaka wa tatu mfululizo. Mwaka huu tunakusudia kutoa uzoefu wetu wa matumizi ya vifaa mbalimbali vya uchimbaji kwa makampuni mengine lakini pia kwa wachimbaji wadogo. 

“Ni jambo zuri pia kwamba tumetoa udhamini huu tukiwa tunaadhimisha miaka 20 ya uwekezaji wetu mkoani Geita na Tanzania. 

“Tunajivunia kuendeleza ushirikiano na jamii inayotuzunguka kunufaisha wafanyabiashara wa ndani wanaokusudia kufanya kazi na sisi,” alisema Simon Shayo, Makamu wa Rais wa GGML anayeshughulikia miradi endelevu.

Alisema wanafarijika sana kuona ndoto ya kuwa na kituo cha uwekezaji na biashara ya nje hapa Geita inatimia na GGML inakuwa sehemu ya mafanikio hayo kupitia mpango wake wa kusaidia jamii.

Alisema pamoja na tunu yake kuu ya kuisaidia jamii ya Geita kuwa na maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi ambayo yatabakia hata baada ya shughuli za uchimbaji kumalizika, GGML pia imetekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika Mkoa wa Geita ikiwemo uwekezaji wa EPZA mjini Geita uliotumia bajeti ya Sh milioni 800.

Maonyesho haya yatakutanisha kampuni za uchimbaji madini, wachimbaji wadogo na wa kati, wawekezaji na wafanyabiashara kutoka Tanzania na nchi nyingine kwa ajili ya kuonyesha teknolojia zinazotumika katika sekta ya uchimbaji madini na fursa za uwekezaji na biashara kwenye sekta hiyo.

Mwaka 2019, Kamati ya Maandalizi ya Maonyesho ya Teknolojia za Uchimbaji Madini, iliitunukia GGML tuzo ya mshindi wa kwanza aliyetoa elimu na mafunzo ya teknolojia muhimu kwa wachimbaji wadogo sanjari na mifumo ya usalama na uokoaji inayopaswa kutumika migodini. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,871FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles