23.6 C
Dar es Salaam
Friday, June 21, 2024

Contact us: [email protected]

GGML inavyotumia teknolojia kuigeuza Geita kuwa ya kijani

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

SHUGHULI za uchimbaji madini hutakiwa kwenda sambamba na urejeshaji mazingira ambayo kwa namna moja au nyingine yanaweza kuharibiwa na shughuli hizo ndio maana kumekuwa na ufuatiliaji mkubwa kwa upande wa Serikali na mamlaka husika kuhakikisha mazingira yanalindwa.

Vivyo hivyo katika kulinda vyanzo vya maji hasa ikizingatiwa yanatumiwa na viumbe hai wote ikiwamo binadamu na wanyama.

Kama ilivyo ada kwa upande wa Serikali ya Tanzania, imeendelea kushajihisha uhifadhi endelevu wa mazingira na vyanzo vya maji kama ilivyo kwa kauli mbiu ya maadhimisho ya Mazingira duniani mwaka huu inayosema “Urejeshwaji wa Ardhi, Ustahimilivu wa hali ya Jangwa na ukame’’.

Wakati Tanzania ikiadhimisha siku hiyo Juni 5, mwaka huu, mkoa wa Geita umeendelea kuwa mfano wa kuigwa kwa kutunza mazingira licha ya kuwa ni moja ya mkoa unaoongoza kwa uzalishaji wa dhahabu nchini.

Ni kwa kupitia kampuni Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) ambayo ni kampuni tanzu ya AngloGold Ashanti, mkoa huo umefanikiwa kupiga hatua katika sekta ya madini.

Pamoja na kwamba GGML inaongoza kwa uzalishaji wa dhahabu, pia inasifika kwa kujitolea kwake kuwekeza nguvu na jitihada katika uhifadhi wa mazingira uili yawe endelevu kwa vizazi vijavyo.

Kampuni hii kubwa ya uchimbaji madini nchini imetambuliwa kwa kuwa ‘championi’ wa uhifadhiwa mazingira kwa sababu malengo yake yanawiana yale ya Siku ya Mazingira Duniani.

Ndio maana Meneja Mwandamizi wa Afya, Usalama na Mazingira wa GGML Dk. Kiva Mvungi anasisitiza dhamira ya GGML kuendelea kubadilisha mandhari ya mji wa Geita kuwa wa kijani.

“Kabla ya kupata leseni yetu ya uchimbaji madini, tulipaswa kuzingatia kanuni zote na kuandaa sera zinazolenga kulinda na kuhifadhi mazingira. Kila mwaka GGML pamoja na wadau wengine wakuu hutenga bajeti kwa ajili ya miradi ya uwajibikaji kwa jamii (CSR) ambayo tunahakikisha sehemu ya bajeti hiyo inaelekezwa katika jitolea kwa ajili ya mipango ya mazingira,” anasema

Akitoa mifano katika mpango wa urejeshaji wa mazingira, Dk. Kiva anasema wa kutambua athari za uchimbaji madini kwenye ardhi, GGML imetekeleza mpango kabambe wa ukarabati wa ardhi.

“Mpango huu unahusisha juhudi za kuendeleza uhifadhi wakati wa uchimbaji madini, kwa kuzingatia upandaji miti na uboreshaji wa udongo ambapo kwa ushirikiano na jamii wenyeji, GGML imepanda takriban miti 473,000 hali iliyokukuza baionowai na kupunguza uharibifu wa ardhi.

Katika usimamizi wa maji, GGML inatekeleza mkakati madhubuti wa usimamizi wa maji na kuboresha matumizi ya maji katika shughuli zao zote.

Dk. Kiva anasema mojawapo ya miradi mikubwa zaidi ya GGML ni mpango wa urekebishaji wa maji wa In Situ, ambao hutumia bakteria zinazotokea kiasili kurekebisha salfa katika maji ya ardhini.

“Mbinu hii bunifu husaidia kudumisha ubora wa maji chini ya ardhi, ambayo ni muhimu kwa mfumo wa ikolojia na jamii inayozunguka mgodi.

“Operesheni za GGML zinahitaji matumizi makubwa cha mashine na vifaa vizito. Ikumbukwe kwamba mashine hizi mara nyingi hutumia mafuta, ambayo yanaweza kuchanganyika na maji wakati wa mchakato wa uchimbaji madini. Kwa upande wa GGML hutumia kifaa maalumu kinachotenganisha maji na mafuta (Drizit Oil Water Separator) ambacho kinasaidia pia kuondoa taka kwenye maji na kulinda afya ya wanyamapori na jamii zinazozunguka mgodi huo.

“Ushirikiano wa kijamii: ni eneo lingine ambalo GGML inajihusisha kikamilifu ili kutekeleza mpango wa uwajibukaji wa pamoja katika uhifadhi wa mazingira.. Programu za elimu zinazotolewa na kampuyni hiyo zimeendelea kuwa shirikishi kwa lengo kuwezesha wakazi kuwa wasimamizi endelevu wa mazingira yao,” anasema.

Anasema mpango wa GGML wa ukarabati wa ardhi umerejsha makazi asili ya wanyamapori, umezuia mmomonyoko wa udongo na kuchangia kuboresha ubora wa hewa na upatikanaji wa maji. Juhudi hizi zimetambuliwa na Wizara ya Madini na kuitaja GGML kama kampuni inayoongoza na ya kuigwa katik uchimbaji madini endelevu kutokana na utunzaji wa mazingira.

Aidha, kutokana na ubunifu wa GGML katika kulinda mazingira, umetambuliwa hata na kampuni nyingine zinazohusika na masuala ya uchimbaji madini kupitia machapisho mbalimbali yanayoongoza katika tasnia hiyo. Kutokana na uhifadhi endelevu GGML wametunukiwa kuwa kampuni bora kwa inayozingatia ulinzi wa mazingira, afya na usalama kazini katika Kongamano la Madini na Uwekezaji Tanzania mwaka 2023.

Ustawi wa wafanyakazi ni kipengele kingine ambacho GGML imeendelea kuwa mfano wa kuigwa kwani katika operesheni zinazofanywa na kampuni hiyo, matukio ya majeraha na ajali mahali pa kazi yamepungua.

Maendeleo ya jamii ni kipengele kingine ambacho GGML kupitia mipango endelevu imeboresha maisha ya wengi katika jamii ya Geita. Juhudi za kampuni hiyo pia zimeonekana katika maeneo mbalimbali kama vile elimu, afya, na maendeleo ya miundombinu.

Wadau wa sekta ya madini akiwemo Makamu Rais wa AngloGold Ashanti – GGML anayeshughulikia miradi endelevu na masuala ya ubia na ushirika Afrika, Simon Shayo anasema kadiri mahitaji ya madini yanavyoendelea kukua, mbinu endelevu za uchimbaji madini zitazidi kuhitajika hivyo, kampuni zinazofuata mwongozo wa GGML sio tu zitachangia ulinzi wa mazingira lakini pia zitajihakikisha faida ya muda mrefu na kuimarisha mpango wa uwajibikaji wa kijamii.

Kiujumla mtazamo wa GGML wa ulinzi wa mazingira, pamoja na dhamira yake katika ushirikishwaji wa jamii, unaonyesha kwamba uwajibikaji wa kampuni wakati wa utekelezaji wa shughuli zake uchimbaji madini sio tu unawezekana bali ni muhimu kwa mustakabali endelevu.

Shayo anasema urithi wa GGML unaenea zaidi ya uzalishaji wake wa dhahabu.

“Tumeanzisha mipango mipya cha utunzaji wa mazingira, na kuwatia moyo wengine kutambua kuwa ustawi wa kiuchumi na ustawi wa mazingira huenda pamoja. Katika maadhimisho ya ya Mazingira Duniani, GGML huitumia siku hiyo kama ukumbusho kwamba hata ndani ya tasnia zinazotumia rasilimali nyingi, uvumbuzi na ari vinaweza kutengeneza njia ya kesho iliyo angavu na endelevu zaidi,” anasema Shayo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles