GGM KUKARABATI GEREZA KWA MIL 69/-

0
544
Meja Jenerali Mstaafu, Ezekiel Kyunga

Na HARRIETH MANDARI-GEITA


MGODI wa Dhahabu wa Geita (GGM), umetoa msaada wa vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya Sh milioni 69.8 kukarabati miundombinu ya mfumo wa majitaka katika Gereza la Mkoa wa Geita lililojengwa mwaka 1947.

Akizungumza baada ya makabidhiano ya vifaa hivyo vya ujenzi, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Meja Jenerali Mstaafu, Ezekiel Kyunga, alisema msaada huo utasaidia kuboresha gereza hilo kutokana na uchakavu wa miundombinu  ya mfumo wa maji taka ambao umetokana na ongezeko kubwa la wafungwa na mahabusu.

Alisema gereza hilo lilijengwa mwaka 1947, lina uwezo wa kuhudumia wafungwa na mahabusu 191 lakini linakabiliwa na changamoto ya wingi wa mahabusu zaidi ya 600.

“Gereza hili lilianzishwa kwa ajili ya kuhifadhi mahabusu na wafungwa 45 mwaka 1947, baada ya maboresho kidogo lilibadilishwa na kuhudumia wafungwa 191, lakini bado mahabusu na wafungwa wamekuwa wengi zaidi ya uwezo wake, hivyo kuharibika kwa mfumo wake wa maji taka kila mara na kusababisha kuwepo kwa adha kubwa na kuhatarisha afya za mahabusu na wafungwa,” alisema Kyunga.

Aidha, Mkuu huyo wa mkoa alisema kuna ongezeko kubwa la wakazi katika Mkoa wa Geita unaotokana na shughuli za uchimbaji madini na biashara, hivyo Serikali ya mkoa ina mpango wa kujenga gereza jingine kubwa katika eneo la ekari 500 ambalo litahimili wafungwa wengi zaidi.

Akikabidhi msaada huo, Mkurugenzi wa GGM, Richard Jordinson, alisema msaada huo ni mojawapo ya mchango wake katika kusaidia maendeleo ya jamii zinazozunguka mgodi huo, huku akiahidi kutoa pia msaada mwingine wa wataalamu na mashine za ujenzi.

“Mgodi wetu unayo furaha kutoa mchango huu kwa jamii, ni moja ya malengo na mikakati ambayo tumejiwekea kila mwaka kama sehemu ya kusaidia Serikali katika kuhakikisha kunakuwa na ustawi katika jamii,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here