27.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Gesi asilia inavyosaidia kuleta mageuzi kiuchumi

Faraja Masinde

NISHATI ya gesi asilia ni kati ya vitu ambavyo Tanzania imejaaliwa kuipata ikilinganishwa na mataifa mengine ya jirani na Afrika kwa ujumla.

Jambo la kufurahisha zaidi ni kwamba kadri muda unavyozidi kwenda, ndivyo manufaa makubwa ya gesi hiyo yanavyozidi kuchukua mwelekeo mnyoofu, lengo ikiwa ni kuwanufaisha Watanzania.

Kumekuwapo na ongezeko la matumizi ya nishati hiyo katika maeneo mbalimbali ambayo moja kwa moja tunaweza kusema kuwa imekuwa na manufaa makubwa tofauti na matarajio ya huko nyuma ambapo ilidhaniwa kuwa huenda ingekuwa na manufaa kwa Watanzania wachache tu.

Hadi sasa, unaposoma makala haya fahamu kuwa gesi hiyo imeanza kutumika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam huku lengo likiwa ni kuvifikia vyuo na taasisi zote za umma ikiwamo majeshi kama alivyoelekeza Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Merdadi Kalemani, alipokuwa akizindua matumizi ya gesi asilia chuoni hapo mapema mwezi huu.

Aidha, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC), Dk. James Mataragio, anakiri kuwapo kwa ongezeko kubwa la matumizi ya gesi hiyo huku uzalishaji wake ukifiakia futi za ujazo milioni 200.

Pia imebainika kuwa viwanda vinavyotumia gesi asilia kuendesha shughuli zake vinapunguza gharama za uzalishaji kwa asilimia 40.

Historia ya gesi asilia nchini

Kama inavyofahamika kwamba TPDC imekuwapo muda mrefu lakini matumizi ya gesi nchini Tanzania yameanza mwaka 2004 ikitumika chini ya futi za ujazo milioni moja. Hata hivyo, kwasasa imefikia kwa siku matumizi ya gesi asilia futi za ujazo milioni 200 kiwango ambacho ni cha juu zaidi.

Ukirejea nyuma kidogo, mwaka 2010 zilifikia futi za ujazo milioni 40 lakini mwaka 2015 zilifikia futi za ujazo milioni 60 na sasa ni futi za ujazo milioni 200.

Kwa mujibu wa TPDC, kiwango hicho kinatafasriwa kwenye matumizi ikiwa ni pamoja na kuzalisha umeme, kusambaza gesi majumbani, viwandani na kwenye magari huku kiwango hicho kikitarajiwa kupaa zaidi kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya nishati hiyo, hatua inayotokana na kuongezeka kwa ufahamu miongoni mwa watumaiaji.

“Uzalishaji wa ueme kwa gesi asilia umeongezeka kutoka MW 553 mwaka 2015 hadi kufikia MW 892.7 mwaka 2019 sawa na ongezeko la asilimia 61.

“Lakini kama hiyo haitoshi, sasa hivi gesi asilia mchango wake kwenye umeme wa giridi ya taifa umefikia asilimia 57 hatua ambayo imechangia kuondoa tatizo la upungufu wa umeme wakati wa kiangazi, lakini pia viwanda 48 tayari vimeunganishwa kwenye mtandao wa gesi asilia katika mikoa ya Dar es Salaam , Pwani na Mtwara.

“Viwanda vitano kati ya hivyo vimeunganishwa katika bomba kuu la TPDC na ni matarajio yetu kuwa faida hii itaongezeka.

“Hii ni kutokana kwamba kwa kutumia nishati hiyo katika uendeshaji wa shughuli zake kiwanda kinaokoa asilimia 40 ya gharama,” anasema Dk. Mataragio.

Hata hivyo, hali haikuwa shwari kwenye upande wa matumizi ya gesi hiyo majumbani. Mwaka 2010 ilikuwa ni nyumba 20 ndio waliokuwa wakitumia huduma hiyo, lakini kiwango hicho kilipanda na kufikia wateja 73 waliounganishwa na huduma hiyo mwaka 2015.

Jambo la kuvutia ni kwamba hadi sasa idadi hiyo imeongezeka na kufikia nyumba 450 huku lengo likiwa ni kuunganisha nyumba 1,500 kupitia bajeti ya mwaka 2019/20.

Waziri Kalemani anasema mradi huo unatekelezwa kwa awamu, lengo likiwa ni kuona wakazi wote wa Jiji la Kibiashara la Dar es Salaam wakiunganishwa na huduma hiyo ili kuondoa uharibifu wa mazingira unaochochewa na matumizi ya mkaa.

“Takwimu za mwaka jana zinaonesha kuwa magunia ya mkaa yanayoingia Dar es Salaam ni zaidi ya 400,000 hadi 500,000 kila mwaka, huku upande wa vijijini mkaa na kuni zinazotumika kijijini ni zaidi ya asilimia 81.7.

“Lazima tuangalie uharibifu huu wa mazingira unaojitokeza na hakuna njia mbadala zaidi ya kutumia gesi asilia. Unapotumia gesi unaokoa zaidi ya asilimia 40 ya gharama yako ya kila siku, tafiti zinaonesha kuwa matumizi ya kila siku nyumbani ni Sh 4,000,” anasema Dk. Kalemani.

Lakini pia matumizi ya gesi asilia yanaelezwa kuongeza uwekaji wa mazingira safi.

Matumizi kwenye magari

Kwa mujibu wa TPDC, magari yanayotumia gesi asilia yameongezeka kwa kiasi kikubwa katika kipindi cha miaka minne ambapo hadi sasa idadi hiyo imefikia magari 305 kwa Jiji la Dar es Salaam huku mkakati wa shirika hilo ukiwa ni kujenga vituo vikubwa viwili vya CNG ikiwamo UDSM ili kuwezesha usambazaji gesi asilia katika mfumo wa CNG.

Lakini kuhusu hilo, Dk. Kalemani anawataka wanaoagiza magari kuanza kuzingatia yale yanayotumia mfumo wa gesi ili kuepusha usumbufu.

“Wanaoagiza magari kuanzia wizara yangu na taasisi zetu zote wanazingatie mfumo unaotumia gesi ili kupunguza gharama za uendeshaji.

“Kwa kuwa kuna manufaa makubwa, niziagize taasisis zote za umma, vyuo vikuu vyote kuanza kutumia gesi ili kupunguza matumizi yasiyo ya lazima. Serikali imejipa mpango wa kuhakikisha kuwa ndani ya mikaa minne ijayo zinakuwa zimeunganishwa na nishati hii.

“Tunayo gesi ya kutosha nchini, jumla ya gesi tuliyonayo ni futi za ujazo trilioni 57.54. Mwaka 2010 mahitaji yetu ya gesi yalikuwa futi za ujazo milioni 40, mwaka 2019 mahitaji yalikuwa futi za ujazo milioni 80 na sasa mahitaji ni futi za ujazo milioni 200 kwa siku,” anasema Dk. Kalemani.

Mtandao wa mabomba Dar es Salaam

Dk. Kalemani anasema lengo la kuanza na Dar es Salaam ni kutokana na kuwapo kwa mitandao ya gesi asilia.

Anaitaja mindao hiyo kuwa ni ule unaotoka Ubungo kuelekea Mikocheni kupitia UDSM, kupitia Mwenge ukijumhisha viwanda mbalimbali.

“Mtandao mwingine ni kutoka Ubungo kuelekea Tegeta, kupitia Mlalakua hadi Survey. Lengo ni kufika hadi Bagamoyo mkoani Pwani.

“Mtandao wa tatu ni ule wa Ubungo Maziwa kwenda hadi Gereza la Keko kupitia Shekhlango na Manzese. Pamoja na ule unaotoka Ubungo kwenda Tabata, Gongo la Mboto hadi Pugu. Tunayo mitandao hiyo minne ambapo kazi iliyobaki ni kusambaza gesi kwa ajili ya kuleta faida,” anasema Dk. Kalemani na kusisitiza kuwa mitandao hiyo lazima itumike vizuri.

Anaongeza kuwa mpango uliopo ni kuifikia mikoa ya karibu ambayo ni Morogoro, Pwani, Iringa, Mbeya na Dodoma.

Tayari TPDC imeunda kampuni tanzu ya Gasco ikiwa ni mahsusi kwa ajili ya kusambaza gesi hiyo nchini.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa William Anangisye, baada ya kuunganishwa na huduma hiyo chuoni hapo, anasema itasaidia kupunguza gharama za uendeshaji kiasi cha Sh milioni 400 zinazotumika kwa mwaka.

“Tunategemea gesi hii itachangia kuboresha mazingira yetu kwa maana ya kutumia gesi hii kwenye maabara zetu, ambapo tutaongeza ufanisi zaidi na kupunguza gharama. Tunatarajia kuokoa kiasi cha Sh milioni 500 katika bajeti yetu ya mwaka,” anasema Profesa Anngisye.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles