NA MOHAMED KASSARA
JINA la kiungo Gerson Fraga Viera limeanza kushika katika vijiwe mbalimbali vya soka hapa nchini, kutokana uwezo mkubwa anaoendelea kuuonyesha akiwa na kikosi cha Simba.
Mbrazil huyo alianza kubezwa hasa baada ya kuonekana hana ufundi mwingi kama walivyozoeleka wachezaji wanaotokea nchi hiyo inayofahamika zaidi kwa umahiri wa kusakata kabumbu.
Lakini kadri siku zinavyozidi kusonga mbele, mashabiki wa Simba wameanza kumuelewa na kufahamu ubora wa kiungo huyo mkabaji ambaye pia anamudu vema kucheza kama beki wa kati.
Viera si miongoni mwa wachezaji waliobakiwa kuuamuru mpira atakavyo kama walivyo Wabrazil wenzie, Ronaldinho Gaucho, Neymar , Robinho na wengineo, yeye anacheza soka la kimsingi (basics) ambalo linachezwa na Waingereza.
Wakati Wabrazil wenzake wakisifika kwa kuwatoa ulimi nje mabeki, yeye anafanya kazi ya mbwa ya kukimbiza viivuli vya washambulaji wa timu pinzani, ndiyo upande aliouchagua kuufanyia kazi.
Mwanaume huyo ni Mbrazil mwenye moyo wa Kiafrika, anafanya kazi ngumu ambazo zinafanywa na Claudio Makelele, Patrick Viera na viungo wengine wa aina hiyo.
Hali hiyo ndiyo inayomfanya kutokuwa kipenzi cha mashabiki, kwani wengi walitegemea kuona akiwalamba chenga za maudhi viungo kadhaa pinzani na kutoa pasi ya mwisho kwa Meddie Kagere.
Imezoeleka Mbrazil hata akiwa beki, basi ni lazima atakuwa na vitu adimu tu kama ilivyo kwa Marcelo na Dani Alves ambao unaweza kudhani ni mawinga kutokana na uwezo mkubwa wa kuuchezea mpira walionao na kusadia mashambulizi.Â
Kiungo wa Kibrazil ambaye kidogo anaonekana kufanya kazi ngumu ni Casemiro wa Real Madrid,hata hivyo nae ni fundi hatari, anamudu vilivyo kukusanya kijiji na kutoa pasi ya bao.Â
Haikuwa rahisi kwa mashabiki kuelewa anachofanya Viera uwanjani, alianza kudhihirisha ubora wake tangu Jonas Mkude alipokosekana kikosini katika michezo miwili ambayo Simba ilicheza dhidi ya Kagera Sugar na Biashara United.
Kazi kubwa aliyoiifanya katika michezo hiyo, iliwafanya wadau wa soka kuanza kumuangalia kwa jicho la kipekee na kugundua umuhimu wake katika kuilinda safu ya ulinzi ya Simba.
Hana mbwembwe nyingi, anatimiza majukumu yake muhimu ya kuilinda safu ya ulinzi, anaziba matundu yote ya wapinzani na kuanzisha mashambulizi kwa haraka.
Anajua kutibua mipango ya adui na kugongana na viungo watukutu na kuwapunguzia kazi mabeki wa kati ya kukutana mara kwa mara na washambuliaji wa timu pinzani.
Kile anachokifanya uwanjani si kila mmoja anaweza kukielewa isipokuwa kwa wale ambao wautazama mchezo kwa jicho la tatu na kuchambua majukumu aliyopewa.
Kazi anayoifanya Viera Simba, haina tofauti na ile anayoifanya Ng’olo Kante kwenye kikosi cha Chelsea na timu ya Tiafa ya Ufaransa kwa miaka mingi sasa.
Kante anasifika kwa uhodari wake wa kupambana vilivyo na viungo hatari wa timu pinzani, kuiba mipira na kuzuia mipira ya hatari kupenya kwenye ngome ya ulinzi, kazi ambayo imeifanya Chelsea kutikisa Ulaya.
Licha ya kutokuwa na ufundi mwingi wa kuuchezea mpira na kupiga pasi makini, lakini linapokuja suala la kudhibiti eneo la kiungo, Kante anaongoza katika chati ya viungo bora wa ulinzi duniani kwa sasa.
Nikukumbushe tu, Kante aliiwezesha Leicester City kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England mwaka 2015/16, mbele ya vigogo Liverpool, Manchester United, Chelsea wakiwa hawaamini.
Msimu ulioufata alihamia Chelsea na kuipa taji hilo, hadi sasa anawindwa klabu kadhaa za Ulaya zikiwemo, Real Madrid na PSG.
Kama ilivyo kwa Viera ambaye, licha ya kutotajwa sana, lakini huwezi kumaliza kusifu ubora wa eneo la kiungo la Simba bila kutaja ubora wake kwa kipindi hiki.Â
Viera alilidhihirisha hilo juzi katika mchezo dhidi ya Azam, unafikiri utampima wapi tena ubora wa Viera kama si kwenye mechi hiyo ambayo mara nyingi huamuliwa na ubora wa viungo ulionao.
Katika mchezo huo, Viera alipangwa kama kiungo mkabaji akisaidiwa na Mzamiru Yassin, huku jukumu lake kubwa likiwa ni kuhakikisha Salum Abubakar, Richard Djodi na wenzao hawapitishi mipira ya hatari kuelekea kwa Obrey Chirwa aliyekuwa akiongoza mashambulizi ya Azam.
Kuna wakati Azam ilikuwa juu sana mchezoni, ikimiliki mpira zaidi, hata hivyo mipango yao ilikuwa ikikatishwa na Mbrazili huyo anaicheza kwa kufuata malelekezo kama ilivyo kwa kiungo wa Liverpool, James Milner.
Viera hana kasi kubwa, hivyo mara nyingi hatoki kwenye eneo lake, hivyo kuisadia kuzuia hata mipira mirefu ya mashambulizi ya kushtukiza yanayoweza kufanywa na wapinzani iwapo wenzake watakuwa wamesogea juu kushambulia.
Kiungo huyo amewasahaulisha mashabiki wa Simba maumivu ya kumkosa Mkude katika kikosi chao hasa katika michezo ambayo inahitaji kuwa viungo wa shoka ili ushinde.
Ni ngumu kidogo kuamini, lakini ukweli ndiyo huo hakuna shabiki aliyehoji uwepo wa Mkude kwenye mchezo huo kitu ambacho ni nadra sana kutokea katika timu hiyo kwa muda mrefu sasa.
Mkude alijijengea heshima ya kipekee hasa inapokuja suala la mechi zinazohitaji utitiri wa viungo kupambania pointi tatu, Viera ameanza kuifuta kasumba hiyo.
Si tu anatishia ufalme wa Mkude, bali kwa sasa anafanya pia maisha ya Said Ndemla kuwa magumu pale Msimbazi, anamfanya aonekane mchezaji wa kawaida mno mbele ya macho Patrick Aussems.