24.4 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

‘Gereza Kwitanga lipatiwe kiwanda’

MWANDISHI WETU –OWM, KIGOMA

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Viwanda na Biashara ihakikishe gereza la Kwitanga mkoani Kigoma linapata kiwanda bora na cha kisasa cha kukamulia mafuta ya mawese kitakachoonyesha dhamira ya Serikali ya kufufua zao la michikichi nchini.

Hata hivyo  alisema ameridhishwa na jitihada zilizofanywa na Jeshi la Magereza katika kuboresha shamba lake la michikichi   na mabadiliko yaliyoyafanywa kwenye kiwanda chake cha kuzalisha mafuta.

Waziri Mkuu aliyasema hayo jana  alipotembelea Gereza la Kwitanga na kukagua shamba la michikichi,   kuzindua trekta na kufungua selo moja iliyojengwa gerezani hapo.

Alisema amefurahishwa baada ya kukuta mashine mpya ya kukamulia mafuta ya mawese inafungwa kwenye kiwanda cha gereza hilo ambayo itakuwa inatumia mota tofauti za zamani wapokuwa wanatumia mashine ya kusukumwa na mikono.

Kadhalika, Waziri Mkuu aliagiza Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) waimarishe teknolojia ya kukamua mafuta kwenye kiwanda hicho  kiweze kuzalisha kwa tija.

Katika kuhakikisha gereza hilo linakuwa la mfano kwenye kilimo cha   michikichi, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi inunue gari lenye winchi litakalorahisisha uvunaji wa chikichi.

Alisema njia inayotumiwa kwa sasa ya kupanda juu ya mchikichi wakati wa mavuno si salama kwa mvunaji, hivyo ni vema wakatumia magari hayo yenye winchi kwa ajili ya kurahisisha shughuli ya uvunaji.

Mkuu wa Magereza Mkoa wa Kigoma, Leonard Burushi alisema wamefanikiwa kuongeza uzalishaji wa mafuta kutoka mapipa 63.4 kwa mwaka 2016/2017 na kufikia mapipa 97 kwa mwaka 2018/2019 na uvunaji   unaendelea.

Burushi alisema mafanikio hayo yametokana na maagizo yalitolewa na Waziri Mkuu alipotembelea gereza hilo Julai, 2018.

Pamoja na mambo mengine aliwaagiza waboreshe eneo la kukamulia mafuta ili waongeze uzalishaji.

Pia mkuu huyo wa Magereza   Kigoma alisema eneo la ekari 20 limetengwa kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha kisasa cha kukamua   mawese, maghala ya kutunzia mafuta machafu na upanuzi wa kiwanda baadaye.

“Maelekezo mengine yaliyotolewa na Waziri Mkuu ni pamoja na Magereza ya Kwitanga na Ilagala yaongeze eneo la mashamba yake kwa ajili ya kupanda michikichi mipya ambalo limetekelezwa. 

“Tayari gereza la Ilagala limeandaa   ekari 150 zenye uwezo wa kupandwa michikichi aina ya tanera 8,550 na Kwitanga ekari 400 ambazo zitapandwa miche 22,800 ya michikichi aina ya tanera,” alisema Burushi. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles