19.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, October 4, 2022

GAZETI LA MAWIO KIFUNGONI MIAKA MIWILI

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe

NA MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

SERIKALI imelifungia gazeti la MAWIO kwa muda wa miaka miwili kwa kuchapisha habari na picha za marais wastaafu, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete na kuwahusisha na sakata la mchanga wa madini (makinikia).

Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya Rais Dk. John Magufuli kuvitaka vyombo vya habari kuacha kuwahusisha marais wastaafu na uchunguzi wa ripoti mbili za tume alizounda kuchunguza usafirishaji makinikia nje ya nchi.

“Wazee wetu hawa wamefanya kazi kubwa katika kulitumikia taifa waachwe wapumzike,” alisema Rais Magufuli katika taarifa yake iliyotolewa juzi na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa.

Kutokana na hali hiyo, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, alichukua uamuzi wa kulifungia kutochapishwa gazeti hilo la MAWIO na mtandaoni kwa mujibu wa kifungu cha 59 cha Sheria ya Huduma za Habari Na. 12, 2016.

Kwa mujibu wa taarifa ya Msemaji wa Serikali, Dk. Hassan Abbasi, hatua hiyo inatokana na gazeti hilo katika toleo na. 196 la 15-21 Juni, mwaka huu kuandika habari hiyo katika ukurasa wa mbele na makala katika ukurasa wa 12 iliyoandikwa ‘Lissu: Mkapa, Kikwete Wanaponaje?’

Alisema habari hizo zinawatuhumu viongozi hao kuhusika katika sakata la madini wakati ukweli ni kwamba hawakuwa sehemu ya uchunguzi wa kamati za Rais na wala matokeo ya kamati hizo hayakuwatuhumu kwa kosa lolote.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, licha ya utetezi wa Mhariri Mkuu wa gazeti hilo, taarifa ya Dk. Mwakyembe  imesisitiza kuwa habari hizo si tu zimekiuka agizo la Serikali, lakini pia zimekiuka vifungu vya 50 (a), (b), (c), (d) na (e) vinavyokataza uandishi wenye dhamira hasi.

“Sina budi kulifungia gazeti lako na kukutaka usitishe kulichapisha kwa nakala ngumu au ya mtandaoni kwa kipindi cha muda wa miezi 24 tangu tarehe ya barua hii kwa mamlaka niliyopewa chini ya Sheria ya Huduma za Habari Na. 12 ya mwaka 2016 kifungu 59.

“Natumia fursa hii kuvipongeza vyombo vingi vya habari ambavyo kuanzia leo (jana) vimefuata weledi wa taaluma na misingi ya sheria na kutii agizo la Serikali kwa kutowaingiza katika sakata hili pasipo na hoja za msingi viongozi wetu wastaafu,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,660FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles