33.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, March 22, 2023

Contact us: [email protected]

Gawio la Airtel kujenga hospitali Dodoma

NORA DAMIAN Na ANDREW MSECHU

-DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli amesema fedha za gawio zilizotolewa na Kampuni ya Bharti Airtel International zitatumika kujenga hospitali kubwa jijini Dodoma.   

Bharti Airtel jana ilikabidhi serikalini Sh bilioni 5.2, kati yake Sh bilioni 2.2 ni mchango wa kampuni hiyo katika kuunga mkono juhudi za Serikali.

Sh bilioni 3 zinatokana na malipo ya Sh bilioni 1 kila mwezi kwa Serikali, ikiwa ni utekelezaji wa makubaliano yaliyofanywa kati ya Serikali na kampuni hiyo kuhusu umiliki wa hisa za Kampuni ya Simu za Mkononi ya Airtel Tanzania.

Akizungumza jana baada ya kupokea fedha hizo, Rais Magufuli alisema sambamba na zile zilizokuwa zimepangwa kwa maadhimisho ya Muungano, zitatumika kujenga hospitali kubwa jijini Dodoma.

“Mazungumzo yamefikia mwisho, fedha zitakazokuwa zinalipwa kila mwezi kwa miaka mitano ni Sh bilioni 60, ukijenga vituo vya afya kwa Sh milioni 500 maana yake ni vituo 120.

“Ukijenga vya Sh milioni 400 maana yake ni vituo 150, kupata vituo hivi ni ukombozi wa hali ya juu.

“Tangu Airtel imeundwa miaka 19 yote, hakukuwa na gawio lolote, ninasema ni historia, tulikuwa na asilimia 40, lakini bado hatukupata hata senti tano, lakini pia tukabambikwa deni la Sh bilioni 930,” alisema.

MWAKILISHI BHARTI AIRTEL

Mwakilishi wa Bharti Airtel, alisema Januari 15 walifikia mkataba ambao ulisainiwa na Serikali na hisa za Serikali zimeongezeka na kufikia asilimia 49.

Hata hivyo, alisema kulikuwa na changamoto nyingi, lakini baada ya makubaliano walifikia hitimisho kwamba kampuni itaendelea kutoa Sh bilioni 1 kila mwezi.

“Hata kama kampuni inafanya biashara, ni lazima tutambue wajibu wetu kwa jamii, kampuni imepata nguvu mpya na tuko tayari kushirikiana na Serikali,” alisema.

Naye Waziri wa Fedha, Dk. Philip Mpango, alisema wamepata manufaa mengi kutokana na majadiliano baina ya Serikali na Bharti Airtel.

“Ulituagiza tuhakikishe tunafikia makubaliano ambayo sisi kama taifa tunapata na mwekezaji naye anapata. Tukio la leo (jana) ni ushahidi kabisa kwamba hilo ndilo lililofanyika, tulitii maagizo yako na kuhakikisha nchi yetu inanufaika na ule uwekezaji,” alisema Dk. Mpango.

Naye Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi, alisema hatua ya Bharti Airtel kufikia makubalianoi na Serikali imetoa funzo kubwa.

Alisema mara nyingi majadiliano ya aina hiyo yamekuwa yakilazimishwa kupelekwa kwenye mahakama au vyombo vya kimataifa kwa ajili ya kupatiwa ufumbuzi, lakini safari hii imekuwa tofauti.

“Kupitia makubaliano haya, tumejifunza kuwa si lazima changamoto kama hizi zipelekwe kwenye vyombo vya kimataifa, bali tunaweza kukaa chini na kufikia makubaliano.

“Tunachotaka kieleweke ni kwamba Serikali haina ugomvi na wawekezaji, bali inataka kujenga mazingira mazuri ili wao wapate na sisi tupate,” alisema.

Alisema ni vyema watumishi wa umma wajifunze kuwa hawana vyeo bali wana majukumu hayo wanayowafanya wawepo kwenye nafasi, hivyo ni vyema waangalie kuwa nchi inataka nini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,079FollowersFollow
563,000SubscribersSubscribe

Latest Articles