26.1 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

GARI LA MBUNGE LAGONGA NA KUUA

gari-la-mbunge

Na PENDO FUNDISHA

-MBEYA

GARI lenye namba za usajili T 161 CPP Toyota Land Cruiser linalodaiwa kumilikiwa na Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Chadema), maarufu Sugu, limemgonga mtembea kwa miguu katika kivuko cha barabara na kumsababishia kifo.

Tukio hilo limetokea jana saa mbili asubuhi katika eneo la Iyunga jijini hapa, wakati gari hilo likiwa njiani kuelekea Uwanja wa Ndege wa Songwe kwa mapokezi ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Dhahiri Kidavashari, aliliambia MTANZANIA Jumapili kwa simu kuwa aliyegongwa ni mtoto anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 13 na dereva wa gari hilo ni Gabriel Endrew (43), mkazi wa Mwakibete.

“Tukio limetokea saa mbili asubuhi ambapo gari T 161 CPP ilimgonga mtembea kwa miguu ambaye ni mtoto anayekadiriwa kuwa na miaka 13 ambaye jina lake halijafahamika na kumsababishia kifo,” alisema Kidavashari.

Pia alisema kuwa gari hilo limekamatwa na dereva anashikiliwa na polisi kwa mahojiano na uchunguzi wa tukio hilo unaendelea.

Gari hilo likiwa katika mwendokasi inadaiwa halikusimama kwenye kivuko cha watembea kwa miguu ndipo likamgonga mtoto huyo aliyefariki wakati akikimbizwa hospitali kwa matibabu.

Wakizungumza na MTANZANIA Jumapili kwa nyakati tofauti jana, baadhi ya mashuhuda, walisema mtoto huyo akiwa na mama yake, walikuwa wakivuka barabara baada ya magari ya upande wa pili kusimama na kuwaruhusu watembea kwa miguu kuvuka.

“Wakati mama na mtoto wakivuka, ndipo lilipotokea gari la mbunge likiwa katika mwendokasi na kumgonga mtoto huyo na mama yake na kusababisha kifo cha mtoto huku mama akijeruhiwa,” alisema Juma Hassan ambaye ni kondakta wa gari dogo la abiria aina ya Toyota Hiace lililokuwa likitokea Mbalizi.

Naye dereva aliyeshuhudia ajali hiyo, Lukas Michael, alisema wakiwa katikati ya kivuko hicho, mama wa mtoto huyo aliliona gari likija kwa kasi ndipo alipoamua kumwachia mtoto wake aliyekuwa amemshika mkono na yeye kutafuta njia ya kujiokoa.

Katika hatua nyingine, Katibu wa Chadema Kanda ya Nyasa, Franky Mwaisumbe, alisema Mbiwe alitarajia kuwasili jana jijini Mbeya kwa shughuli za kichama lakini ilishindikana baada ya kukosa usafiri wa ndege, hivyo atawasili leo asubuhi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles