*Hakuna madhara, ni baada ya kudhibitiwa
Na Esther Mnyika, Kahama
Dereva mmoja kati ya madereva 10 waliokuwa wakisafirisha sumu aina ya Sodium Cyanide amejeruhiwa baada ya gari alilokuwa akiendesha aina ya lori lenye namba za usajili T 124 ECX Scania mali ya Taifa Transport & Logistic kupata ajali eneo la Kagongwa-Kahama mkoani Shinyanga.
Akizungumzia ajali hiyo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Janeth Magomi amesema lori hilo lilipata ajali saa 3 asubuhi na kusababisha sumu hiyo iliyokuwa ikisafirishwa kupelekwa kwenye migodi mitatu kumwagika na kuleta taharuki kwa wananchi.
“Nilipata taarifa majira ya saa 3:20 asubuhi kuwa gari la Kampuni ya Taifa Transport & Logistic limedondoka katika Kata ya Kagongwa wilayani Kahama, hivyo nikawahi eneo la tukio, nilivyofika kwenye eneo la tukio ni kweli ajali imetokea na huduma za uokaji zilikuwazinaendelea ambapo dereva mmoja kati ya madereva kumi waliokuwa wakisafirisha sumu ya sodium cyanide amepata ajali na kapewa huduma na kuhakikisha madhara hayatokei kwa wananchi,” amesema ACP Mgomi na kusisitiza kuwa wananchi wa eneo hilo walipewa tahadhari wasisogee eneo la tukio kuna hatari hatua iliyosaidia kuepeusha madhara zaidi.
Amesema dereva huyo amepewa huduma ya kwanza kutoka kwa waaguzi na anaendelea vizuri.
Aidha, ACP Mgomi amewasisitiza wananchi waendelee kutoa taarifa kwa jeshi la polisi wanapoona matukio ya aina hiyo na wasisogee eneo hilo kwa tahadhari huku akisisitiza kwa kuwatoa hofu wananchi kuwa hali ni salama katika eneo hilo licha ya ajali hiyo kutokea na hivyo waendelee na shughuli zao.
Naye Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na Mkaguzi wa Wilaya ya Kahama, Edward Selemani amesema wao wamejianda kufanya uokaji muda wowote tukio linapotokea.
Amesema walivyopokea taarifa za tukio hilo walijiaanda kwa kuvaa vifaa vya uokozi na kuhakikisha sumu ya sodium cyanide isilete madhara kwa wananchi.
“Wananchi waendelee kuwa na tahadhari kubwa matukio kama haya yanapotokea na wasigelee eneo husika kwa sababu sumu ni hatari na unaweza kupoteza maisha,” amesema Selemani.
Upande wake Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kashime, Mabula Mabula amesema walipata mshituko kuona tukio la ajali hiyo.
“Ajali hii imetuogopesha tulikuwana taharuki maana gari limeandikwa hatari na sumu tukaona dereva anadondoka baada ya muda tukaona watu wanaangaika na kutoa huduma ya kwanza ikabidi tukae mbali na eneo hili,” amesema Mabula.
Awwali, Meneja wa Mradi wa Kampuni ya Taifa Transport &Logistic, Happiness Nyiti amesema amepokea taarifa za ajali akiwa kwenye Mgodi wa Buzwagi na kwamba ilimlazimu kufika kwenye eneo la tukio.
“Ni kweli ajali iliyotokea ni gari ya kampuni yetu gari aina ya scania lenye usajili wa namba T 124 ECX linalobeba sumu aina ya sodium cyanide inayopelekwa kwenye migodi ya Buzwagi, Bulyankulu na North Mara,” amesema Nyiti.
Amesema kwanza anashukuru vyombo vya usalama na wadau kwa kuweza kudhibiti ajali hiyo hadi sasa hakuna madhara yoyote yaliyotokea kwa wananchi na hali ya dereva anaendelea vizuri kwa sasa.
Aidha, amesema wanafanya mafunzo ya madereva wote wanaoendesha magari yanayobeba sumu ya sodium cyanide.
“Mafunzo hayo yanatolewa na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali na kupewa vyeti kwa ajili ya kusafirisha sumu ya sodium cyanide na tunahakikisha wakiwa safarini madereva wana vifaa vya kujikinga na sumu hizo ikiwepo mbele convoy leader na escot,”amongeza.