26.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, January 18, 2022

GAMBO AWAONYA POLISI MATUMIZI YA NGUVU KUPITA KIASI

MKUU wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo

 

ABRAHAM GWANDU Na JANETH MUSHI – ARUSHA

MKUU wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, ameviagiza vyombo vya dola mkoani hapa kuacha kutumia nguvu kubwa kupita kiasi wanapokuwa wakikabiliana na wananchi.

Gambo alitoa kauli hiyo juzi, kufuatia tukio la juzi la kuuawa kwa kupigwa risasi mwanafunzi wa darasa la saba, Nyangusi Long'ida (15) na watu wanaodaiwa kuwa askari wanaolinda msitu wa Meru-Usa katika Kijiji cha Lenjani, Wilaya ya Arumeru.

"Baadhi ya watu wetu wa vyombo vya dola wanatumia nguvu kupita kiasi, kwa mara ya kwanza walikufa watu wanne, juzi ameuawa mtoto wa miaka 15, kwanini vyombo vya dola vinaua watu wetu? Tena mtoto mdogo kama huyu asiyekuwa na hatia," alihoji Gambo.

"Nawahakikishia hatukubaliani na jambo hili, nitumie fursa hii kuviasa vyombo vya dola ni vizuri mkaacha kutumia nguvu zilizopitiliza, zipo namna nyingi za kuhakikisha tunaweka amani katika eneo lile, amekutuma nani kuua mtoto?" alisema.

Kiongozi huyo alitumia fursa hiyo kuwaomba wananchi wa eneo hilo kuwa watulivu wakati huu tukio hilo linapofuatiliwa na kuwa kitendo hicho kilichofanywa na askari huyo siyo dhamira wala maelekezo ya Serikali, bali ni utashi wa aliyefanya tukio hilo la kinyama.

Tukio hilo lilitokea juzi jioni, wakati marehemu akiswaga ng’ombe kandokando ya msitu huo na walinzi hao walipojaribu kumkimbiza ili wamkamate, alikimbia, ndipo wakampiga risasi na kufa papo hapo.

Akizungumza na vijana waliojaribu kuandamana jana ili kuwasilisha malalamiko yao kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, Diwani wa Kata ya Lemanyata, Loiseku Kiluso, alisema kuwa kijana huyo hakuwa ameingiza mifugo yake msituni, bali alikuwa akiwapitisha kando kando ya msitu huo kuwapeleka nyumbani.

“Yule mtoto marehemu alitoka kunywesha maji mifugo yake, akiwa njiani kuwarudisha nyumbani ndipo askari walipotaka kumkamata, akakimbia wakampiga risasi nne mgongoni na kufa palepale.

“Matukio haya ya kuua na kutesa watu sasa yamekithiri, hakuna wiki inapita bila watu kuteswa na hawa askari kwasababu tu ya kupita karibu na msitu. Wajawazito wanagaragazwa kwenye vumbi, wakina mama wanaopeleka watoto kliniki wananyanyaswa, wazee wananyanyaswa, hii haikubaliki,” alisema Diwani huyo.

Kiluso alisema tukio hili la kuuawa kwa Nyangusi lazima liwe tukio la mwisho na aliitaka Serikali kuwachukulia hatua kali za kisheria viongozi wa msitu huo waliohusika na kutoa amri ya wananchi kuuawa.

“Hakuna anayeshabikia msitu huu ufe, faida zake tunajua wote, lakini haiwezekani tukaulinda msitu kwa gharama za damu ya watoto wetu, kama Serikali haitatutetea tutajitetea wenyewe, kwasababu hii ni nchi yetu na tuna haki ya kufaidi matunda ya uhuru wetu,” alisema.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
174,926FollowersFollow
531,000SubscribersSubscribe

Latest Articles