26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 27, 2021

GAMBO ALIKOROGA

ABRAHAM GWANDU Na JANETH MUSHI

-ARUSHA

SIKU moja baada ya Jeshi la Polisi kwa amri ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, kuwakamata Meya wa Jiji hilo, Calist Lazaro, viongozi wa dini pamoja na waandishi wa habari 10 waliokuwa katika tukio la kukabidhi rambirambi katika Shule ya Msingi  ya Lucky Vincent, Jukwaa la Wahariri  nchini (TEF) limemuonya.

Kwa mujibu wa taarifa ya TEF iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Makamu Mwenyekiti wake, Deodatus Balile, chombo hicho kinafuatilia kwa karibu uhusiano wa Mkuu huyo wa Mkoa wa Arusha na vyombo vya habari kutokana na matukio ya mara kwa mara ya kudhalilisha wanahabari wanapokuwa kazini kwa amri yake.

“Matukio haya yakiendelea, tutalazimika kupitia uhusiano wa RC Gambo na vyombo vya habari nchini,” ilieleza taarifa hiyo ya TEF.

Hivi karibuni TEF ilipiga marufuku vyombo vya habari kuripoti taarifa nzuri zinazomhusu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, kutokana na hatua yake ya kuvamia kituo cha Clouds Media Group akiwa na watu wanaodhaniwa kuwa ni askari na zaidi akishindwa kuomba radhi.

Wakati TEF wakitoa msimamo huo, jana Gambo alisema agizo lake hilo lililenga kudhibiti wale wanaotishia amani katika mkoa wake.

Ingawa waandishi wa habari waliachiwa, lakini viongozi 13, akiwamo Meya pamoja na viongozi wa Shirikisho la wenye Shule na Vyuo binafsi nchini (Tamongsco) hadi jana walikuwa bado wanaendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi kwa agizo la Gambo.

Wengine wanaoshikiliwa ni Katibu wa Mbunge wa Arusha Mjini, Innocent Kisanyaga, Diwani wa Kata ya Olasiti, Alex Martin, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Lucky Vincent, Ephraim Jackson na viongozi wanne wa dini.

Akizungumza jana wakati akifungua warsha ya siku mbili iliyokutanisha wadau mbalimbali pamoja na jumuiko la mifuko ya hifadhi ya jamii nchini (TSSA), Gambo alisema yeye kama Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa anao wajibu wa kudhibiti viashiria vya kutoweka kwa amani katika eneo lake.

“Tofauti na nchi za wenzetu uchaguzi unapokwisha kila mmoja anaendelea na majukumu yake ili kupisha yule ambaye ilani yake imekubalika kwa wananchi atekeleze ilani hiyo, kama ulikuwa mwalimu unarudi kufundisha, Afrika na hasa Tanzania ni tofauti kidogo, watu wanafanya siasa kwa saa 24 mwaka mzima,” alisema Gambo na kuongeza;

“Hii kazi ni vita, unatandika pale unapoona viashiria vya kutoweka kwa amani, kama wanapanga maandamano unawafuata huko chumbani kabla hawajatoka huku nje kwa sababu ukiacha wakaandamana inakuwa mazoea, halafu siku ukitaka kuchukua hatua watadai unawaonea,” alisema Gambo.

Juzi Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Yusufu Ilembo, alithibitisha kuwa amri ya kuwakamata viongozi hao na waandishi wa habari 10 wakitekeleza majukumu yao walipewa na Gambo.

 

Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi kwa njia ya simu jana, Ilembo alisema hadi sasa wanaendelea kuwachunguza viongozi hao ili wajue wanawashitaki kwa makosa gani.

Kuhusu taratibu za mahakamani, alisema hawezi kujua kwa sababu utaratibu wa kupeleka watu mahakamani ni hadi mkuu wa polisi wa wilaya afungue mashitaka.

“Hadi sasa bado tunawashikilia kuwachunguza na kuhusu majina siwezi kuyatoa sasa hivi, ila wako 13 na kuhusu taratibu za kuwafikisha mahakamani wewe  unajua utaratibu wa kupeleka watu mahakamani hadi OCD afungue mashitaka,” alisema.

Juzi akiwa shuleni hapo, Katibu Mkuu wa Tamongsco Kanda ya Kaskazini, Leonard Mao, alisema walitoa Sh milioni 18 za rambirambi kwa walengwa moja kwa moja ambao ni familia za wanafunzi 32, walimu wawili na dereva mmoja aliyepoteza maisha katika ajali hiyo iliyotokea Mei 6, mwaka huu katika eneo la Marera, Rotia Wilaya ya Karatu mkoani Arusha na majeruhi watatu wanaopatiwa matibabu nchini Marekani.

 

“Hakuna senti ya mtu itaenda pembeni, hatumpi mtu kama si mzazi, wala shule, tuliona majeneza 35 na majeruhi watatu, hivyo kiasi hiki kitagawiwa kwa familia 38, watakaokuwepo hapa na wale ambao hawapo shule itatupa utaratibu wa kuwafikia, kila mtu atapewa fedha mkononi,” alisema.

Pia alisema kuwa, michango hiyo imetolewa na watu 139 na wataweka wazi katika mitandao ya kijamii baada ya kukabidhi rambirambi hizo ili waliozitoa wasione fedha zao zimeliwa na kuwataka wazazi kuendelea kujipa moyo.

Awali, kabla ya kukamatwa kwa viongozi hao, Lazaro alisema shirikisho hilo limetuma wawakilishi kwa ajili ya kuwasilisha rambirambi zao kwa wazazi na watoto waliofariki, hivyo aliwaomba waje wakabidhiwe.

Wakati huo huo, TEF imesema kuwa, Kituo cha Star TV kimejitangaza kama adui wa tasnia ya habari nchini kutokana na uamuzi wake wa kutoa matangazo kuwa watafanya mahojiano na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.

TEF ilisema katika uamuzi wao huo wa kumfungia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ambao pia uliungwa mkono na Umoja wa Klabu za waandishi wa habari nchini (UTPC), Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari nchini (MOAT) na taasisi nyingine za kihabari, waliazimia kuwa yeyote atayeshirikiana na kiongozi huyo naye watamhesabu kama adui wa tasnia ya habari nchini.

“Star TV wameamua kushirikiana na Makonda, basi ni wazi wameamua kwa hiari yao wenyewe kujitangaza kama adui wa tasnia ya habari nchini, kila Mtanzania anajua jinsi ya kupambana na adui kwa nia ya kujilinda na tasnia haitasita kufanya hivyo,” ilieleza taarifa hiyo ya TEF.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
163,371FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles