HATIMAYE Mutasim Sirelkhatim Gaffar wa Sudan, amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), baada ya kupata kura sita kati ya 10 katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika jana mjini Addis Ababa, Ethiopia.
Katika uchaguzi huo, Mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Leodegar Tenga, alijitoa dakika za mwisho kutetea nafasi yake baada ya kuliongoza baraza hilo katika vipindi viwili.
Katika uchaguzi huo, mgombea mwingine ambaye ni bosi wa zamani wa Shirikisho la Soka nchini Uganda (FUFA), Lawrence Mulindwa, alibwagwa vibaya baada ya kupata kura mbili.
Mulindwa alichaguliwa kuwa mjumbe wa kamati ya utendaji ya Cecafa Novemba 2013 na pia alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Cecafa Februari 2014.
Wagombea wengine ambao waliwania nafasi ya uenyekiti ni Vincent Nzamwita (Rwanda), alipata kura moja wakati  Juneid Bashar Tilmo wa Ethiopia alipata kura moja.
Tenga ambaye alikuwa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuanzia mwaka 2014- 2013, alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa Cecafa tangu mwaka 2007, alipochukua nafasi ya Dennis Obua kutoka nchini Uganda.