26.8 C
Dar es Salaam
Saturday, September 7, 2024

Contact us: [email protected]

Gadiel hataki masihara Simba

>>Atinga kambini asubuhi na mapema, Kahata naye hakuna kuchelewa

NA SOSTHENES NYONI-DAR ES SALAAM

BEKI mpya wa Simba, Gadiel Michael ameonyesha kwamba hataki masihara linapokuja suala zima la umakini katika kazi, baada ya kuwa miongoni mwa wachezaji wapya wa timu hiyo ambao jana waliwasili mapema kambini.

Gadiel aliyesajiliwa na Simba kwa mkataba wa miaka miwili, akitokea Yanga, aliwasili katika kambi ya timu hiyo iliyoko Hoteli ya Sea Scape, Dar es Salaam saa 3 asubuhi, akiwa katika gari aina ya Toyota Crown.

Mbali ya Gadiel, wengine wapya waliowasili hotelini hapo ni   Francis Kahata, Wilker Henrique da Sliva, Gerson Fraga, Traone Santos da Sliva, Eldin Sharaf ‘Shibobo’,  Beno Kakolanya, Kennedy Juma na Miraji Athuman.

Kwa upande wa nyota wa zamani walioshuhudiwa na MTANZANIA wakitinga kambini hapo, ni beki wa kulia, Shomari Kapombe, nahodha msaidizi, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’,  Rashid  Juma na Clatous Chama.

Katika hatua nyingine, klabu ya Simba leo  itaendesha semina ya ndani kwa wachezaji na viongozi wake wa benchi la ufundi.

Kwa mujibu wa taarifa ya Simba, semina hiyo ina lengo la kuwapa wachezaji na viongozi wa  benchi la ufundi, historia yake, miiko ya klabu hiyo, kanuni, desturi, nidhamu na malengo ya msimu wa 2019-2020.

Kikosi cha timu hiyo, kitakwenda Afrika Kusini, ambako kitapiga kambi ya kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano ya kimataifa.

Wekundu hao ndio mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, wakitwaa ubingwa msimu huu ikiwa ni mara ya pili mfululizo, baada ya kufanikiwa kufanya hivyo pia msimu wa 2017-18.

Pia ilifanikiwa kutinga  hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika,  kabla ya kutupwa nje na TP Mazembe ya Jamhuri ya  Kidemokrasia ya Kongo (DRC), baada ya kulazimishwa suluhu nyumbani kisha kuchapwa mabao 4-1 jijini Lubumbashi.

Mafanikio hayo ya Simba na kuchanganya na yale ya Yanga, yaliifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 12, ambazo Shirikisho la Soka Afrika (CAF) huziruhusu  kuingiza timu nne katika michuano yake, ambayo ni Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho.

Timu za Simba na Yanga zitaiwakilisha Tanzania katika michuano ijayo ya  Ligi ya Mabingwa Afrika, wakati Azam na KMC zitashiriki Kombe la Shirikisho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles