30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Fukuto la Maalim Seif

*Apewa kadi namba moja ACT, asema kama CUF walidhani chama ni majengo amewaachia

*Profesa Lipumba aonya wanaochoma bendera, ataka waliokuwa kwa Seif warudi kujenga chama

*Msajili, Polisi wawashukia wafuasi wanaofanya vitendo vya kihalifu,

NORA DAMIANNa ANDREW MSECHU-DAR ES SALAAM

ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, amekabidhiwa kadi ya uanachama wa ACT – Wazalendo huku akisema si nia yake kukiteka chama hicho.

Maalim Seif alikabidhiwa kadi namba moja jana na Kiongozi wa ACT – Wazalendo, Zitto Kabwe, sambamba na wafuasi wengine waliokuwa wakimwunga mkono kutoka Zanzibar na Bara.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa kadi hiyo, alisema amekwenda ACT kuongeza nguvu ili Watanzania wajue kuna chombo kinachoweza kuleta mabadiliko makubwa ya kisiasa na kiuchumi.

“Nimehemewa kwa mapokezi mazuri, najiona ni mwenyeji hapa, mmenipa heshima kuniambia nichukue kadi namba moja, mama yangu wee, nawashukuru sana.

“Tulipokuwa CUF tulijitahidi kujenga taasisi ndio maana wakati mwingine nilikuwa naondoka nchini kwa miezi sita chama kinakwenda. Hata ACT tunajenga taasisi lakini huwezi kuzuia watu na mapenzi yao,” alisema Maalim Seif

Alisema ACT imejipambanua inataka kufikia malengo na kwamba hakuna ubabaishaji ndio maana alivutiwa kujiunga nacho.

“Nimejiunga na ACT kwa sababu tumeridhika na malengo yake, ‘serious’ na utendaji wa shughuli za kisiasa katika nchi.

“Si kwamba vyama vingine havina maana, tulikwenda Chadema, NCCR – Mageuzi na NLD lakini kwa kuwa ACT walileta ombi la kujiunga na Ukawa, tulichagua kile ambacho moyo wangu utaridhika na sisi tuliridhika kuja ACT.

“Niwatoe wasiwasi wanachama wa ACT, tujue tuna jukumu kubwa kwa wananchi, wanababaika hawajui waende wapi, tunaungana nanyi kuwaonyesha njia,” alisema.

Aliwataka wanachama wa ACT – Wazalendo kuepuka kuingia kwenye malumbano na badala yake wafikirie watasonga vipi katika mapambano ya kisiasa.

“Mtachokozwa hasa na mitandao ya kijamii, msikubali kuchokozeka wala msijibizane nao, muwapuuze. Tutawala mitandao kwa fikra na mawazo vipi tutasonga mbele katika mapambano haya.

“Nchi inahitaji kurudi kwenye misingi ya demokrasia, tupambane lakini kwa busara kubwa na si kwa maguvu,” alisema Maalim Seif.

Alipoulizwa kama ana nia ya kugombea urais Zanzibar katika uchaguzi mkuu ujao alisema hivi sasa ni mapema kuzungumzia suala hilo.

“Mbona hili swali waandishi mnalipenda sana, sasa ni mwaka 2019 hivyo bado halijafika wakati wake,” alisema.

Alimmwagia sifa Zitto kuwa ni kiongozi mwenye ujasiri wa pekee na amekuwa akipambana na wakubwa kwa hoja.

“Hatoi matamko bila kufanya utafiti kwanza na haogopi hata kusema hadharani. Zitto si mnafiki si aina ya kiongozi anayejikombakomba kwa wakubwa…anapambana na wakubwa kwa hoja,” alisema.

Alisema wao wameamua kuondoka CUF na baadhi ya watu wamewafuata, hivyo waliobaki huko kama wanadhani chama ni majengo basi wabaki nayo.

Kuhusu ofisi za CUF zinazobadilishwa rangi na kupakwa ya ACT, alisema ofisi nyingi zilikuwa za watu na kwamba ambazo ni mali ya CUF ni Ofisi ya Makao Makuu Mtendeni, Kilimahewa pamoja na ile ya Buguruni Dar es Salaam.

ZITTO

Kwa upande wake Kiongozi ACT – Wazalendo, Zitto Kabwe, alisema ujio wa Maalim Seif katika chama hicho ni hatua muhimu ya kuimarisha juhudi za kujenga demokrasia nchini na kuimarisha upinzani.

“Nasisitiza tutaendelea na safari ya mapambano ya kudai haki na demokrasia katika nchi yetu. Jambo hili litafsiriwe kwamba ni hatua muhimu za kuimarisha juhudi zetu za kujenga demokrasia Tanzania na kuimarisha zaidi upinzani.

“Ukiwa kiongozi ambaye uko kwenye mioyo ya wananchi kamwe hawawezi kukutupa. Kupitia somo la Maalim tuone umuhimu wa kujenga demokrasia na imani ya watu ambao wanakupa dhamana, wanakuwa tayari kufanya lolote ili mradi kufika mlikotarajia.

“Nchi hii ni yetu sote na Watanzania wanataka wafanye kazi na wafurahie matunda ya kazi zao, tutahakikisha Tanzania Bara na Zanzibar wananchi wanaweza kupata uongozi mbadala utakaoleta mabadiliko,” alisema Zitto.

Zitto alisema pia tangu juzi baada ya Maalim Seif kutangaza kujiunga na chama hicho, viongozi wengi wakiwamo wa Chadema walimpigia simu na wengine kumtumia ujumbe mfupi kumpongeza kwa hatua hiyo.

“Viongozi wengi wamefarijika sana, Mbowe (Mwenyekiti Taifa Chadema), Salum Mwalim (Naibu Katibu Mkuu Chadema Zanzibar) na wengine wamenipigia simu kutupongeza.

“Nimefarijika sana kwa sababu juhudi za ujenzi wa mshikamano na upinzani katika nchi yetu ni za lazima kwa sababu changamoto zinatulazimisha kushirikiana,” alisema.

KADI ZA UANACHAMA

Zitto alisema walipozindua chama walitenga kadi maalumu ambazo viongozi wao mbalimbali walizichukua lakini kuna baadhi yao walikumbwa na dhoruba.

“Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje, Venance Msebo, alisema anakomboa kadi namba moja atakayopewa Maalim Seif pamoja na kumlipia ada ya miaka 10. Mimi kadi yangu ni namba nane,” alisema Zitto.

Wengine waliokabidhiwa kadi ni Juma Duni Haji, Mbarara Maharagande, Ismail Jussa, Shaweji Mketo, Rehema Shamte Rwambo, Hassan Abdallah Hassan, Asha Msangi, Ishaka Machinjita, Kuluthum Mchuchuri na Omary Ally Sheikh.

Wengine ni Nurudin Msati, Zahra Ally Hamad, Najma Khalifan, Abdallah Said Hatawu, Mustapha Wandwi, Bonafasia Mapunda, Bamkubwa Buda, Mohamed Nurudin Mohamed, Halima Ibrahim, Hamad Khalifan, Muhidin Thabiti, Hania Chaurembo, Masoud Faki Masoud, Juma Mkumbi na Hassan Bakari Haji.

Kiongozi huyo wa ACT alisema wafuasi wengine wa Maalim Seif wataendelea kupatiwa kadi za chama hicho kupitia kwenye matawi ili wawe na rekodi sawa na kuepuka kuingia kwenye mtego wa msajili wa vyama vya siasa.

“Kama Bimani ameshindwa kuja leo (jana) kwa sababu ana kazi maalumu anaendelea nayo kule (akimaanisha Zanzibar) hivyo, kadi yake tutakwenda kumkabidhi kule kule,” alisema Zitto.

Msajili aibuka

Katika hatua nyingine, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, amewaonya wafuasi wa Maalim Seif, wanaochoma bendera za Chama cha CUF.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana jioni, Jaji Mutungi alisema kifungu cha 11C cha Sheria ya Vyama vya Siasa Sura ya 258 kinakataza  mwanachama au kiongozi yeyote kufanya kitendo hicho.

“Mwanachama au kiongozi yeyote wa chama cha siasa anayefanya kitendo chochote kinachodhihaki bendera ya chama kingine na adhabu ya kosa hii ni faini isiyozidi Sh milioni moja  au kifungo kisichozidi miezi sita au adhabu zote mbili.

“Vile vile katika mtandao wa kijamii kuna video inaonyesha  watu wakipandisha bendera ya ACT-Wazalendo kwa kutumia tamko takatifu la dini ya kiislamu (Takbira).

“Kitendo hiki sio tu ni dhihaka bali pia ni ukiukwaji mkubwa wa sheria za nchi hususani sheria ya vyama vya siasa, hivyo jambo hili linafanyiwa kazi na ofisi ya Msajili kwani kifungu cha 9 cha sheria ya vyama vya siasa kinakataza chama cha siasa kutumia dini kufikia malengo yake.

“Natumia fursa hii kuwaasa wanachama na mashabiki wote wa vyama vya siasa waepuke na wasijihusishe na vitendo vyote vile vya uvunjifu wa sheria, kwani wakifanya hivyo watachukuliwa hatua za kisheria wao binafsi na chama chao.

“Mwisho japo si kwa muhimu, nawasihi na kuwasisitiza viongozi wa Vyama vya Siasa katika ngazi zote kwamba mnaowajibu wa kuwaongoza na kuwaasa wanachama mnaowaongoza kuhakikisha wanatii sheria za nchi, ikiwamo kujiepusha na uvunjifu wa sheria wa aina yoyote ile,”ilisema taarifa hiyo.

Lipumba na mali za chama

 Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, alisema watachukua hatua dhidi ya wanachama wanaohamia ACT Wazalendo ambao wanapora mali za chama hicho kinyume cha sheria.

Akizungumza na wandishi wa habari jana, jijini Dar es Salaam, Profesa Lipumba alisema chama hicho hakitawavumilia wanaopora mali za chama hicho ambazo zimetafutwa kwa jasho la wanachama.

“Hatua hiyo ni utapeli na wizi wa wazi, hivyo chama changu kitafuata utaratibu wa kisheria kuzirejesha. Hili ni jambo la kisheria, mali za chama zitaendelea kuwa za chama.

“Hao wanaobadili rangi majengo ya chama ninawaambia, akili za Maalim Seif wachanganye na zao, kwa sababu jinai itawahusu wao binafsi na huyu maalim hatakuwa nao,” alisema Profesa Lipumba.

Alisema hata vitendo vya kuchoma bendera za chama hicho vinavyofanywa na wafauasi wa Maalimu Seif, havikubaliki kwa kuwa ni kinyume cha tararibu na sheria za nchi.

Alisema anatambua kuwa zipo ofisi za chama katika baadhi ya maeneo ambazo zilitolewa za wanachama, lakini zipo nyingine ambazo ni mali ya chama kwakuwa zilinunuliwa na kuwa chini ya umiliki wao.

Alitaja mali  zilizo Zanzibar anazokumbuka kwa haraka kuwa ni ofisi ya Mtendeni, ambayo ilinunuliwa kwa Sh milioni 83, ofisi ya Kilimahewa iliyonunuliwa kwa Sh milioni 23, Ofisi ya Shamba Jumbi iliyonunuliwa kwa Sh milioni 21, viwanja vya Tunguu vilivyonunuliwa kwa Sh milioni 28.

Alisema anafuatilia kwa karibu mali hizo za chama kwakuwa ana uhakika ofisi nyingi za  matawi na wilaya ni mali za chama.

Profesa Lipumba alisema kuna watu wenye fikra nzuri ambao walikuwa wanamuunga mkono Maalim Seif na hawawezi kubadilisha maamuzi yao na kumfuata ACT.

Alisema anawashukuru baadhi ya wanachama wenye nia njema ambao wameamua kutokubaliana na uamuzi wa Maalim Seif kuhama.

“Nataka kuwambia wale wote ambao mlikuwa sambamba na Maalim Seif, wenyeviti, madiwani, wabunge na wanachama wa CUF tujumuike na tuwe pamoja katika kukijenga chama chetu,” alisema.

Wabunge

Katika hatua nyingine, baadhi ya wabunge waliokuwa wakimuunga mkono Maalim Seif wameanza kumuunga mkono Profesa Lipumba.

Jana, mbunge wa Mchinga, Hamidu Bobali (CUF) alitangaza kumuunga mkono Profesa Lipumba.

Alisema wapo wengi watakaorudi kuungana na Profesa Lipumba na hivi sasa ni wakati wa kukijenga chama na walioondoka kwenda sehemu nyingine ni utashi wao.

“Nimerudi nyumbani baada ya msuguano uliodumu kwa miaka mitatu ndani ya CUF na uliokidhoofisha chama, nawaomba mnisamehe kwa yaliyotokea.

“Najua kuna wenzangu wanataka kurudi lakini wanashindwa wataanzia wapi, nawaambia mimi nimeonyesha njia waje wasiogope wakati ndio huu,” alisema.

Alisema makubaliano yao yalikuwa kwamba wataheshimu uamuzi wa mahakama na kurudi kujenga chama, wala si kuhama kama alivyofanya Maalim Seif.

Alisema ni vema wabunge wote, madiwani na wenyeviti wa Serikali za Mitaa na Vitongoji waendelee kukiunga mkono chama chao kwa kuwa si vema kuchukua maamuzi ya hasira kwa kukurupuka au kufuata mkumbo.

Polisi na bendera

JESHI la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi  Zanzibar limesema kuwa halitosita kuchukua hatua za kisheria juu ya watu wanaoshusha bendera na kuzichoma moto kwani kufanya hivyo ni kuvunja sheria.

Akizungumza jana Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Thobias Sedoyeka alisema pamoja na baadhi ya wafuasi wa CUF kushusha bendera na kupandisha za Chama cha ACT- Wazalendo, ni lazima wajue kwamba wapo wanaovunja sheria za nchi.

Alisema licha ya shughuli hiyo kuendelea katika maeneo mbalimbali, lakini alitahadharisha kwa wafuasi hao watekeleze shughuli zao hizo kwa kufuata sheria za nchi pamoja na utaratibu na kanuni za uendeshaji wa vyama vya siasa.

“Tunasikia kuna watu wanatia rangi matawi yao pamoja na kushusha (bendera za CUF) na kupandisha bendera za ACT- Wazalendo, tunachowaomba sisi wafanye shughuli zao hizo kwa kufuata sheria.

“Ila kama itatokea kuna ishara ya kufanyika uvunjifu wa amani hatutasita kuchukua hatua stahiki mara moja,” alisema Kamanda Sodeyeka.

Kamanda Sedoyeka, alisema si busara kuona hivi sasa amani ya nchi inaendelea kuwa katika hali nzuri kisha wakajitokeza watu wachache wakaichafua kwa maslahi yao au kisingizio cha siasa.

Kutokana na hali hiyo alitoa wito kwa wafuasi na wananchi mbalimbali wanaoshiriki shughuli hizo kuendelea kutunza amani huku akisema Jeshi la Polisi limejipanga vyema kiulinzi katika maeneo yote.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles