*Pluijm asema hana taarifa ya kibarua chake kuwa shakani
Na WINFRIDA NGONYANI-DAR ES SALAAM
KLABU ya Free State Stars ya Afrika Kusini, imeungana na Yanga katika kutaka kunasa saini ya Mzambia, George Lwandamina, aliyetajwa kufanya mazungumzo na Yanga kwa ajili ya kujiunga na mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Free State Stars klabu ambayo aliwahi kuchezea winga wa zamani wa Yanga, Mrisho Ngassa, iliwahi kuwa chini ya Kocha Mmalawi, Kinnah Phiri ambaye anaifundisha Mbeya City, lakini kwa sasa mshambuliaji aliyewahi kuichezea klabu za Simba na Yanga Mganda, Hamis Kiiza, amejiunga nayo.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Lwandamina ambaye ameifundisha Klabu ya Zesco United kwa mafanikio ambayo msimu huu ilifanikiwa kuingia hatua ya nusu fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya kutolewa na Mamelody Sundown ya Afrika Kusini, kocha huyo alisema anazo ofa nyingi mezani ambazo zimemfikia hivyo ataangalia ipi itakuwa na manufaa kwake.
“Timu ambazo nimezungumza nazo ni Yanga na Free State, ila zipo nyingine zimetuma ofa ambazo bado sijazijibu, naangalia timu yenye masilahi niweze kujiunga nayo, pia si masilahi tu naangalia na ubora wake hasa ushiriki wa michuano ya kimataifa inayohusisha klabu,” alisema.
Kocha huyo aliyeifundisha Zesco kwa miaka mitatu ya mafanikio, alisema anatumai klabu zote zilizotuma ofa zimeona uwezo wake wa kunoa timu na kuzipa mafanikio, hivyo si kama zimebahatisha kutuma ofa zao.
Hata hivyo, Kocha wa Yanga, Hans van der Pluijm, alisema hana taarifa ya kibarua chake kuwa shakani.
“Sijapata taarifa yoyote bado, nasoma magazetini subirini labda uongozi utaeleza hatima ya haya yanayosemwa,” alisema Pluijm.