27 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Foleni bandarini Dar iangaliwe sawasawa

Na MWANDISHI WETU

-DAR ES SALAAM

KWA muda sasa wadau mbalimbali wakiwemo watumiaji mbalimbali wa bandari, wazawa na wageni kutoka nchi jirani, wasafirishaji wa mizigo, madereva  wa malori, makampuni mbalimbali yaliyopo jirani na bandarini hasa makampuni ya mafuta, makampuni ya kuhifadhi makontena na wengineo wengi  wamekuwa wakilamikia  foleni  ndefu  katika  Bandari  ya Dar es  Salaam inayodaiwa  kutokana  na mfumo  wa uendeshaji  wa bandari  hiyo. 

Wadau hao wanasema foleni hiyo hutokea wakati  uongozi  wa bandari  wanapoyafanyia ukaguzi  katika mashine  za kukagua  mizigo inayotoka ama kuingia  ili kubaini  kama ina taarifa  sahihi  ama la na hasa taharuki kubwa sana ipo upande wa Kurasini Highway kwenye mizani mipya ya kupima uzito wa malori yanayotokea bandarini au yanayotoka kupakia mizigo mbalimbali kutokea maghala ya jirani na bandarini.

Ukaguzi ni suala muhimu sana ili kujiridhisha kuhusu mizigo iliyoko kwenye makontena na hasa suala la uzito wa haya malori ili kulinda na kutunza barabara zetu, lakini ukaguzi huo usiwe usumbufu na kusababisha gharama kubwa sana zinazotokana na kuchukua saa nyingi sana za uendeshaji wa zoezi la kupima mizigo katika mizani ya Kurasini.

Ikumbukwe baadhi ya mizigo hiyo inakwenda nchi za nje na wasafirishaji mizigo wamepewa muda mahsusi wa kufikisha mizigo hiyo kunakohusika na hasa katika mipaka mbalimbali ya nchi yetu. 

Hali kadhalika, ikumbukwe kuwa bandari ya Tanzania ipo katika ushindani mkubwa na bandari za jirani kama vile Mombasa, Beira, Nacala, Maputo, Djibouti na Durban. Kwa sasa Bandari ya Dar es Salaam ina uwezo wa  kupokea meli kubwa yenye urefu wa mita 264 aina ya Northern Power ambapo awali meli zenye ukubwa huo hazikuweza kutia nanga kwenye bandari hiyo na kutoa fursa kwa Bandari za Durban, Afrika Kusini  na Mombasa nchini Kenya.

Wahusika wa Bandari ya Dar es Salaam wanapaswa kulichukulia suala hili kwa umuhimu mkubwa ili kuendelea kulinda heshima ya bandari yetu ambayo imekuwepo kwa muda mrefu.

Ukiachana na ushindani, kuna suala nyeti sana la usalama. Bandari imezungukwa na maghala makubwa sana ya mafuta na gesi na mabomba mbalimbali yanayotoka bandarini kuelekea katika haya maghala. 

Msongamano huu wa malori unaosababisha barabara zote jirani kufungwa, shughuli kusimama ni hatari sana endapo ajali ya moto au dharura ya kupitisha magari ya zimamoto, magari ya wagonjwa ama utatuzi wa dharura nyingineyo huenda isiwe na mafanikio sababu ya huu msongamano. Katika siku za wiki, msongamano wa magari yasiyotembea huanzia Kurasini Highway kupita maghala ya mafuta.

Ili kuondoa msongamano wa malori hayo wakati wa ukaguzi ni suala ambalo liko ndani ya uwezo wa mamlaka nzima ya bandari na mamlaka nyingine zinazohusika kwani kwingineko mbona imewezekana. 

Mfano, mitambo ya kupimia uzito ingetofautisha magari ya hapahapa Dar es Salaam, magari ya hapahapa nchini na magari yanayoenda nje ya nchi. Wangeweka kima cha chini cha uzito ambapo gari ikiwa ndani ya hiki kima, isipoteze muda bali ipite na kuendelea na safari. 

Endapo gari imezidisha uzito, ipewe muda mchache sana wa kuegesha maeneo maalumu kwa muda mfupi, ambapo ukizidishwa mwenye gari alipishwe tozo. 

Magari yanayopanga mizigo upya yawe na maeneo maalumu au kuwekwe tozo maalumu ili kusukuma ufanisi.

Hivyo, tunaamini wakati huu wa Serikali ya Awamu ya Tano ya hapa kazi tu, usumbufu huo utatafutiwa jawabu kwani inawezekana.

Ni jambo la ajabu kwa karne ya sasa watu wenye weledi kushindwa kutafuta namna rahisi ya kukagua na kupima mizigo kwa njia ambayo haitasababisha msongamano kama huu tunaoshuhudia katika Bandari ya Dar es Salaam.

Mmoja wa madereva hao, Hamisi Dongo, anasema  wamekuwa wakilazimika  kukaa  kwa muda  mrefu  katika foleni kutokana na kaguzi mbalimbali zinazofanyika  bandarini  hapo  na hivyo aliiomba Serikali  kuangalia upya namna bora  ya kufanya  ukaguzi  ili kurahisisha na kuokoa muda unaopotea.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles