30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Flaviana Matata Foundation yasaidia taulo za kike wanafunzi wenye ulemavu

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Taasisi ya Flaviana Matata, imetoa msaada wa katoni 12 za taulo za kike kwa wanafunzi wenye ulemavu wa macho katika Shule ya Msingi ya Uhuru Mchanganyiko ili kuhakikisha hawakosi masomo kwa sababu ya kutomudu gharama ya taulo hizo.

Baadhi ya walimu katika shule hiyo wamekuwa wakilazimika kuchangishana fedha kwa ajili ya kuwanunulia wanafunzi wao taulo za kike ambao wengi wanatoka katika familia zenye kipato cha chini na hivyo kushindwa kumudu gharama ya taulo hizo.

Taulo hizo za kike zimekabidhiwa na Diwani wa Viti Maalumu Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Asha Johari Mohamed ambaye pia aliambatana na Mwakilishi wa Taasisi ya Flaviana Matata, Kisha Kishaju.

“Tunaamini msaada huu utasaidia kuinua ufaulu kwa mabinti zetu, tuwaombe utumike kwa malengo ambayo taasisi na wahisani wamekusudia,” amesema Asha.

Mwakilishi wa taasisi hiyo, Kisha Kishaju, amesema wana maombi mengi na kwamba msaada kama huo umepelekwa pia Shule za Msingi Mbigili, Ikungi na Shule ya Sekondari Korogwe.

Flaviana Matata foundation imetoa taulo hizo za kike Shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko kufuatia habari iliyoandikwa na mwandishi wetu juu ya wanafunzi wengi wenye ulemavu shuleni hapo kushindwa kuhudhuria masomo kwa kukosa taulo za kike wanapokuwa kwenye hedhi.

Naye Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko, Sezaria Kiwango, ameshukuru kwa msaada huo na kuwaomba wadau wengine kujitokeza kuwasaidia kwani kuna uhitaji mkubwa.

“Kuna uhitaji mkubwa wa taulo za kike kwa sababu wanafunzi wengi wenye ulemavu wanatoka familia za kipato cha chini na wengine wanaishi hosteli,” amesema Mwalimu Kiwango.

Taasisi hiyo imekuwa ikigawa taulo za kike katika maeneo mbalimbali nchini huku walengwa wakiwa ni wale walio katika mazingira magumu ili wanapokuwa katika hedhi waweze kujisitiri na kuendelea kuhudhuria masomo.

Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) mwaka 2019 ulibaini kuwa asilimia 60 ya wasichana walionekana kutomudu taulo za kike hivyo uhamasishaji wa kupata taulo hizo bado unahitajika zaidi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles