25.4 C
Dar es Salaam
Monday, January 30, 2023

Contact us: [email protected]

FINLAND YATOA BIL 71/- KILIMO BIASHARA CHA MITI

Na HARRIETH MANDARI


KATIKA jitihada za kuboresha kilimo biashara cha miti nchini pamoja na utunzaji misitu, Serikali ya Finland kupitia ubalozi wake hapa nchini, imetoa msaada wa kiasi cha Sh bilioni 71.6.

Hata hivyo, wadau wa kilimo hicho wamesema ili kiweze kuleta tija na kuchangia zaidi pato la taifa, ni muhimu kuwepo na sera pamoja na sheria rafiki hususani kwenye masuala ya ukusanyaji wa kodi kutokana na zao hilo.

Akizungumza Dar es Salaam, Hanta Rwegashora kutoka Kampuni ya Miti ya Mitiki ya Kilombero Valley Teak Company (KVTC), alisema ipo haja ya kurekebisha sheria na sera za kilimo cha miti ya kibiashara. Alisema sheria zilizopo sasa zimejaa urasimu ambao unakwamisha kwa kiasi kikubwa kasi ya ukuaji kwa sekta hiyo.

“Sera za sekta hii bado zinatusumbua sisi wadau wa kilimo biashara cha miti. Tunatozwa kodi kwa kila shamba hata kama yapo chini ya kampuni moja,” alisema.

Aliyasema hayo baada ya kusaini msaada  wa Euro milioni 30 (Sh bilioni 71.6) kutoka kwa Serikali ya Finland kwa ajili ya kilimo biashara cha  miti katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.

Msaada huo ni moja ya njia za kusaidia si tu kilimo biashara, lakini pia kuhifadhi mazingira ambapo ukataji miti ovyo umeleta athari kubwa  kimazingira katika baadhi ya mikoa nchini.

Maeneo ambayo msaada huo unalenga  ni pamoja na wilaya za Njombe, Kilolo mkoani Iringa na Bonde la Kilombero mkoani Morogoro, ambapo makampuni yanayojishughulisha na ununuzi wa miti na utoaji elimu ya upandaji miti bora kwa wakulima wadogo na utengezezaji mbao na bidhaa zitokanazo na miti ya KVTC na New Forest Company (NFC), yalisaini makubaliano ya msaada huo.

Kampuni ya kimataifa ya NFC ina matawi yake nchi za Rwanda, Uganda, na Tanzania. Kampuni hiyo  imekuwa ikiwezesha wakulima wadogo katika ulimaji wa kisasa wa miti aina ya Mikaratusi  (Eucalyptus) na Mitiki (Pine)  ambapo tangu mwaka 2010, mradi huo ulipoanzishwa, jumla ya ekari 5,000 zimepandwa, asilimia 50 ya ekari hizo ikiwa ni miti aina ya Mikaratusi na asilimia 50 iliyobaki miti aina ya Mitiki.

“Pamoja na kufanikiwa kulima miti mingi, kampuni imekuwa ikisaidia wakulima wadogo walio na mashamba kwa kuwapa ujuzi wa kilimo cha kisasa. Hadi sasa, kiasi cha Dola za Marekani milioni 13.8  zimetumika kwa elimu  na utoaji mbegu bora za miti kwa wakulima wa maeneo ya Kilolo na Njombe na hivyo kuwainua kiuchumi,” alisema  Mwakilishi wa Kampuni ya KNC, Agrippa Mandiwona.

 Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa kusaini makubaliano ya msaada huo, Balozi wa Finland nchini Tanzania, Pekka Hukka, alisema nchi hiyo imekuwa na mahusiano mazuri na Serikali ya Tanzania hasa katika suala la uhifadhi wa mazingira kwa kuhakikisha zoezi la upandaji miti linakuwa endelelvu kwa manufaa ya kizazi cha baadaye.

Alisema kupitia kilimo biashara cha miti, Tanzania inaweza kujiinua kiuchumi iwapo itatilia mkazo kilimo cha kisasa hasa kwa kuwasaidia wakulima wadogo.

“Iwapo Tanzania itajikita zaidi katika sekta ya kilimo cha miti, inaweza kuinua uchumi wake kwa kiasi kikubwa kama ilivyo kwa Finland ambayo historia ya ukuaji ya uchumi wake ni pamoja na sekta hiyo  ambayo imekuwa ikipewa kipaumbele kwa miaka 150 iliyopita,” alisema balozi Hukka.

Aliongeza kuwa mazingira mazuri ambayo wakulima hao wanatakiwa kusaidiwa ni pamoja na uundwaji wa sera na sheria rafiki ambazo zitawahakikishia wakulima kupata soko la uhakika kuongeza thamani ya bidhaa zao na hivyo kuweza kushindana katika soko la kimataifa.

“Ikumbukwe kuwa, nchi nyingi duniani  zinazojihusisha na kilimo hiki zimekuwa na sera nzuri za kusaidia wakulima hasa wadogo. Kutokana na hili, zimefanikiwa kwa kiasi kikubwa,” aliongeza.

Balozi huyo alisema  jambo la muhimu kwa sekta ya misitu kukua ni kuwepo kwa ushirikiano mzuri kati ya Serikali na wakulima  haswa wadogo wadogo  kwa kuwasaidia na kuwawekea mazingira mazuri ya uendeshaji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles